Matola -10 : Mechi za Yanga sio mchezo

JANA tuliishia sehemu ambayo Matola anaeleza jinsi Simba ilivyoondolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, akikiri kwamba kundi lao lilikuwa dume kwelikweli kutokana na timu ilizopangwa nazo, Ismailia ya Misri, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Enyimba ya Nigeria ambayo kipindi hicho ilikuwa bora sana na ilikuwa na mastaa wengi. Enyimba ndio iliyobeba taji la msimu huo baada ya kukutana na Ismailia kwenye fainali na kushinda jumla ya mabao 2-1, Wanigeria wakishinda nyumbani 2-0 na kulala ugenini 1-0.
Endelea naye kwenye simulizi hii iliyotokana na mahojiano maalumu aliyofanya na Mwanaspoti na kujua nini kiliendelea. Tiririka nayo...!
KUNDI DUME
Matola anakiri kundi lao lilikuwa gumu haswa na ndio maana haikushangaza timu zilizofuzu mbele yao, yaani Enyimba na Ismailia kuja kukutana tena kwenye mechi ya fainali na Wanigeria waliokuwa moto kwelikweli enzi hizo kubebea ndoo.
Anasema pamoja na kwamba walifanya vizuri kwenye baadhi ya michezo ikiwemo kuwafunga Asec Mimosas na Enyimba bado hawakuweza kufuzu kwa hatua illiyofuta.
Juu ya mechi asiyoisahau kwenye hatua hiyo ya makundi kwa mwaka 2003, Matola anaitaja ile ya mwisho ya kundi hilo iliyopigwa ugenini dhidi ya Asec Mimosas.
Anasema ni mchezo ambao hawezi kuusahau kwa vile Simba ilikuwa inahitaji ushindi wa mabao 2-0 tu na kuisikilizia mchezo wa Enyimba na Ismailia zilizokuwa ikimalizana Nigeria, kwani kama Wanigeria wangelala kwa Ismailia na Simba kushinda zingefuzu pamoja, kwa vile kabla ya mechi hizo Ismailia ilikuwa ikiongoza Kundi na pointi 11, ikifuatia Enyimba iliyokuwa na pointi tisa na Simba ikiwa na saba, wakati Asec ikiburuza mkia na alama moja tu mkononi.
Matola anasema kwa bahati mbaya Simba ikafungwa mabao 4-3, wakati Enyimba ikiizidi akili Ismailia kwa kuifumua mabao 4-2 na kumaliza kama kinara, ikifuatiwa na Wamisri, kisha Simba kusaliwa na alama saba na Asec kumaliza mkiani na pointi nne.
MAKOMBE YA SIMBA
Baada ya michuano hiyo, Simba ilirudi nyumbani na kuwasha moto kwelikweli kwani ilikuwa kwenye kiwango cha juu na kutesa kwenye ligi kati ya 2000-2005.
“Miaka hii ya 2000, ndiyo soka lilianza kuwa kama biashara kubwa, wachezaji walianza kupata hela hapa hata bingwa naye alianza kulipwa hela nzuri. Nakumbuka maisha ya wachezaji wengi yalianza kubadilika na hata usajili ulikuwa unafanyika wa hela nyingi na wachezaji walianza kutoka mataifa makubwa kuja hapa nchini.
Wachezaji walianza sana kuendesha magari mazuri kuanzia kipindi hiki lakini pia wale waliokuja kutoka nje nao walitufundisha wengine maisha, kwa kuwa walishaenda nje na kuanza kuja mazoezini na magari makali. Sina maana kuwa huko nyuma walikuwa hawaji na magari hapana sasa kasi iliongezeka zaidi.
MECHI ZA YANGA KIBOKO
Matola anasema upinzani wa Simba na Yanga hauwezi kumalizika hata kidogo kwa kuwa ni utamaduni ambao upo kwa miaka mingi na wenyewe waliukuta.
Maandalizi ya Simba na Yanga hayajawahi kuwa sawa na unapojiandaa na timu nyingine kwa kuwa mechi hii ni kubwa sana, huwa ni mchezo ambao unachukua hisia za watu wengi sana. Mashabiki wa soka kuanzia kipindi cha nyuma walikuwa wanakuja nchini kutoka nchi majirani kutazama mechi za Simba na Yanga.
“Hata bungeni kumekuwa na utaratibu wa mechi za Simba na Yanga wanacheza hii yote inaonyesha ukubwa wa mchezo huu,” anasema ilikuwa kawaida kwenda mbali na Dar kuweka kambi kwa kuwa kwanza timu zilikwepa hujuma na zilihitaji maandalizi sahihi.
“Tazama mfano sisi tulikuwa tunacheza michuano ya kimataifa lakini lilipokuwa linafika suala la mechi ya Yanga mambo yalikuwa yanabadilika kabisa, maandalizi yalikuwa tofauti na akili za viongozi kuhusu mechi hii zilibadilika.
“Nafikiri sasa hivi kidogo hali ni tofauti unaona timu inakaa kwenye kambi yake ya kawaida wakati inajiaandaa na mchezo huu, nafikiri ni mabadiliko makubwa sana na ni vyema tukaendelea hivyo.”
MATAJI AKIWA NA SIMBA
Matola anasema anaweza kuwa mmoja kati ya wachezaji wa Simba waliotwaa makombe mengi zaidi kwa kipindi anacheza Simba ingawa anaamini kuwa wengine watakuja kutwaa makombe mengi likiwemo la Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Nimetwaa makombe mengi sana nikiwa na Simba, lakini ninachosikitika ni kwamba sikupata nafasi ya kutwaa Klabu Bingwa Afrika.
“Kwenye makombe ya ligi sina shaka kuwa nimefanya vizuri nafikiri sana yanafika... Ukitazama kuanzia 2000 tu hadi 2006 nimetwaa makombe kama sikosei ni manne. Lakini jambo ambalo nilikuwa nalitamani kwa muda mrefu lilikuwa ni kutwaa ubingwa wa Afrika ambao sikupata nafasi ya kufanya hivyo kama mchezaji.
“Lakini nataka kukuambia leo, hifadhi maneno yangu kuna siku nitatwaa ubingwa wa Afrika nikiwa kocha. Naomba Mungu nimalize shule salama, nakuhakikishia kuna siku sijafahamu ni lini lakini hilo litatokea.
“Nimekaa kwenye hili soka la Afrika nimeona mambo mengi, nakuambia hii Simba unayoiona inafika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika viongozi wake wanafanya kazi kubwa sana, siyo jambo rahisi kufikia hapo wanapofikia kuna kazi kubwa sana wanakuwa wameifanya.
“Na kama wataendelea hivyo, mipango ikaendelea kufanyika hivi nakuambia miaka miwili au mitatu Simba watakuwa mabingwa wa Afrika, kwa sasa kila timu Afrika inaiogopa Simba siyo kwa kuwa inaitwa Simba ni kwa kuwa imeshafanya mambo makubwa Afrika, wapeni muda utaelewa hili ninalosema leo.
“Kila mtu anatakiwa kuelewa siyo kazi rahisi, soka la Afrika limekua sana kwa sasa. Nimeenda nchi zote kubwa za kisoka hapa Afrika nimeona mambo mengi, Simba wapewe muda watafanya jambo la kuushangaza ulimwengu huu.
“Kuna timu zinasajili wachezaji wakubwa wanalipwa mishahara mikubwa ukielezwa unashangaa. Huko ndiyo tunakwenda tuwe na subira. Soka la Tanzania linakua kwa kasi kubwa lakini kila mmoja lazima amuunge mwingine mkono.
ITAENDELEA KESHO