Makata: Mbona bado, subirini muone muziki
Muktasari:
- Polisi Tanzania imerejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kukosa uhondo huo misimu mitatu mfululizo ambayo ni 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026, ambapo imeonekana kuwa ya moto ikivuna pointi nne nyumbani na sasa inajiwinda dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.
KIWANGO walichoonesha nyota wa Polisi Tanzania katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu, zimemuibua Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata, akieleza kuwa bado muziki unaendelea akiwataka vijana wake kutokata pumzi.
Polisi Tanzania imerejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kukosa uhondo huo misimu mitatu mfululizo ambayo ni 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026, ambapo imeonekana kuwa ya moto ikivuna pointi nne nyumbani na sasa inajiwinda dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.
Katika mechi mbili ilizocheza, ilianza na sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam, kabla ya kuikandamiza mabao 2-0 JKT Tanzania na kuwa nafasi ya nne kwa pointi nne, na sasa itakuwa ugenini Agosti 25, 2026 kukipiga na Dodoma Jiji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makata ambaye aliipandisha timu hiyo, amesema matokeo hayo ni mwanzo katika kusaka mafanikio msimu huu, akieleza kuwa kiwango hicho bado hakijafikia wastani anaotaka.
Amesema kutokana na mwanzo huo anauona mwendelezo mzuri akiwapongeza nyota wake na kuwataka kutokata pumzi badala yake kuendeleza moto huohuo ili kufikia malengo yao msimu huu.
“Bado ni mapema lakini vijana wanaonesha kitu, niwapongeze kwa kuzingatia maelekezo lakini wasibweteke, nahitaji kuona moto huu ukiendelea kila mechi, tunayo malengo yetu hivyo lazima tukaze,” amesema Makata.
Kocha huyo ameongeza kuwa, anahitaji kuboresha eneo la ushambuliaji kuongeza makali ili kila mechi wapate japo bao, lakini kurekebisha na kusahihisha makosa eneo la beki kuhakikisha hawaruhusu bao.
Amesema anafahamu ugumu wa ligi, hivyo ili kukabiliana na upinzani lazima waendelee kuonesha ushindani kwa kila mechi kwakuwa timu zote zimeonesha nia ya kuhiatji matokeo mazuri bila kujali nyumbani au ugenini.
“Ninao uzoefu wa ligi, hivyo ugumu wake naujua, lazima tujipange tucheze kwa nguvu kila mechi, timu zinaonesha ushindani kwakuwa kila mmoja anayo malengo yake, hatuchezi cha nyumbani wala ugenini,” amesema kocha huyo.