Makocha wataja tatizo Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Hadi sasa zimechezwa dakika 270 na timu sita bado hazijaonja ladha ya pointi tatu na kuwa katika presha ya kukwepa kushuka daraja huku ugumu wa ligi ukitajwa na makocha.
HAWAJAJIPATA. Ndivyo unaweza kusema baada ya mechi tatu zilizopigwa kwenye Ligi Kuu na baadhi ya timu hazijaonja ushindi wowote ikilinganishwa na msimu uliopita namna zilivyotesa.
Hadi sasa zimechezwa dakika 270 na timu sita bado hazijaonja ladha ya pointi tatu na kuwa katika presha ya kukwepa kushuka daraja huku ugumu wa ligi ukitajwa na makocha.
Yanga inayotetea ubingwa kwa msimu wa sita mfululizo, ndiyo kinara kwenye msimamo ikiwa na pointi tisa, ikifuatiwa na watani zao Simba ambayo haijapoteza mechi yoyote, ikivuna pointi tisa ktika mechi tatu.
Azam iliyomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita ipo nafasi hiyohiyo kwa pointi saba baada ya ushindi wa mechi mbili na sare moja sawa na Geita Gold iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.
Timu ambazo hazijaonja pointi tatu hadi sasa ni TRA United inayoongozwa na kocha raia wa Burundi, Ettiene Ndayiragije na imepoteza mechi moja na sare mbili na kuwa nafasi ya 11 na Pamba Jiji iliyovuna pointi moja.
Pia Dodoma Jiji ambayo ilikuwa uwanjani jana dhidi ya Polisi Tanzania, imekusanya pointi moja sawa na Coastal Union iliyopo nafasi ya 14, Kagera Sugar na JKT Tanzaniainaburuza mkia.
Msimu uliopita, TRA United ilimaliza nafasi ya tano kwa pointi 43, huku JKT Tanzania ikimaliza nafasi ya sita kwa pointi 42, Pamba Jiji nafasi ya saba kwa pointi 36 ikifuatiwa na Coastal Union na Dodoma Jiji.
Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Vicent Mashami amesema ugumu wa ligi na makosa binafsi ya nyota wake ndio imewapa mwanzo mgumu, akitoa matumaini kuwa bado ni mapema na inaweza kufanya vizuri.
“Tunahitaji ushirikiano wa pamoja kwa kuwa bado ni mapema, matokeo haya si mazuri sana na lazima tuamke kupambana kwa kusahihisha makosa, kiwango cha nyota wangu kinaridhisha ni makosa tu binafsi,” amesema Mashami.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amesema ugumu wa ligi na makosa kwenye eneo la beki ndio tatizo lakini hata presha za Championship ndani na nje ya uwanja zimechangia.
“Tutasahihisha makosa haswa eneo la beki, yapo makosa binafsi ambayo yanarekebishika, kimsingi hatujaanza vizuri ila tunao uwezo wa kubadili matokeo,” amesema Kaseja.