Matola -8: Mapokezi Simba Dar yaua shabiki mmoja

KATIKA mwendelezo wa makala iliyotokana na mahojiano maalumu na nyota za zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na timu kadhaa ikiwamo Simba na Taifa Stars, Seleman Matola tuliona namna kikosi kizima cha timu hiyo kilivyohamishwa kambi.
Hii ilitokana na wenyeji wao kuwaweka video za picha za ngono sambamba na kuwafanyia fujo kisha wakati wa mechi yao ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri waliokuwa watetezi wa michuano, alivyokabidhiwa straika wa kumbana asiwasumbue.
Nini kilichoendelea kwenye mchezo huo? Endelea naye kwani Matola anafichua jinsi Simba ilivyowazima Waarabu hao na kushindwa kuamini na kuliamsha mtiti wa aina yake uwanjani!
REFA AWANYIMA WAARABU BAO
Anasema mechi ilianza kwa kasi kubwa sana, mashabiki walikuwa wanapiga kelele kiasi kwamba uwanjani tu walikuwa hawasikilizana kwani kelele zilikuwa kali sana.
“Nakumbuka waamuzi wa ule mchezo walikuwa wanatokea Morocco, jamaa walianza kwa kutushambulia sana, walikuwa wanakuja kama mvua, yule jamaa niliyepewa nimkabe niliamua kumchezea ubabe, kila akigusa mpira namvaa nachukua mpira nasikia Talib nje ananimbia safi sana Matola, tena.
“Nilimnyima raha sana jamaa, akawa anahama namba naenda naye, jamaa wakaanza kucheza kibabe nao lakini kwa sasa wakawa wanatumia mipira mirefu, nakumbuka dakika kama ya 25 hivi, walipiga krosi, Alex akapiga kichwa akajifunga, tukajua kila kitu kimeisha, ghafla tukaona mwamuzi wa pembeni kanyanyua kibendera, fujo zikaanza wakamfuata wote, mwamuzi akasema kabla mpira kumfikia Alex, ulitoka nje kidogo hivyo bao sio halali.
“Kwa mara ya kwanza niliona haki ikitendeka ugenini, jamaa walikasirika sana tukaenda mapumziko 0-0, wale mashabiki waliokuwa wanashangilia muda wote uwanjani walitulia kimya, mwanzo walijua kuwa wangekuwa wameshatupiga labda bao nne, mashabiki walianza kusimama kinyonge, nasi tukasema hapa hapa tushikilie.
“Tulipokwenda mapumziko sisi tulikuwa na morali kubwa kuliko wao kwa kuwa nyumbani tulishashinda bao 1-0, mapumziko makocha walikuja wakiwa na furaha, lakini wakatupa tahadhari kubwa kuwa tusipokuwa makini mambo yanaweza kubadilika, walitupa mbinu mpya, tukawa tunalinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza.”
KASEJA AGEUKA SHUJAA
Tukiwa tumekaa anaibuka shabiki, anafurahi sana kumuona Matola, anamuomba apige picha na familia yake, ni mtu mzima flani hivi, anakatisha mazungumzo yetu kwa kuwa anaanza kuongea yeye:
“Unajua mimi naipenda sana Simba, kuanzia nikiwa mdogo, baba yangu alikuwa ananipeleka uwanjani, enzi hizo wanacheza kina Abadallah Kibadeni siyo ninyi wa sasa, wale jamaa walikuwa wanajua sana, Matola unamkumbuka Hamis Gagarino, alikuwa anapiga mashuti sana, vipi hivi Iddi Pazi siku hizi yuko wapi?. Inabidi nimwite pembeni na kumuomba aondoke, vinginevyo tungekesha hapo.
Matola anacheka, namuomba aendelee, anaendelea: “Basi kipindi cha pili tunaingia uwanjani tukiwa tunajiamini sana, golini kwetu alikuwepo Juma Kaseja, Tanzania imebarikiwa kuwa na makipa bora sana, Kaseja ni kati ya makipa wenye uwezo mkubwa sana kuwahi kutokea hapa nchini, ile mechi aliokoa sana, mwanzo walimuona mdogomdogo wakafikiri ni kipa wa mchezo, lakini walipiga kila engo akawa anasafiri.
“Zikiwa zimebaki dakika tano hivi mchezo umalizike, jamaa walisawazisha bwana wakafunga bonge la bao, uwanja mzima uliamka kwa furaha mashabiki walishangilia sana na jamaa nao wakawa wamepagawa, kwa kuwa hawakuwa wanaamini, tulianza kupata hofu, tukasogea kwenye benchi letu tukaambiwa kazi haijaisha zimebaki dakika tano lazima tupambane, hapo sasa jamaa wameamka wote majukwaani wanashangilia na wachezaji wao uwanjani wanahimizana kupambana kufa na kupona.”
KIPA ATOLEWA, ALIAMSHA BALAA
Anasema wakati mpira ukiwa kati wanataka kuanza kibao kilinyanyuliwa na kipa wao Zamalek namba moja alitakiwa kutoka ili aingie kipa mtaalamu wa penalti.
“Yule kipa aligoma kutoka, alikataa katakata, alianza kupiga magoli teke, walipomlazimisha alipiga teke kila kitu kilichokuwa mbele yake akavunja mageti ya kuingia vyumbani, yaani jamaa alifanya vurugu kubwa sana utafikiri kachanganyikiwa, mwisho tuliendelea kucheza lakini bado jamaa walikuwa wa moto sana dakika tano zikaisha mechi ikamalizika tumefungwa bao 1-0, kwa kuwa tulishinda kwetu 1-0 tukaenda kwenye matuta.”
SIMBA YAKOSA PENALTI MBILI
Matola anaomba tupumzike kidogo angalau tupate soda, namkubalia, tunakaa dakika tano anaendelea: “Tulipofika kwenye matuta jamaa walitakiwa wao ndio waanze kupiga, kumbuka langoni kwetu alikuwepo Kaseja mmoja kati ya makipa bora sana wa penalti hapa nchini, tuliamini wanaweza kutufunga, lakini Kaseja ataokoa angalau moja ilikuwa kawaida yake.
“Walianza kupiga wakafunga, kwetu akaenda kupiga Steven Mapunda, akakosa, wakaenda kupiga wao wakafunga, akaenda kupiga Said Sued akakosa, jamaa wakaanza kushangilia ushindi.
“Wakaenda kupiga, Kaseja akaokoa, akaenda kupiga Ulimboka Mwakingwe, akafunga, wakapiga ukagonga mwamba, akaenda kupiga Patrick Betwel akafunga, wakapiga Kaseja akaokoa tena, wakaanza kupata hofu, wakalala chini, mashabiki wakatulia, viongozi wao wakanyanyuka, hawaamini kinachotokea, akaenda kupiga Christopher Alex, akiwa anajiamini sana, alikuwa kati ya wachezaji mahiri sana, hakuwa na papara, akapiga bonge la penalti akafunga. Tukafuzu.”
VURUGU KUBWA UWANJANI
“Baada ya pale wakati tunaanza kushangilia, zilizuka vurugu kubwa sana tukachukuliwa na kufungiwa chumbani, jamaa walifanya fujo kubwa sana, walirusha mawe, walivunja viti majukwaani, walivunja mageti yaani kulikuwa na vurugu kubwa sana.
“Tulifungiwa kwenye chumba kwa saa nne bila kutoka, walinzi walituambia tunatakiwa kukaa kimya kwa kuwa jamaa wanaweza kutudhuru sana, walikuwa na hasira haswa, hata kombe lao sikumbuki kama walipewa, baada ya saa nne tulipelekwa hotelini na magari manane ya jeshi gari letu lilikuwa katikati ya jeshi yakapita pembeni yetu tukapelekwa hadi hotelini, tukakuta pia ulinzi mkali.
“Viongozi walifurahi sana, walifika hotelini wakiwa na furaha, ukweli ilikuwa rekodi, wengine mpaka machozi yalikuwa yanawatoka kwa furaha, tulilala kesho yake tukaenda shooping.”
MASHABIKI AL AHLY WAISHANGILIA
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Vijana ya Simba B, anasema kesho yake walipewa ruhusa ya kwenda kwenye maduka makubwa pale Cairo kwa ajili ya kununua baadhi ya vitu, walikutana na mashabiki wa Al Ahly, waliwapongeza sana na kuwaambia wamewafunga mdomo wapinzani wao.
“Jamaa walifurahi kila tulipokuwa tunakutana nao walituona mashujaa, unajua pale jamaa walikuwa hawajafungwa muda mrefu sana, hivyo tulionekana wanaume haswa, tulipokuwa tunakutana nao walikuwa wanatushangilia na kutusifu na sisi tulitembea kibabe haswa, lakini jambo la ajabu ni kwamba mji ulikuwa umetulia sana, hakukuwa na watu kabisa kwa kuwa wakati huo, Zamalek ndiyo walikuwa na mashabiki wengi zaidi pale Misri.”
MAPOKEZI DAR YAUA MASHABIKI
Matola anasema wakiwa wanajiandaa kuondoka, Talib aliwaweka kikao akiwa na Siang’a na kuwaeleza yale waliyofundishwa wayashike, hiyo ni hatua moja tu bado mbele kuna safari kubwa zaidi ya mafanikio, lakini anarudia kusema, Talib aliwasaidia sana kugundua mbinu za Waarabu.
“Sikumbuki kama Talib tulikuja naye, lakini nafikiri misheni yake iliishia pale akaelekea Oman na yupo huko hadi sasa, baada ya pale tuliondoka tukaenda Uwanja wa Ndege na kurejea Dar es Salaam kibabe.
“Tulifika uwanja wa ndege tukawa tunashangaa, chini tulikuwa tunaona vitu kama maua tukawa tunalizana nini, kumbe walikuwa mashabiki wameshajaa uwanja wa ndege hakuna hata sehemu ya kukanyaga, walikuwa wengi sana, kwa wanaofahamu uwanja wa ndege hapa Dar watanielewa, hakukuwa na nafasi hata kidogo.
Anavuta pumzi, anapiga simu anaongea na mtu, anamwambia amsubiri kwenye gari nje. Anaendelea: “Ulinzi ulikuwa mkubwa sana uwanjani, ukweli tulipokelewa kishujaa, tulikuwa na gari la wazi na tulielezwa kuwa tunatakiwa kwenda Uwanja wa Uhuru tutapokelewa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
“Nakumbuka gari lilikuwa halitembei kwa kuwa mashabiki walikuwa wengi, wengine wanasukuma wengine wamepanda kwenye magari, wamekosa nafasi wamekaa juu, kila baada ya muda tuliona watu wengine wakifariki baada ya kushika au kupita kwenye nyaya za umeme na kupigwa shoti wakiwa juu ya magari kama fuso na mengine, sikumbuki walifariki watu wangapi lakini walikuwa kadhaa na majeruhi wengi sana.
“Tulifika uwanjani tukakuta uwanjani umejaa sana, Mwinyi alikuwepo pale akatupokea lakini rangi iliyokuwa inatawala uwanjani ni nyekundu tupu, siwezi kusahau tukio hili.”