Kwa Morrison… Milango ya Sheria bado ipo wazi kwa Yanga
MAAMUZI ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kati ya Bernard Morrison na Klabu ya Yanga, yalishatolewa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 39(1) (h) na 40 (8) zote za Katiba ya TFF, iliyorekebishwa mwaka 2019, zinatambua kamati hii na kutoa majukumu yake bayana.
Katika kufanya kazi zake, hasa za utatuzi wa migogoro ya mikataba kati ya klabu na mchezaji, inawezeshwa pia na Kanuni ya 70 (14) ya Kanuni za Ligi Kuu, Toleo la 2018.
Kila mdau wa soka nchini anafahamu kwa mujibu wa kamati hii, Morrison ameshinda kesi yake dhidi ya Yanga.
Moja ya hoja zilizoelezwa ni mkataba wenye mgogoro yaani wa miaka miwili ulikuwa na mapungufu makubwa upande wa tarehe.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hii, mkataba huu ulisainiwa tarehe 20.03.2020 na ule uliokuwa unaisha ni tarehe 14.07.2020.
Kama hiyo haitoshi, alinukuliwa mkataba halisi unasoma tarehe 15.07.2020.
Pia inadaiwa kuna ukurasa wa saini kwenye mkataba unaonyesha kuwa umekatwa.
Binafsi, uamuzi huu unanifikirisha sana, ukianza tu na namna tarehe za mkataba alivyozisema.
Maana kuna tarehe mbili tofauti ambazo anakiri mkataba kusainiwa, pia tarehe ya kumalizika kwa ule wa awali, ambao kimsingi haubishaniwi.
Kwa ufahamu wangu, utimamu wa mkataba unapimwa kwa vitu muhimu zaidi na vyenye uzito kuliko hivyo alivyosema.
Vitu hivi ni ikiwa kuna uwezo wa kuingia mkataba baina ya pande zote, makubaliano huru, thamani na nia ya kuweka mahusiano kisheria.
Ninatambua ni muhimu mkataba uwe na tarehe ya kuanza na kumalizika, lakini hauwezi kukosa utimamu kisa tu kuna tarehe tofauti, au hakuna kabisa.
Pande mbili katika mkataba zinaweza kufikia makubaliano leo, lakini utekelezaji wa makubaliano hayo, ukaanza siku nyingine.
Hivi ndivyo pia hata makubaliano ya awali huwa yanafanyika baina ya klabu na mchezaji, hasa anapokuwa hajamaliza mkataba wake.
Ninasisitiza tena hapa kuwepo kwa tarehe mbili tofauti kwenye mkataba siyo hoja kubwa ya kuunyima haki upande fulani kwenye mkataba halali.
Endapo kama mkataba hauonyeshi tarehe ya kusainiwa kwake au ina tarehe tofauti, bado kumaliza utata huu inabidi tuangalie lini mkataba huu utaanza kufanya kazi.
Hata kama pande zote mbili zimesahau ni lini zilisaini mkataba, bado chombo kinachotatua mgogoro wa aina hii, kinatakiwa kujiridhisha zaidi ya hapo.
Hapa ni pamoja na kupitia nyaraka zingine katika mkataba huo, ili kuona kama kuna utekelezaji wa mkataba huo kutoka kwenye kila upande wa mkataba huo.
Katika shauri la Morrison, kuna mahali Mwenyekiti wa Kamati alinukuliwa akimtaka mchezaji huyu kuirudishia Yanga Dola 25,000 na ile 5,000 maana alipewa.
Hivi ni vitu muhimu ninavyovizungumzia hapa, kulikuwa na mkataba timilifu, ndiyo maana malipo yalifanyika terehe fulani na alipokea.
Hii ndiyo thamani kama kipengele muhimu katika mkataba wowote timamu kisheria na siyo tarehe peke yake ya kusainiwa.
Kupitia nyaraka ya malipo kutoka kwa klabu kwenda kwa mchezaji, ni rahisi kugundua uwepo na utekelezaji wa mkataba huo maana kuna tarehe ya malipo.
Unapolipa mchezaji, maana yake unatekeleza mkataba na tarehe hiyo inaweza kuchukuliwa kuwa tarehe ya mkataba ikiwa kuna utata wa lini ulisainiwa au kuanza kutekelezwa.
Kuhusu kukatwa kwa ukurasa wa saini kwenye mkataba, siyo hoja ya msingi ya kuunyima thamani mkataba.
Kwanza hatuambiwi bayana kwenye kukatwa ukurasa saini nayo imekatwa, imekatwa na nini, nani aliyekata na ikiwa kuna upande unalalamikia ukatwaji huo.
Ikiwa saini imekatwa kwenye ukurasa huo, je imefutwa ili kuleta udanganyifu?
Je, kitendo hicho cha kukatwa ukurasa kinamaanisha ni kughushi nyaraka?
Huwezi kuacha kuupa thamani mkataba mzima kwa hoja ya kukatwa ukurasa, ikiwa hakuna ubishi kwenye vipengele vyake na saini za pande zote mbili.
Ndiyo maana kwenye uamuzi huo sijasikia hoja saini zinabishaniwa kwenye mkataba huo licha ya kukatwa kwa ukurasa wa saini.
Katika mazingira kama haya, pande zote mbili zilikuwa zinaelewa mkataba huu hata kama ulikuwa haujafika mbali sana katika utekelezaji wake.
Kitu cha kushangaza zaidi ni licha ya kanuni ya 70 (8) ya Kanuni za Ligi Kuu kutaka Mikataba yote ya wachezaji wa Ligi Kuu kusajiliwa na kuthibitishwa na TFF, hatujaambiwa bayana ikiwa mkataba huo uliwahi kusajiliwa huko au la.
Kama ulisajiliwa, je, unafanana na ule unaobishaniwa au upo tofauti?
Swali linalobaki hapa ni je, Yanga baada ya kushindwa shauri hili, wanaweza kutafuta haki yao sehemu nyingine?
Kwa mujibu wa kanuni ya 70 (14) ya Kanuni za Ligi Kuu, Uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ni wa mwisho katika usuluhishi na utatuzi wa mgogoro wowote wa mkataba.
Nafuu pekee iliyotajwa kwa upande ambao haujaridhika na uamuzi ni kuomba marejeo (review) ya usikilizwaji wa shauri hilo.
Moja ya sababu ya kuomba marejeo ni ikiwa kuna ushahidi mpya ambao haukugunduliwa wakati wa shauri, licha ya kuhitajika.
Sasa, ikiwa Yanga hawana ushahidi mpya, rufaa ndiyo njia sahihi zaidi kwao.
Kwa mujibu wa Ibara ya 51 ikisomwa pamoja na Ibara ya 77 ya Katiba ya TFF, inaitambua Mamlaka ya Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo kwa kimombo, Court of Arbitration for Sport (CAS) iliyopo pale Lausanne, Uswisi.
Katika Ibara hizo, zinakataza uamuzi wa vyombo vya TFF kupelekwa kwenye Mahakama za kiraia isipokuwa CAS.
Chombo hiki huru kimeanzishwa chini ya Ibara ya 57 ya sheria ya FIFA (FIFA Statutes) toleo la mwaka 2019 kwa ajili ya kusuluhisha migogoro, mathalani baina ya FIFA, wanachama wake, mashirikisho, ligi, klabu, wachezaji na maafisa wa soka.
Hakuna ubishi vilevile, mamlaka ya CAS yamewekwa bayana katika Ibara ya 58 (1) ya sheria hiyo na inaruhusu rufaa kutokana na uamuzi wa mwisho wa vyama vya soka mwanachama wa FIFA.
Kitu kikubwa cha kuzingatia hapa ni rufaa kwenda CAS inatakiwa kupelekwa ndani ya siku 21 baada ya uamuzi wa chama cha soka kutolewa.
Vilevile, mrufani anatakiwa awe ametumia vyombo vyote vya ndani vinavyohusika na mgogoro huu, kabla ya kugonga mlango wa CAS.
Ndani ya nyaraka ya rufaa, mrufani anaweza kuomba kusimamishwa kwa utekelezaji wa uamuzi uliofanywa na shirikisho kupitia kamati yake.
Hivi ndivyo ninavyoielewa kanuni ya 48 ya Kanuni zinazotumiwa na CAS, yaani the Code of Sports-related Arbitration, 2020.
Hapa ndipo pia ninapata wasiwasi wa uamuzi wa Morrison kusaini Simba maana endapo Yanga watakata rufaa hii na pengine kushinda, balaa litakuwepo.
Hapa adhabu itakuwa kwa Morrison na Simba, maana mchezaji atahesabiwa alisaini Simba wakati ana mkataba halali Yanga.
Adhabu yake ni kufungiwa miezi minne na timu yake mpya kufungiwa kusajili kwa madirisha mawili, kulipa fidia na pengine adhabu kali zaidi.
Ndivyo ninavyoielewa kanuni ya 17 (3), na (4) ya Kanuni za Hali na Usajili wa Wachezaji, Toleo la Juni, 2020.
Ninajaribu tu kuwaza ikiwa katika kipindi hicho atakuwa ameichezea timu yake mpya wakati ana mkataba halali na Yanga.
Je, hiyo michezo atakayokuwa ameichezea timu yake mpya, pointi zake zitabaki salama kwao?
Hakika kama kweli Yanga watakwenda CAS, huenda kuna makubwa zaidi tukayashuhudia. Wakati ndiyo shahidi wa kweli katika haya.
Ninakutakia Tafakuri Njema.
Kasanda Mitungo, ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na pia Mwandishi wa masuala ya kisheria, kijamii, na siasa za kimataifa, anapatikana kupitia:
Simu: +255 712 786 051; Barua pepe: [email protected]