Manchester United ilivyochomoa dili la Neymar kuhofia matanuzi yake
Muktasari:
Katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto Neymar alikuwa amepania kuondoka PSG na kurudi Hispania ambako alikuwa akihusishwa kurudi katika klabu yake ya zamani, Barcelona huku pia akihusishwa kwenda kwa wapinzani wao Real Madrid.
MANCHESTER ,ENGLAND . IMEBAINIKA kwamba Manchester United walikuwa tayari kuitingisha dunia katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto kwa kutoa kiasi kikubwa cha pesa kumchukua staa wa kimataifa wa Brazil, Neymar kutoka PSG.
Ghafla wakashtuka. Wakamtafakari zaidi Neymar na kugundua kwamba kama wakimchukua watapata tabu sana. Inadaiwa kwamba mabosi wa United waliamini kwamba Neymar ni mchezaji ambaye anakosa umakini na kazi yake licha ya kuwa na kipaji kikubwa.
Hapo hapo walikuwa na wasiwasi na tabia ya baba yake Neymar Snr, ambaye anajulikana kwa tabia yake ya kupenda pesa, huku mara nyingi akifurahia kumhamisha mwanaye na kuvuna kiasi kikubwa cha pesa.
Neymar Snr ndiye aliyesimamia dili za mwanaye kutoka Santos ya Brazil kwenda Barcelona mwaka 2013 ambapo alilamba dau kubwa la pesa, lakini pia akasimamia dili wakati alipohama Barcelona na kuhamia PSG mwaka 2017 kwa dau la Pauni 198 milioni lililovunja rekodi ya uhamisho ya dunia. Katika dili hilo mzee Neymar Snr pia alivuta kiasi kikubwa cha pesa.
Katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto Neymar alikuwa amepania kuondoka PSG na kurudi Hispania ambako alikuwa akihusishwa kurudi katika klabu yake ya zamani, Barcelona huku pia akihusishwa kwenda kwa wapinzani wao Real Madrid.
United ilikuwa miongoni mwa timu ambazo zilikuwa na uwezo mkubwa wa kifedha wa kumnasa staa huyo wa Brazil, lakini inaonekana kwamba waliamua kuachana na mpango huo baada ya kukerwa na tabia za baba yake Neymar, pamoja na mchezaji mwenyewe.
Mwandishi Daniel Taylor wa Gazeti la The Athletic anadai kwamba Neymar alikuwa katika anga za United kwa sababu aliwekwa katika kipengele cha kwanza cha mchezaji mzuri (A genuine, category-A superstar) huku bosi mtendaji wa United, Ed Woodward akiamini kwamba walikuwa wanahitaji kumnunua walau mchezaji mmoja ambaye yupo katika nafasi ya kuwania tuzo za Ballon d’Or.
Hata hivyo, kulikuwa na kundi la mabosi wa klabu hiyo ambao walikuwa na wasiwasi na aina yake ya maisha ya kujirusha pamoja na kukosa umakini katika maisha yake ya soka nje ya uwanja.
Taylor anaandika, “Old Trafford kuna utani ambao unaendelea klabuni. Huwa wana msemo wao ‘Kama una Mbrazil mmoja, basi una Mbrazil mmoja, kama una Wabrazil wawili, basi una Wabrazil wawili, kama unao watatu basi una sherehe ya Samba’. Katika suala la Neymar, United walikuwa wanaamini ingekuwa ni suala la Neymar kumimina Vodka yenye malimao katika glasi kila wakati.”
Hakuna siri kwamba Neymar amekuwa akifurahia maisha ya kujirusha zaidi. Mara zote amekuwa akitoka usiku akiwa na mastaa mbalimbali wakubwa ambao ni marafiki zake, lakini pia amekuwa akijitokeza katika shughuli kubwa kubwa za kifahari.
Katika mtandao wake wa Instagram ambao una wafuasi 127 milioni, Neymar amekuwa akiposti picha akiwa na mastaa mbalimbali wakubwa duniani akijirusha nao kama vile Lewis Hamilton, Rihanna na Drake. Lakini pia amekuwa katika matukio na mastaa wenzake wa PSG kama vile Kylian Mbappe na pia amekuwa akionekana na wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona.
Mei mwaka huu, katika tabia yake ya mwendelezo wa matanuzi Neymar alijikuta matatizoni baada ya mwanamitindo mmoja wa Brazil, Najila Trindade kudai kwamba mwanasoka huyo alimbaka katika hoteli moja jijini Paris.
Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa na ofisi ya mwendesha mashtaka jijini Sao Paulo nchini kwao Brazil kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukosefu wa ushahidi kutoka kwa dada huyo na hiyo ilikuwa nafuu kwake ambapo mara zote alisisitiza kwamba hana hatia.
Staili yake ya kujirusha imekuwa ikizua matatizo kwa klabu nyingine kama vile ile yake ya zamani, Barcelona. Tayari alimuingiza katika matatizo staa mwenzake wa Brazil anayekipiga Barcelona, Arthur Melo ambaye alikwenda nje ya muda.
Melo pia alilazimika kuomba msamaha kwa Barcelona msimu uliopita baada ya kuwa mchezaji pekee wa Barcelona aliyehudhuria sherehe ya kuzaliwa ya staa huyo jijini Paris, ikiwa ni saa 48 kabla ya Barcelona haijacheza pambano la El Clasico na wapinzani wao wa jadi, Real Madrid.
Achilia mbali hilo, wasiwasi mkubwa upo kwa baba yake, Neymar Snr ambaye amekuwa akifanya kazi kama wakala wa mchezaji huyo huku akiwa mhusika mkuu katika mazugumzo yote ambayo yanamhusu staa huyo. Anajulikana kwa kupenda pesa zaidi huku mwanaye akiwa kitega uchumi pekee anachokitegemea katika maisha yake.
Inaaminika kwamba nje ya uwanja, Neymar hana tabia kama za mastaa wawili walio juu, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kujichunga kwa ajili ya kuendelea kuwa juu muda mrefu. Ni kutokana na hilo United waliamua kutoweka ofa yao mezani ingawa walikuwa na dhamira pamoja na pesa. Neymar pia kwa sasa amekuwa akikabiliwa na majeraha ya mara kwa mara. Ni wiki iliyopita tu aliumia tena na anatazamiwa kukaa nje kwa wiki nne.
Hilo limekuwa jambo la kawaida kwa staa huyo wakati katika umri wake Ronaldo na Messi walikuwa hawakabiliwi na majeraha ya mara kwa mara.
Na sasa Neymar ambaye aliumia akiwa katika majukumu ya timu ya taifa atakosa mechi mbili zijazo za PSG katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji na Real Madrid ya Hispania.
Mwaka huu, Neymar aliikosa michuano ya mataifa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa America kutokana na kuumia kifundo cha mguu. Alirudi uwanjani miezi miwili baadaye lakini sasa amepata pancha nyingine.
Januari mwaka huu, Neymar aliumia mfupa laini uliopo chini ya mguu upande wa nyuma (metatarsal) na alikaa nje kwa kipindi cha miezi mitatu.
Hiyo ilikuwa ni mara yake ya tano kuumia mfupa huo. Neymar pia aliumia mguu wake wa kulia kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Russia mwaka 2019.