Mathias Lule atua Mbeya City

Muktasari:
- Mchakato wa kumpata kocha huyo ulianza kwa zaidi ya wiki tatu zilizopita ambapo uongozi ulipokea maombi ya makocha 14 wenye leseni A waliomba, Watanzania wanne wakati makocha wa kigeni walikuwa 10.
UONGOZI wa Klabu ya Mbeya City imemtangaza kocha Mathias Lule ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes' kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukuwa nafasi ya Amri Said 'Stam'.
Mchakato wa kumpata kocha huyo ulianza kwa zaidi ya wiki tatu zilizopita ambapo uongozi ulipokea maombi ya makocha 14 wenye leseni A waliomba, Watanzania wanne wakati makocha wa kigeni walikuwa 10.
Makocha walioomba nafasi kuifundisha timu hiyo ni kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Ureno, Mexico na Italia pamoja na Tanzania.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel imbe alisema Lule atawasili nchini leo Alhamisi ambapo atakwenda moja kwa moja jijini Tanga ambako timu hiyo itacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
"Amepewa mkataba wa miaka miwili, atawasili kesho (leo) na kujiunga moja kwa moja na timu huko Tanga. Bodi ya klabu iliunda kamati maalumu kupitia maombi na wasifu wa makocha waliokuwa wameomba kazi.
"Walikubaliana kwa pamoja kumpitisha Lule ambaye ni kocha wa timu ya Taifa ya Uganda na ndiye aliyeifikisha katika michezo ya mataifa ya Afrika (AFCON) iliyofanyika nchini Misri," alisema Kimbe
Moja ya kazi kubwa atakayotakiwa kuifanya Lule ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kuondoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
...................................
Na Mwandishi wetu