Loh Azam! Wamekufa namna hii

Muktasari:
Kipigo hicho cha ugenini kimeifanya Azam kung’oka mashindanoni kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya ushindi wa mabao 2-1 nyumbani wiki iliyopita kutowabeba.
AZAM imeshindwa kuweka rekodi. Imekwama kuvuka raundi ya pili ili iingie katika hatua ya mwisho ya 16 Bora (play-off) ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Esperance ya Tunisia.
Kipigo hicho cha ugenini kimeifanya Azam kung’oka mashindanoni kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya ushindi wa mabao 2-1 nyumbani wiki iliyopita kutowabeba.
Hata hivyo zipo sababu zilizoiangusha Azam katika mechi hiyo ya marudiano, ambayo imeikwamisha kuvuka rekodi yao ya mwaka 2013 ilipokwamia raundi ya pili mbele ya FAR Rabat ya Morocco iliyowang’oa pia katika michuano kama hiyo.
MAJERUHI
Kocha Stewart Hall amefichua kuwa kukosekana kwa wachezaji wake muhimu katika mchezo huo imewagharimu.
Stewart alikiri mapema hata kabla ya mchezo huo kuwa, walikuwa na kibarua kigumu kutokana na kuwa na wachezaji wengi muhimu majeruhi.
Baadhi ya mashabiki wa timu ya Azam waliopo hapa Tunisia walisema uwezekano wa Azam kushinda mechi hiyo iliyochezwa Jumanne usiku kwenye Uwanja wa Olimpiki, ulikuwa mdogo kwa asilimia 50 licha ya kuonesha ushindani katika kipindi cha kwanza.
Pengo la Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Kipre Tchetche na kiungo Jean Baptiste Mugiraneza, ambaye hakucheza kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, lilikuwa wazi hata kama wengine waliopangwa walijitahidi kupambana.
Pia kuja kuumia kwa Farid Mussa siku moja kabla ya mechi akiwa mazoezini alipogongana na beki wake, Morad Said ni pigo jingine lililoigharimu Azam katika mchezo huo ambao Esperance ilitumia udhaifu huo wa Azam kuvuka salama.
NYONI
Licha ya Farid kuchezeshwa akiwa bado hajapona vizuri na kuja kuumia tena uwanjani, lakini kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa Azam, Erasto Nyoni alilazimika kuwepo kikosini licha ya kusumbuliwa na mafua. Ilikuwa lazima Nyoni acheze kwa vile orodha ya majeruhi ilikuwa kubwa na ilikuwa vigumu kumuacha nje.
Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alilazimika kuweka viungo watano, Kipre Balou, Ramadhani Singano ‘Messi’, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy na Farid Mussa kati kati kwa lengo la kuzuia mashambulizi yasiende mbele ili kulinda ushindi wa 2-1 walioupata Dar es Salaam, huku safu ya ushambulizi akimuweka nahodha John Bocco.
Bocco alijaribu kufurukuta katika kutafuta magoli lakini alishindwa kufanya chochote kutokana na kudhibitiwa huku wachezaji wengine kama Sure Boy na Farid licha ya kucheza vizuri, walizidiwa maarifa na wachezaji warefu wa Esperance.
Pamoja na kukosekana wachezaji wanne muhimu, Azam waliweza kucheza mpira wa ushindani katika dakika 45 za kipindi cha kwanza na kuwafanya Esperance, iliyo nafasi ya tatu kwa ubora kwa Afrika, kupaniki na mashabiki wao wapatao 5000 kukosa uvumilivu.
Kipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada katika kipindi cha kwanza kwa kuzuia zaidi ya magoli manne, kabla ya kufungwa kirahisi katika kipindi cha pili.
Hata hivyo, kufungwa kwa Azam goli la kwanza katika dakika chache cha kuanza mpira kipindi cha pili kilipelekea mabingwa hao wa Kagame kulazimika kufunguka kutafuta bao na kuruhusu wenyeji kuwaelemea zaidi.
VURUGU
Mchezo huo uliochezwa mjini Tunis uligubikwa na vurugu za mashabiki waliokuwa wakirusha chupa na kung’oa viti kuwatupia polisi wakati mchezo ukiendelea.
Wapenda soka wa Tunisia wana historia ya kufanya vurugu uwanjani na kutokana na matukio yao ya kupambana na polisi mara kwa mara, mashabiki wachache (wapatao 5000) tu ndio walioruhusiwa kuingia katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki zaidi ya 50,000 huku kukiwa na upekuzi mkali uliofanywa na polisi.
Mwandishi wa habari hii alishuhudia polisi wengi wakiwa na silaha pamoja na vifaa maalumu vya kujikinga kutokana na tabia ya mashabiki ya kurusha chupa na viti pindi wapatapo hasira.
BAO LILILOWAUA
Bao lililowatoa Azam mchezoni lilifungwa na Saad Bguir dakika ya 47 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Fakhreddine Ben Youssef kuangushwa na David Mwantika nje kidogo ya boksi.
Dakika ya 63 Haithem Jouini alifunga kwa kichwa akimalizia mpira uliotemwa na kipa Aishi Manula kufuatia krosi ya Hoiucine Regued na dakika ya 80 Fakhreddine Ben Youssef akafunga la tatu akimalizia pasi ya kiungo Driss Mhirsi.
Azam haikuweza kabisa kulitia misukosuko lango la Esperance ambao walikuwa wanafurahia uchezeshaji wa marefa wa nchi jirani yao, Morocco.
Katika mchezo huo Azam ilipa kona moja dhidi ya 11 za wenyeji wao, pia ilishambulia lango la Esperance mara tisa dhidi ya mashambulizi 16 ya Esperance na Azam iliotea mara tatu dhidi ya nane za wenyeji na wachezaji wake watatu kupewa kadi za njano.
WAARABU TATIZO
Azam imeendeleza wimbi la timu za Tanzania kushindwa kufurukuta mbele ya klabu za Afrika Kaskazini. Kwa miaka mingi timu za Tanzania iwe klabu au timu za taifa zimekuwa zikikwama mbele ya Waarabu hata kama zipo vema.
Wachezaji na hata mashabiki wamekuwa na imani kwamba timu zetu haziwawezi Waarabu na hisia kwamba zinapocheza kwao hazifungiki na huwa zinafanya kila hila ili kusonga mbele, kitu ambacho kimekuwa kikiziangusha timu za Tanzania.
Simba, Yanga na hata Taifa Stars, ukiacha Majimaji Songea na Prisons Mbeya zote zimeshachezea vichapo vya Waarabu, japo Simba ina nafuu kulinganisha na wengine.
Historia hiyo ndiyo iliyoiua pia Azam, ambayo walitakiwa kumalizana mapema na Esperance tangu mechi ya Dar es Salaam. Azam, kwa kutumia uwanja wa nyumbani, walitakiwa kujichukulia chao mapema.
Azam, kama ilivyo Yanga, walishindwa kutumia nafasi ya kupata mabao katika mechi zao za nyumbani ambapo kama wangefanya kweli mechi za ugenini kwao zingekuwa nyepesi. Hata hivyo ni wakati wa klabu zetu kukaa chini na kukata minyororo hii ya ‘utumwa’ kwa timu za Waarabu.
USHABIKI
Wakati mwingine mashabiki wanapaswa kuacha ushabikia timu za Kaskazini. Wanapaswa kuungana na kushangilia vikosi vya nyumbani kwani klabu inapofanya vizuri sifa inakuja kwa nchi na si kwa mtu mmoja.