KVZ, Simba hazichekani Kagame Cup
Muktasari:
- Simba ambayo ipo Kundi B, imeambulia suluhu katika mechi zote mbili ilizocheza, ilianza kwa kutoka suluhu dhidi ya Mogadishu City kabla ya kurudia matokeo hayo ilipokutana na Jamus ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
LICHA ya kuwa na historia tofauti katika soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Simba na KVZ zimejikuta zikiwa na rekodi moja isiyovutia kwenye michuano ya Kombe la CECAFA Kagame baada ya kuwa miongoni mwa timu ambazo hazijafunga bao ndani ya michezo yao miwili ya kwanza.
Simba ambayo ipo Kundi B, imeambulia suluhu katika mechi zote mbili ilizocheza, ilianza kwa kutoka suluhu dhidi ya Mogadishu City kabla ya kurudia matokeo hayo ilipokutana na Jamus ya Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Kwa upande wa KVZ ya Zanzibar, hali imekuwa mbaya zaidi kwani mbali na kushindwa kufumania nyavu, imepoteza mechi zake zote mbili, ilianza kwa kuchapwa mabao 2-0 na Rayon Sports ya Rwanda, kabla ya kupokea kipigo kingine cha mabao 4-0 kutoka Al Hilal ya Sudan.
Mbali na Simba na KVZ, Tusker ya Kenya pia bado haijaonja ladha ya bao katika mashindano hayo. Wakenya hao walifungwa mabao 2-0 na Al Hilal katika mchezo wa kwanza, kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports, hivyo kubaki bila kufunga katika mechi mbili.
Hata hivyo, tofauti na KVZ na Tusker ambao wamekuwa wakiruhusu mabao, Simba imeonyesha uimara mkubwa wa safu yake ya ulinzi kwa kutoruhusu bao hata moja katika michezo yake miwili ya kwanza, ingawa nayo imekuwa na wakati mgumu wa kuzitumia nafasi ilizotengeneza.
Nayo Garde Républicaine, licha ya kuwa miongoni mwa timu zilizoruhusu mabao mengi zaidi, ikiwa imefungwa mabao sita sawa na KVZ, angalau imefanikiwa imefunga bao moja, jambo linaloifanya isitoke kabisa kwenye orodha ya timu ambazo hazijafunga katika mashindano hayo.
Katika mechi za mwisho za hatua ya makundi Simba ambao wameaga katika mashindano hayo watacheza dhidi ya Singida Black Stars ambao bado wananafasi ya kwenda nusu huku KVZ ikicheza dhidi ya Tusker.