Kipa aweka rekodi ya mabao 12 ya Yanga
Muktasari:
- Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi amempongeza kwa kazi aliyoifanya katika mechi iliyopita.
YANGA imeendelea kumchafulia rekodi kipa wa JKT Tanzania, Ramadhan Chalamanda ambaye ndani ya misimu miwili amefungwa mabao 12, huku akitaja sababu za kuruhusu vipigo hivyo.
Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi amempongeza kwa kazi aliyoifanya katika mechi iliyopita.
Chalamanda alitua JKT msimu uliopita, akiwa ni miongoni mwa makipa wazawa ambao wamekuwa na rekodi nzuri lakini kikosi kimoja tu kimeongoza kwa kumtoa nishai mara tatu mfululizo.
Tangu atue amekuwa na bahati mbaya na Yanga kwani ndio iliyoongoza kumfunga mabao mengi, huku akiwa na rekodi ya kukutana nayo mara tatu kwenye mechi za ligi.
Msimu uliopita timu hizo zilikutana mara mbili mechi za ligi, ya kwanza Yanga iliitandika JKT nyumbani mabao 5-0 na ya pili ilichapa tena 0-3 akiwa langoni.
Msimu uliopita Chalamanda alifanya kazi kubwa ya kuzuia mabao na kuisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya tano, Yanga ikiwa kileleni ikifuatiwa na Simba, Azam na Singida Black Stars nafasi ya nne.
Simba katika mechi zake iliifunga mabao 2-1 ya kwanza na ya pili ilishinda bao 1-0 nyumbani. Huku Azam FC ikianza kwa sare 1-1 na kumaliza kwa 3-0 mechi ya pili.
Singida ilipokutana na JKT Tanzania ilipoteza 0-1 mechi ya kwanza na uliofuata iliitandika mabao 2-1.
Katika timu zote nne mkubwa, Yanga imekuwa timu iliyovunja rekodi ya Chalamanda na JKT Tanzania kwa ujumla, ikiongoza kuifunga mabao mengi zaidi ndani ya msimu mmoja. Huku ikionekana kuwa na hesabu za kuendeleza makali hayo hata msimu huu wa 2026/27, baada ya juzi kuichapa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza ikionekana kuwa dhahama ya msimu uliopita inaweza kutokea.
MSIKIE CHALAMANDA
Akizungumza na Mwanaspoti Chalamanda amesema hakuna mchezaji bora anayepimwa kwa mechi moja licha ya kwamba amekuwa na rekodi mbaya na Yanga.
“Tangu msimu uliopita kumekuwa na hiyo changamoto unaweza kusema ni ubora wa wapinzani ingawa yameshapita hayo, kwa sasa natazama zaidi msimu huu.
“Kwenye mechi iliyopita kilichoniangusha sana ni safu yangu ya ulinzi kuna muda ni kama walijisahau na mashambulizi yalikuwa makali huenda tungefungwa mengi zaidi.”
MSIKIE KOCHA YANGA
Akizungumza na Mwanaspoti kocha wa Yanga Manqoba Mngqithi amesema licha ya kuifunga Yanga, lakini kipa huyo alifanya kazi kubwa ya kuisaidia timu hiyo.
“Tungeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi ya huu bahati kwao wana kipa mzuri kama ambavyo nilisema kabla ya mechi yule kijana Chalamanda ni mchezaji mzuri alikuwa na utulivu sana,” amesema Manqoba.