KVZ katika mtihani mzito Cecafa Kagame Cup
Muktasari:
- KVZ inaingia katika mchezo huo ikiwa na presha ya kutafuta matokeo baada ya kuanza vibaya mashindano hayo kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Rayon Sports katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Amahoro.
WAWAKILISHI wa Zanzibar katika Kombe la CECAFA Kagame, KVZ SC, leo Jumatano wanakabiliwa na mtihani mkubwa watakaposhuka dimbani kuikabili miamba ya Sudan, Al Hilal SC katika mchezo wa Kundi C utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kigali Pele jijini Kigali.
KVZ inaingia katika mchezo huo ikiwa na presha ya kutafuta matokeo baada ya kuanza vibaya mashindano hayo kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Rayon Sports katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Amahoro.
Kwa upande mwingine, Al Hilal imeanza kwa kasi baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-0 na kujipa nafasi nzuri kwenye mbio za kufuzu hatua ya nusu fainali.
Mchezo huu unakuwa muhimu kwa KVZ kwani ushindi unaweza kuirudisha kwenye nafasi nzuri ya kuwania kufuzu, lakini matokeo mabaya yataifanya safari yake ya Kagame kuwa ngumu zaidi katika kundi lenye timu zenye uzoefu mkubwa.
Kocha wa KVZ, Bababuu Omar, alieleza baada ya mchezo uliopita kuwa moja ya changamoto zilizowafanya wapate matokeo mabaya ilikuwa ni presha ya kucheza dhidi ya wenyeji Rayon Sports pamoja na mazingira ya mchezo.
Hata hivyo, kocha huyo anaamini mazingira ya Uwanja wa Kigali Pele yanaweza kuwa msaada kwa timu yake katika mchezo dhidi ya Al Hilal, hasa kutokana na tofauti ya aina ya nyasi walizotumia kwenye mchezo wa kwanza. Katika mchezo dhidi ya Rayon Sports, KVZ ilicheza kwenye nyasi halisi za Amahoro, lakini safari hii itakuwa kwenye uwanja wa nyasi bandia wa Kigali Pele ambao kocha anaamini wachezaji wake wanaweza kuuzoea vizuri zaidi.
Kwa upande wa Al Hilal, mchezo huu ni nafasi ya kuthibitisha ubora wao kama moja ya timu kubwa kwenye ukanda huu. Timu hiyo ya Sudan ilimaliza ikiwa mshindi wa pili katika mashindano yaliyopita ya Kagame, hivyo inaingia na uzoefu mkubwa wa mashindano haya.
KVZ sasa inahitaji zaidi utulivu, nidhamu ya mchezo na kutumia nafasi zitakazopatikana ili kuzuia Al Hilal kuendelea na mwendo wake wa ushindi.