ZBL yatoa tahadhari upangaji matokeo
Muktasari:
- Amesema hakufurahishwa na mambo namna yalivyotokea msimu wa 2025-2026 hadi kuifanya ligi hiyo kupoteza hadhi mzunguko wa mwisho.
MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL), Issa Kassim Ali, amesema wamejipanga kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya upangaji matokeo wakati wa mechi za Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027.
Amesema hakufurahishwa na mambo namna yalivyotokea msimu wa 2025-2026 hadi kuifanya ligi hiyo kupoteza hadhi mzunguko wa mwisho.
Mtendaji huyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Mwanaspoti viwanja vya Mao Zedong uliopo kisiwani Unguja.
Alieleza kuwa, Bodi ilishazungumza na Jeshi la Polisi Zanzibar kuwasaidia hilo, hivyo na yeyote atakayeshikwa na madai hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni ya mashindano.
“Wakati tukielekea kuanza msimu mpya wa ligi, Bodi imejipanga kudhibiti vitendo vya upangaji wa matokeo na tumeshazungumza na Jeshi la Polisi,” amesema.
Alifafanua, kilio kikubwa cha Zanzibar ni kupata uanachama katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), hivyo endapo watashindwa kudhibiti mambo ambayo yanaharibu ligi hiyo hawawezi kupata wanalolitaka.
Amewataka viongozi wa klabu zote 16 zinavyoshiriki Ligi Kuu Zanzibar kushindana uwanjani na sio kujihusisha na kupanga matokeo.
Amesema Bodi haitamvumilia kiongozi au mchezaji yeyote ambaye atajihusisha na vitendo hivyo kwani wanaiharibu ligi, huku akisisitiza upangaji wa matokeo unapunguza mvuto wa ligi na hayo yanatokea zaidi katika mzunguko wa pili ambao ndio lala salama.
“Timu yoyote ambayo haihitaji kushuka daraja inapaswa kufanya maandalizi mapema kuepuka hayo na siyo kutegemea njia ambayo haikubaliki kisheria,” amesema.
Ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 29, 2026 kwa kuchezwa mechi tatu ambazo ni KVZ dhidi ya Polisi, KMKM vs Kipanga na FSC vs Raskazone.