Matukio yanayosubiriwa hafla ya Simba Day
Uwanja wa Uhuru umebakiza hatua chache kujaa kutokana na mashabiki wengi kuendelea kuingia tayari kwa kushuhudia kilele cha Simba Day.
Hata hivyo, wakati mashabiki wakiendelea kuingia, kuna matukio yanasubiriwa na mashabiki wengi waliofika uwanjani hapa.
AHMED ALLY ATAINGIAJE?
Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally amekuwa sehemu ya kivutio kwenye staili yake ya kuingia uwanjani kwenye tamasha kama hili.
Ahmed amekuwa akichagiza kwamba safari hii anaingia kwa kupaa na ungo.
Mashabiki wanasubiri kuona msimu huu ataingia kwa mtindo upi na kuendelea kujizolea mashabiki wake wengi kwa ubunifu wake.
SHOO YA ALI KIBA
Msanii mkubwa wa tamasha hili ni Ali Kiba akiwa anapata nafasi hiyo kwa mara ya pili mfululizo na leo anasubiriwa kuona burudani yake itakuwa na vitu gani.
Tayari kuna jukwaa kubwa limejengwa pembeni kidogo ya mpaka wa Uhuru na ule wa Benjamin Mkapa, hapo ndipo Kiba atashusha shoo yake na mashabiki wa Simba ambao wameshakuwa watu wake wa nguvu wanamsubiri kukonga nyoyo zao.
MIAKA TISINI INA KIPI?
Simba Day ya msimu huu inabeba pia maadhimisho ya klabu hiyo kufikia miaka 90 tangu kuzaliwa kwake na sasa mashabiki wanasubiri kuona uongozi wa klabu hiyo utakuwa na matukio gani ambayo yataacha kumbukumbu hiyo ikielezwa kwamba zipo tuzo tofauti zitatolewa kwa viongozi na mashabiki.
WACHEZAJI WAPYA
Simba msimu huu imesajili wachezaji sita ambao ni Nathaniel Chilambo, Kelvin Nashon, Ibraheem Jabaar, Keletso Makgalwa, Bakari Msimu, Ibrahim Doumbia na kipa Ahmed Issa ambaye anaweza kuwa sapraizi baadaye.
Ndani ya usajili huu mpya wa msimu ujao, mashabiki wa Simba wanasubiri kuona ni mchezaji gani atakuwa na kitu kitakachowapa matumaini mashabiki wa timu hiyo wakati watakapocheza dhidi ya Kenya Police kwenye mchezo utakaopamba sherehe hizo.
SAPRAIZI
Mashabiki wa Simba kiasi fulani ni kama hawajashtuka sana na usajili wa msimu huu wakiona kama wachezaji wengi waliosajiliwa kwa msimu ujao ukilinganisha na mtani wao Yanga wakiwa na staa mkubwa kama Peter Shalulile.
Kama kuna kitu kitawafurahisha Simba ni kutangazwa kwa sapraizi yoyote lakini hata hivyo labda iwe kwa mchezaji wa ndani kwani, timu hiyo haitakuwa na nafasi ya kuingiza mchezaji wa kigeni.
Simba haikusajili sana kutokana na msimamo wa kocha wao, Steve Barker ambaye ametaka kutosajiliwa kwa idadi kubwa ya wachezaji wapya akitaka kuongezewa nguvu pekee kwenye timu.