Maisha ya Sinza maji marefu kwa Atupele
Muktasari:
Ni baada ya Mwanaspoti kupiga hodi nyumbani kwake, maeneo ya Kimara, King’ong’o jijini Dar es Salaam ambapo amepanga katika nyumba moja na yeye akimiliki vyumba viwili vilivyosheheni kila kitu.
UNAMJUA straika wa Ndanda FC, Atupele Green? Basi jamaa kweli ameamua na ana hasira juu ya maisha yake.
Ni baada ya Mwanaspoti kupiga hodi nyumbani kwake, maeneo ya Kimara, King’ong’o jijini Dar es Salaam ambapo amepanga katika nyumba moja na yeye akimiliki vyumba viwili vilivyosheheni kila kitu.
Ameamua kujichimbia katika eneo hilo baada ya kukimbia Sinza, Kumekucha ambako ni katikati ya jiji alikokuwa amepanga hapo awali.
Malengo ya kukimbia huko ni baada ya kuona maisha anaoyoishi nje ya jiji, yamempunguzia gharama kwani alipokuwa huko, alikuwa anakutana na vishawishi vingi na kumfanya aishi maisha ya juu kama gharama za msosi, kodi ya nyumba na mazingira na kampani, alilazimika kufanya matanuzi mbalimbali kama kwenda disko kujirusha. King’ongo anakoishi sasa ni mji ambao umejitenga, uko mbali kidogo na mjini kwenye fujo na anasema, hapo ndiyo sahihi kwake kwa sababu hakuna vishawishi, anapojifungia ndani, hakuna wa kumsumbua zaidi ya kuchezea gemu (play station), pia inakuwa vigumu kufanya safari zisizokuwa na umuhimu kutokana na eneo hilo kuwa nje ya mji.
Kwenye masuala ya msosi, Atupele anasema, urahisi wake ni kwa sababu anaijua sehemu ya kukusanya mazagazaga ya bei chee pale Kimara Mwisho na kwenda kupika mwenyewe, wakati alipokuwa anaishi Sinza, chakula chake chote kuanzia asubuhi hadi usiku kilikuwa cha hotelini.
Mambo ambayo yalichangia afanye maamuzi hayo magumu ni kutunza fedha zake ili atimize malengo aliyojipangia likiwemo suala la kukamilisha nyumba yake anayojenga maeneo ya Chamazi, pia anapopata muda mzuri wa kupumzika, inakuwa rahisi kuimarisha kiwango chake.
Katika nyumba hiyo, anaishi mwenyewe ingawa wakati mwingine, hutembelewa na mchumba wake, Khadija anayesomea Sheria Chuo cha Eckenford jijini Tanga kama alivyokutwa na Mwandishi.
Pia, amefafanua, anapokuwa kwenye majukumu yake ya soka, nyumbani hapo huwa anamwachia jamaa yake aliyemtaja kwa jina moja la Bakari.Safari.
NYUMBANI
Mwanaspoti: Hodi!
Atupele: Karibu. Hapa ndiyo nyumbani. Nimeamu kuja kujificha huku sitaki fujo, kama unavyoona, naishi kwa amani na mambo yangu yanakwenda vizuri.
Mwanaspoti: Kwa nini uliamua kuja kukaa huku na nani aliyekutafutia nyumba?
Atupele: Niliamua kwa sababu ya malengo niliyojipangia. Kama unavyojua mimi ni kijana, muda huu ndiyo wa kutengeneza maisha, huku naona ni mahali sahihi, mambo ya anasa yanakuwa mbali. Nimependa kwa sababu ni mahali tulivu, hakuna fujo pia maisha ni nafuu na aliyenitafutia nyumba ni jamaa yangu anaitwa Bauba.
Awali nilikuwa nikikaa Sinza lakini kule nilikuwa natumia pesa nyingi, tena kwa mambo yasiyo na umuhimu, nikaona bora nije nikae huku na tangu nimehamia, nimeshafikisha mwaka sasa.
Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani unapenda kufanya nini?
Atupele: Ninapokuwa nyumbani, napenda kucheza gemu (play station) kama unavyoniona, pia nasikiliza muziki wa Bongo Fleva na napenda kuangalia picha za Kihindi.
Mwanaspoti: Nani anayekupikia na kukufanyia usafi?
Atupele: Nafanya mambo yote mwenyewe, lakini bibie (mchumba wake) anapokuwepo, huwa ndiyo nafuu yangu kwa sababu anamaliza kila kitu.
MALAVIDAVI
Mwanaspoti: Umenitambulisha Khadija ni mchumba wako, malengo yenu ni kufunga ndoa lini na ulimpata vipi?
Atupele: Ndiyo Khadija ni mchumba wangu, lakini tulizungumza juu ya suala hili la ndoa tukakubaliana tufanye kwanza mambo yetu. Kama unavyojua yeye bado ni mwanafunzi ana mipango yake kielimu na mimi kazi yangu mpira ambayo nataka nifanikiwe zaidi, hivyo kwa sasa hatujajua ni lini tutakamilisha siala hilo. Nilivyompata ilikuwa hivi. Ni mwaka wa kwanza baada ya kujiunga na Coastal Union ya Tanga. Mpaka sasa imepita miaka mitatu. Ilikuwa siku ya mapumziko nilikwenda kujipumzisha ufukweni mwa Bahari ya Hindi kule Raskazone na wao walikwenda kusheherekea sikukuu ya kuzaliwa ya rafiki yao ndipo nilimwona. Sikuwa namjua kabla, lakini nilipomwona alinivutia nikatamani kuzungumza naye. Wakati nazungumza naye, nilikuwa namsaminisha kila kitu na kujifunza vitu vingi kutoka kwake, nikajikuta nampenda zaidi na ndipo tulipoanzisha uhusiano hadi leo hii.
Mwanaspoti: Ni kitu gani kilivutia ukampenda Khadija?
Atupele: Mwonekano tu, lakini jicho lake ndiyo lilinimaliza kabisa (anacheka). Ukiacha na hayo baada ya kumzoea na kumsoma, niligundua ni mwanamke ambaye anajua maisha, anaweza kuishi maisha yote na hajui kuigiza, ni mkweli na msikivu pia. Kusema kweli anapokuwa mbali na mimi, huwa nakosa amani kabisa, nammisi hadi basi.
KHADIJA AZUNGUMZA
Mwanaspoti: Kitu gani ambacho ukikifanya, unajua utamkorofisha Atupele na wewe huwa anakuuzi anapofanya nini?
Khadija: Kusema kweli, katika kitu ambapo Atupele hakipendi ni uongo, fanya yote lakini usimwongopee.
Kwake nachukia baadhi ya mavazi anayopenda kuyavaa na mnyoo (kiduku). Unajua katika mazingira niliyokulia pamoja na kaka zangu, kuwaona wakiwa wamenyoa viduku au kuvaa kaptula zimechanwachanwa ni ngumu, nilijua wanaofanya hivyo ni wahuni na ndivyo nilivyomzania hata yeye wakati ananifuata. Lakini niligundua sivyo alivyo, lakini ili awe vizuri, nimekuwa nazungumza naye kidogokidogo ananielewa, anaweza kuzivaa hizo nguo zake hapa nyumbani lakini ninapotoka naye (out) havai.