Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumbe Godliver angekuwa mjeshi aisee

Muktasari:

  • Umahiri wa sanaa yake ndio uliomfanya akachukua tuzo kadhaa, kama unataka kuujua utamu wake kwenye uigizaji, jipe muda angalia filamu za ‘Siri Ya Mtungi,’ ‘Aisha’ na ‘Bahasha’ iliyofanikiwa kufungua uzinduzi wa Tamasha la ZIFF 2018.

KWA mashabiki wa filamu za Bongo, mwanadada Godliver Gordian si mgeni kabisa kwao. Ni kwa sababu ameonekana katika filamu kibao akifanya yake.

Umahiri wa sanaa yake ndio uliomfanya akachukua tuzo kadhaa, kama unataka kuujua utamu wake kwenye uigizaji, jipe muda angalia filamu za ‘Siri Ya Mtungi,’ ‘Aisha’ na ‘Bahasha’ iliyofanikiwa kufungua uzinduzi wa Tamasha la ZIFF 2018.

Godliver ana majina kibao tu ya kisanii; Cheusi, Aisha, Tina na pia Anita, yote hii ni kutokana na filamu alizoigiza huku akiweza kuziteka hisia za mashabiki kutokana na kuzitendea haki nafasi anazocheza.

Si filamu tu, Godliver pia ni mshereheshaji wa shughuli mbalimbali, ni kama alivyofanya usiku wa tuzo za AZIF za chaneli ya Sinema Zetu baada ya kumuuliza Hamisa Mobetto kuwa nani alipendeza usiku ule na Mobeto kujibu kuwa ni Diamond.

Mwanaspoti lililoweka kambi mjini Unguja, Zanzibar kwenye Tamasha la ZIFF limezungumza na Godliver anayekuja na mambo kadhaa hapa ambayo pengine haukuwa ukiyafahamu.

Mwanaspoti: Una lipi la kuzungumza kuhusu Filamu ya Bahasha kufungua pazia la tamasha la ZIFF?

Godliver: Kwanza namshukuru Mungu kwa kufanikisha ubora wa kazi yetu kuonekana na kukubalika hivi. Ubora huu tutazidi kuuimarisha, lakini pia niishukuru ZIFF kwa kuipanga filamu hii kuzindua tamasha la mwaka huu.

Mwanaspoti: Kuna ambao hawajaiona ‘Bahasha’, kwa kifupi tu inahusu nini?

Godliver: Inahusu rushwa. Ni filamu inayofichua mengi yanayoendelea kichinichini katika Idara za Serikali.

Mwanaspoti: Vipi, unaweza kunyakuwa tuzo ya ZIFF kwa filamu ya ‘Bahasha’?

Godliver: Naamini hivyo, na si hiyo tu bali kwa vipengele vyote tunavyoshiriki ZIFF.

Mwanaspoti: Kuna nini unachokiona katika ZIFF hii?

Godliver: Bado wasanii wa filamu za Kibongo hawana mwamko na elimu juu ya Tamasha la ZIFF, si wengi wanaoshiriki japo mimi nilikuwepo pia mwaka juzi kupitia filamu ya Aisha.

Mwanaspoti: Ulishawahi kuchukua tuzo ya uigizaji?

Godliver: Kwa maana ya zile kubwa, nilichukua Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike mwaka 2016 kupitia filamu ya Aisha.

Mwanaspoti: Kwanini unapenda kuigiza filamu za mateso?

Godliver: (Huku anacheka) Huwa napangiwa na waandaaji, ila naweza kuigiza sehemu yoyote nikipewa.

Historia yake

Katika tamaduni za Kimagharibi, mtoto ana uhuru wa kuchagua afanye nini au ajikite kwenye taaluma gani. Huko wazazi huwa mstari wa mbele kumsaidia mtoto kwa kumwekea mazingira ya kufanikisha kile anachokitaka, yaani atimize ndoto zake.

Kwa Afrika ni tofauti, wazazi ndio humwongoza mtoto cha kufanya, sasa inapotokea mtoto akachagua kufanya kitu tofauti na matakwa ya wazazi wake, huchukulia kuwa ni mkaidi. Na hapo unaweza kutokea mtiti balaa.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Godliver pia ambaye mbali ya uigizaji, kitaaluma yeye ni Mwandishi wa Habari. Lakini unadhani huo ‘Upaparazi’ aliupata kirahisi? Au unadhani huu uigizaji ulimjia kama maji yanavyoshuka mlima? Msikie anachosema.

“Baba yangu alikuwa askari na hakuna mtoto wake wa kiume hata mmoja ambaye alifuata nyayo zake, hivyo akawa anataka mimi binti yake nirithi kazi hiyo. Alitaka niwe mwanajeshi,” anasema.

“Sasa mimi sikuwa kabisa na mzuka huo. Nilikuwa na kazi ya kumfanya anielewe. Kila alipozungumza nami alinisisitizia kufanya kazi ile ya uaskari.

“Nilipohitimu elimu ya sekondari kwa ajili ya kujiunga na chuo, hapo nikasema liwalo na liwe. Nikalazimika kumwambia ukweli kwamba napenda kuwa mtangazaji na si huo uaskari, hivyo nataka kusomea uandishi wa habari.”

Anasema alifanikiwa kumshawishi baba yake baada ya kumuahidi kuwa ataenda jeshini baada ya kumaliza elimu yake ya chuo, jambo ambalo litamwezesha kupata vyeo ndani ya muda mfupi. Ilikuwa bonge la chenga.

Uigizaji wake

Baada ya kuhitimu mafunzo ya uandishi wa habari, anasema akiwa bado kwenye harakati za kutafuta kazi, aliamua kujiingiza katika uigizaji, fani ambayo alikuwa akiipenda pia tangu utotoni. Ndipo alipofanikiwa kukutana na Single Mtambalike (RichieRichie) aliyemchezesha kwenye filamu ya Mahabuba.

Baadaye alipata taarifa za usaili wa waigizaji wanaotakiwa kucheza ‘Siri Ya Mtungi’ naye akajitosa kwa vile aliamini anaweza. Ndivyo ilivyokuwa akafanikiwa kupata nafasi hiyo.

“Kufikia hapo ikabidi tu baba akubaliane na ninachokifanya, alianza kuona dalili za mafanikio yangu, akabadilika na kuniunga mkono hali iliyozidi kunipa faraja na morali ya kusonga mbele zaidi,” anasema.

Anakiri ujasiri na msimamo wake vimechangia kumfikisha alipo sasa licha ya kupitia vikwazo mbalimbali ikiwamo kukatishwa tamaa, lakini aliongeza juhudi na kusonga mbele.

Akizungumzia amani

Godliver anasema hakuna kitu anachokitamani kiendelee kuwepo nchini kama amani.

Katika hilo, anaamini wanawake wana nafasi kubwa ya kuhakikisha amani inaendelea kutawala kwa kujenga misingi ya upendo na utulivu kuanzia kwenye ngazi za familia.

“Jamani tuache hasira na chuki, bali upendo utawale katika maisha yetu kwa nyakati zote. Tanzania ni kisiwa cha amani,” anasema huku akiachia tabasamu.