Kombe la Dunia 2022 kuja na mpya

Muktasari:
- Akizungumza na Gazeti la The Guardian la Uingereza, Infantino alisema: “Yawezekana soka ikawa njia ya kuponya majeraha na kurejesha uhusiano mwema. Tumeshuhudia hata katika kuwania maandalizi ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026, nchi tatu zilizopewa fursa hiyo (Marekani, Canada na Mexico) hazina uhusiano mzuri kisiasa au kidiplomasia. Lakini kama ujuavyo, soka hutenda miujiza.”
RAIS wa Fifa, Gianni Infantino, anaendelea kusisitiza pendekezo lake la kupanua wigo wa timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia 2022 kutoka 32 hadi 48, kuwa litaongeza ujirani mwema baina ya nchi zenye msuguano na Qatar, ambayo ni mwenyeji mtarajiwa wa mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Novemba 21, 2022. Ingawa Infantino amekiri uwezekano wa pendekezo lake kukubalika ni finyu, anasisitiza soka ni mchezo unaoweza kumaliza uadui wa kisiasa. Mwaka jana, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri ziliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Qatar.
Akizungumza na Gazeti la The Guardian la Uingereza, Infantino alisema: “Yawezekana soka ikawa njia ya kuponya majeraha na kurejesha uhusiano mwema. Tumeshuhudia hata katika kuwania maandalizi ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026, nchi tatu zilizopewa fursa hiyo (Marekani, Canada na Mexico) hazina uhusiano mzuri kisiasa au kidiplomasia. Lakini kama ujuavyo, soka hutenda miujiza.”
Licha ya zogo la kimataifa lililotokana na kuuawa kwa mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi, akiwa katika ofisi za Ubalozi wa nchi hiyo jijini Istanbul, Urutuki, mwezi uliiopita, bado Infantino anaamini mjadala huu kuhusu ushirikiano katika mechi za Kombe la Dunia unaweza kusaidia Saudi Arabia kuponya madonda hayo na kujenga taswira mpya.
“Ni wazi, uhusiano mbovu wa majirani wa Qatar unachangia kuharibu mambo; kwa upande mwingine, hata kama kuna uhusiano mbovu au mgumu kidiplomasia, inapofika mahali pa kujadili soka, watu huzungumza,” alisema Infantino.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ndio waliongoza wenzao katika kuiwekea Qatar vikwazo vya kiuchumi Juni mwaka huu kutokana na msimamo wa muda mrefu wa nchi hiyo kuhusu mapinduzi ya kisiasa yaliyotokea katika nchi za Kiarabu miaka michache iliyopita, na kuzuia shirika na utangazaji la Aljazeera, la nchi hiyo, kuripoti matukio hayo.
Raia wa Qatar, kwa kiasi kikubwa, wanaunga mkono msimamo wa mtawala wao, Sheikh Hamad bin Khalifa al-Thani. Na kwa jumla wanasema mauaji ya Khashoggi yameonyesha dunia taswira halisi ya utawala dhalimu wa Saudi Arabia.
Ameongeza licha ya vikwazo hivyo vya kiuchumi dhidi ya Saudi Arabia, timu za soka za nchi husika zinaendelea kushiriki michuano ya Shirikisho la Soka la Asia linalohusisha timu kutoka Ghuba na eneo pana la Mashariki ya Kati.
“Kuwa na moyo mkuu: Tunaweza kufanya jambo kwa ajili ya dunia. Inawezakana. Lolote linaweza kutokea. Twende nalo hatua kwa hatua. Ndiyo, matarajio ni kidogo, lakini mimi ni mtu nisiyetanguliza roho ya kushindwa, tutaona hapo baadaye.”
Kamati maalumu ya Qatar inayoandaa Kombe la Dunia – ambayo inahusika pia na ujenzi wa viwanja saba vipya vyenye thamani ya kati ya Dola za Marekani bilioni nane na 10, inashirikiana na wataalamu wa upembuzi yakinifu wa Fifa katika kujadili suala hilo la kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki, lakini bado serikali ya Qatar haitoi ushirikiano wa kutosha.
Infantino angependa baadhi ya mechi zichezwe katika nchi jirani na Qatar ili kufanikisha maandalizi na ufanisi wa michuano hiyo.
“Qatar ina viwanja vinane, na inajiandaa kuwa mwenyeji wa michuano inayoshirikisha timu 32; ni wazi, huihitaji kuwa bingwa kung’amua kuwa litakuwa jukumu kubwa na gumu sana kwa nchi moja kuandaa mashindano yanayoshirikisha timu 48 katika viwanja vinane,” alisema.
Kwa mujibu wa Infantino, iwapo Qatar itashirikiana na nchi jirani katika maandalizi ya mechi hizo, kutapunguza chuki na uadui miongoni mwao, licha ya sakata la mauaji ya Khashoggi.
“Jambo hili linajadilika. Iwapo litawezekana, nitafurahi sana. Likishindikana (zikabadi timu 32) , vilevile itakuwa sawa tu. Jambo jema ni walau nitakuwa nimejaribu kulisukuma.
“Iwapo jambo hili linasaidia kuboresha soka, itakuwa vema zaidi. Iwapo madhara yake kwa usitawi wa eneo hilo yataonekana kuwa makubwa, basi liachwe.
Kuhusu uwezekano wa Saudi Arabia kuwa mwenyeji mwenza wa michuano, Infantino alisema: “Lazima tulitazame katika muktadha wa hali ya kisiasa katika eneo husika, tukitarajia mambo yatakuwa yameimarika na kuwa bora zaidi kwa ajili ya soka na dunia kijumla. Iwapo mjadala wowote kuhusu jambo hili utaimarisha ustawi katika ukanda huu, hasa kuhusu Saudi Arabia, litakuwa jambo jema sana.
Akisisitiza umuhimu wa soka katika kuboresha ustawi wa kijamii, Infantino ametoa mfano wa Iran ambayo ilitoa ruhusa kwa wanawake wapatao 1,000 (kwa mujibu wa Fifa) kuingia uwanjani kama washangiliaji kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa ya Asia kati ya timu ya Persepolis kutoka Tehran na Antlers kutoka Japan, iliyochezwa Novemba 10, mwaka huu.
Tangu mwaka 1981, kwa sababu za kusisitiza misingi ya Dini ya Kiislam, Iran ilipiga marufuku wanawake kuingia katika viwanja vya soka.
“Sisi si wakamilifu lakini, licha ya makosa kadhaa tunayotenda, tunajitahidi kufanya tuwezalo” alisema Infantino.