Matola -11 : Mimi ni bosi wa vijana Simba
JANA tuliona Kocha Msaidizi wa Simba, Suleimani Matola akizungumza kuhusu jinsi ambavyo wamekuwa wakijiandaa na michezo dhidi ya Yanga, alizungumza kuhusu mabadiliko ambayo yapo kwa sasa na jinsi ambavyo wanaona soka kwa sasa linaendeshwa kisasa zaidi kuliko hali ilivyokuwa huko nyuma.
Lakini Matola anazungumzia tageti zake kuwa ana uhakika wa kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika miaka ijayo, amerudi mara mbili hadi tatu kusema kauli hiyo na kusema hajafahamu atakuwa na timu gani wakati huo, lakini ana uhakika kuwa atafanikiwa kufanya hivyo kwa kuwa anaona kuwa baada ya kusoma atakuwa ameshalifahamu sana soka la Afrika lilivyo.
Lakini pia amezungumza kuhusu ukubwa wa Simba na kusema kuwa ni timu kubwa ambayo imekuwa ikifanya mambo makubwa kwa ushirikiano wa hali ya juu, huku akiamini baada ya miaka miwili timu hiyo itakuwa na mafanikio makubwa zaidi kwenye soka la Afrika.
TIMU ZA VIJANA ZA LIGI KUU
Matola anasema maendeleo ya soka yanaanzia kwenye timu za vijana ni vyema timu nyingi zikawekeza kwenye soka la vijana, ili kuhakikisha zinakuwa na timu bora hapo mbele lakini pia inasaidia kutengeneza timu bora ya taifa.
“Ukweli soka la vijana haliepukiki, lazima tuwe na utaratibu mzuri wa soka la vijana, unajua nilianzia kupatia umaarufu huko, hawa kina Ndemla, Jonas Mkude, kina Ajibu Ibrahim walianzia kwenye soka la vijana na kukua taratibu na leo wana maisha yao kwenye soka la Tanzania.
“Nchi nyingi zimeendelea baada ya kuwa na mfumo mzuri wa soka la vijana, hivyo nafikiri ni jambo ambalo haliepukiki lakini wakati mwingine linapunguza sana matumizi kwenye timu kwa kuwa unamsajili mchezaji wako mwenyewe, unachofanya ni kumpandisha tu juu na kuhakikisha kuwa anakuwa na ubora uleule au zaidi.
“Sina shaka na mfumo ambao Simba inao, ni moja kati ya timu ambayo inajali sana soka la vijana, linaweza lisiwalipe leo, lakini baada ya miaka kadhaa litakuwa na faida kubwa sana kwao.
KUMBE SASA NI BOSI WA VIJANA
“Kwa sasa nasoma na watu wote wanafahamu, lakini cheo changu sasa Simba ni msimamizi wa soka la vijana wa Simba, nakuhakikishia baada ya muda mchache kutakuwa na mabadiliko makubwa naamini kwa kushirikiana na makocha ambao wapo tutafanya jambo kubwa.
“Tanzania kuna vijana wengi wanajua soka, lakini wanatakiwa kuendelezwa, tunatakiwa kufanya jambo hilo kwa pamoja, kila mtu anatakiwa kuwashika mkono vijana kuhakikisha kuwa wanakuwa bora zaidi.
“Mara nyingi hata uswahilini huwa naenda kutazama mazoezi, nikiwa nyumbani naweza kutoka nikaenda sehemu na kuangalia mazoezi hata wengine hawanifahamu lakini nafurahi tuna kuona vijana wanacheza na huko kuna wachezaji wengi sana ambao wakiendelezwa baadaye watakuwa mastaa wakubwa, nakuhakikishia nchi hii ina wachezaji bora.
LIPULI YAICHAPA YANGA
Matola anasema alipata mafanikio akiwa na Leseni C ya ukocha, lakini baada ya kuanza kusoma amejifunza mambo mengi zaidi yanayoweza kuusaidia mpira wetu kusonga mbele.
“Nilipata mafanikio nikiwa na Lipuli, ile ilikuwa timu kweli nafikiri kila mmoja anaikumbuka, nakumbuka nilikuwa kocha wa mwanzo mwanzo mzalendo kufika fainali ya Kombe la FA, tukafungwa na Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Ilulu pale Lindi.
“Lakini ubora wa timu hiyo ulichangiwa na ubora wa wachezaji waliokuwepo, hatukufika fainali kwa bahati mbaya, nakumbuka Jumamosi tuliichapa Yanga kwenye ligi na siku tatu mbele tukawachapa tena kwenye FA, Yanga walikuwa na timu bora, lakini wakati ule Lipuli tulikuwa na kikosi imara zaidi, baadaye nilienda Polisi napo tukawa na timu bora na kurudi Simba.
FAIDA YA KUSOMA MAKOCHA
Matola anasema alienda shule kwasababu muda umefika, alisema makocha wanatakiwa kusoma kwa kuwa soka la sasa limekuwa la sayansi zaidi kocha asiposoma utaachwa nyuma.
“Nafikiri kabla mwaka huu haujamalizika nitakuwa nimemaliza kozi yangu, nitakuwa na leseni yangu na itakuwa siku ya furaha sana kwangu, watu waelewe nasomeshwa na Simba, lakini nataka kukuambia kwenye dunia ya sasa, makocha ni lazima tusome, siyo kusoma leseni tu, lazima tufahamu mambo mengi kutoka na dunia kubadilika na soka kuwa tofauti bna zamani.
“Ukitazama mimi nasoma leseni A ya Caf, lakini wakati huohuo najiongeza kwa kusoma lugha na kompyuta kwa kuwa huko mbele ni vitu ambavyo vinatakiwa viwepo kwa makocha, tazama leo tuna wachezaji wengine wanatoka Ulaya, wengine Congo, Afrika Kusini na sehemu nyingine, lazima tuwe tunafahamu lugha wanazoongea, kama hujui itakusumbua sana.
“Mimi pamoja na kwamba Kiingereza nilikuwa nafahamu lakini kuna vitu lazima niviongeze, nasoma pia Kifaransa ili niweze kwenda sawa na maendeleo ya soka yalivyo.
“Napenda kuwashauri makocha kujiendeleza, sisi tuna makocha bora sana lakini wakipata nafasi wajiendeleze hii itatusaidia sana huko mbele, naamini baada ya muda tutakuwa kwenye viwango bora sana kama tutakubali kusoma.