Prime
Kolabo ya Nabi, Gamondi ilivyoibeba Yanga CAF
Muktasari:
- Mafanikio inayopitia Yanga yamebebwa na makocha wawili tofauti. Yanga ilianza na Nasreddine Nabi kuandika historia ya kufika fainali na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa sare ya mabao 2-2.
Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga moto wake unazidi kuchoma hadi kwenye michuano ya kimataifa baada ya msimu huu kuweka rekodi kadhaa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikitinga robo fainali ikiwa ni miezi michache tangu ilipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mafanikio inayopitia Yanga yamebebwa na makocha wawili tofauti. Yanga ilianza na Nasreddine Nabi kuandika historia ya kufika fainali na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa sare ya mabao 2-2, Yanga ikilala nyumbani 2-1 na kushinda 1-0 ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria iliyobeba taji hilo, kabla ya msimu huu mziki wa Yanga kuwa chini ya Kocha Miguel Gamondi.
Sasa unaambiwa, kolabo iliyofanywa na makocha hao wawili kwa misimu tofauti imeifanya Yanga iwe tishio barani Afrika na hata kwenye michuano ya ndani na hapa chini ni uchambuzi juu ya makali ya Nabi na Gamondi yanayowapa raha mashabiki wa klabu hiyo kutokana kushirikiana kwa baadhi ya maeneo yaliyokifanya kikosi hicho kukimbiza.
UKUTA WAO
Eneo la kwanza ambalo unaweza kuliangalia ni ukuta wa Yanga. Msimu huu ikiwa chini ya Gamondi kuna mabeki watatu pekee ndio walioongezeka mmoja wao Yao Attohoula akiingia moja kwa moja kuwa mtu muhimu upande wa kulia, huku Nickson Kibabage akiwa anapishana na mwenzake kule upande wa kushoto wakati Gift Freddy akiwa nje akisubiri.
Mabeki watatu wa kati - nahodha wao Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Hamad 'Bacca', kule kushoto kukiwa na Lomalisa Mutambala huku kipa akiwa Djigui Diarra wote wameendelea kuwa muhimu tangu kocha akiwa Nabi.
Gamondi hakupata shida kubwa kwani ukuta tayari alishaukuta, ila alichofanya ni kuuimarisha na kuendelea kucheza kwa ubora mkubwa bila kuubadilisha sana kutokana na kuwa tayari mabeki hao hasa wale wa kati walishatengeneza muunganiko mzuri.
MFUMO MMOJA
Nabi akiwa Yanga alikuwa anatumia mfumo wa 4-2-3-1 ambapo baada ya Gamondi kufika akauendeleza uleule, lakini kuna mambo akayabadilisha kulingana na falsafa yake.
Yanga ya Gamondi inakaba sana na hapa ndipo timu nyingi zinakwama zinapokutana nayo, huku nidhamu ya kukaba inaanzia kwa washambuliaji wa juu kushuka chini, lakini pia ikiunasa mpira inashambulia kwa kasi ndio maana imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Ikiwa chini ya Nabi, Yanga haikuwa na kasi kubwa katika kusukuka mashambulizi ikicheza pasi nyingi za kwenda mbele ingawa ilikuwa ikifunga, lakini haikuwa na uzalishaji wa mabao mengi kama ambavyo chini ya Gamondi imekuwa ikionekana kufanyika.
VIUNGO WANNE
Viungo wanne wa Yanga wanaocheza sasa wawili ni wale walishatengenezwa wakati wa utawala wa Nabi ambao ni Khalid Aucho na Mudathir Yahya, kisha mrithi wake Gamondi akaja na watu wa maana wawili juu Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli ambao wameongeza makali ya timu hiyo.
Gamondi, mafanikio yake Yanga yapo kwenye idara hii ambapo amebadilisha mambo machache yakiwemo matumizi ya Mudathir ambaye amekuwa kwenye ubora tofauti akiongeza akili ya kufunga mabao zaidi, lakini hata Stephanie Aziz KI ambaye anacheza eneo la juu la ushambuliaji akiwa na mabao 10 mpaka sasa kama kinara wa ufungaji kwenye ligi.
SHIRIKISHO VS LIGI YA MABINGWA
Yanga ya Nabi ilikuwa na moto mkubwa ikiweka historia ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikilikosa kwa kanuni tu ya bao la ugenini, lakini haikuwa na maisha mazuri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiishia hatua ya mtoano wa awali au ile ya pili.
Gamondi, raia wa Argentina akashuka na kitu kipya, akaja na msuli mkubwa kule ambako Nabi kulimshinda ambapo tayari sasa Yanga iko hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa - tena ikikata tiketi hiyo ikiwa na mchezo mmoja kabla ya kumaliza mechi sita za hatua ya makundi.
USIMAMIZI WA WACHEZAJI
Makocha wote wawili kwa nyakati tofauti wamefanikiwa kuifanya Yanga kuwa timu yenye nidhamu bora kuanzia ndani mpaka nje wakiwa wakali kwa makosa ya kinidhamu.
Nabi alikuwa hana muda wa kuangalia jina la mchezaji linapokuja suala la nidhamu Yanga ikiwa chini yake wachezaji wengi walikumbana na rungu la kinidhamu mfano ikiwa ni Bernard Morrison, Djuma Shaban, Yannick Bangala, Aziz KI na wengine waliokumbana na adhabu tofauti chini ya Mtunisia huyo.
Gamondi alipotua Yanga akashikilia makali hayo akikomaa na wachezaji wake wote walioonyesha makosa ya kinidhamu. Waulize Metacha Mnata na Jonas Mkude ambao walipofanya kosa dogo tu la utoro jamaa akawageukia kibabe na kuwaweka sawa na sasa mambo yanakwenda.
REKODI ZAWABEBA
Wakati Gamondi akibebwa na rekodi ya kuiongoza timu hiyo kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika akiivusha kutoka raundi za awali hadi makundi kisha robo fainali ikiwa na mchezo mmoja mkononi, kwa upande wa Nabi kitendo cha kuipeleka timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kimeacha alama kwenye mioyo ya Wanayanga.
Kabla ya Nabi kuifikisha Yanga huko timu hiyo ilishacheza mara mbili tofauti makundi ya Kombe la Shirikisho ikipenya kutokea Ligi ya Mabingwa ambako iling'olewa mwaka 2016 na 2018, lakini ikikwama kwenda robo fainali.
Lakini maufundi wa kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia yaliifanya iende hadi fainali kama utani.
Kwa michuano ya ndani kocha huyo alibeba mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, moja la kwanza bila kupoteza na kuiongoza Yanga kucheza mechi 49 bila kupoteza ikiwa ni rekodi kwa ligi hiyo na pia akinyakua Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili na Ngao ya Jamii mara mbili pia kwa kuifunga Simba mara zote.
Gamondi, licha ya kuanza vibaya kwa kupoteza Ngao ya Jamii mbele ya Simba kwa penalti, lakini ameanza Ligi Kuu na moto akigawa dozi ya tano tano kwa wapinzani ikiwamo kuifyatua Simba ambayo ilikuwa haijawahi kukumbana na kipigo kikubwa kama hicho katika Ligi Kuu mbele ya Yanga tangu ilipofungwa 5-0 mwaka 1968.
Yanga ya Gamondi imezifunga pia JKT Tanzania, KMC, kisha kugawa dozi kama hizo kwenye ASFC dhidi ya Hausung na Polisi, lakini ikiitandika Jamhuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na kipigo kama hicho iliipa Asas ya Djibouti katika mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha huyo ameivusha Yanga makundi ya Afrika kwa rekodi ya kuifunga Al Merrikh kwa mabao 3-0 ikiwa ni mara ya kwanza katika historia, kwani vijana wa Jangwani walikuwa hawajawahi kuifunga timu hiyo, lakini ikaipiga CR Belouizdad mabao 4-0 na kutinga robo fainali ikiwa ni rekodi kwa timu ya Waarabu kufungwa idadi hiyo na klabu ya Tanzania.
Mashabiki kwa sasa wanasikilizia kuona kama Gamondi ataendelea na moto kwenye Ligi ya Mabingwa na kuifikisha Yanga hadi hatua ipi, kwani imani yao kwa mziki ilionao timu hiyo wanaitabiria kufika hata fainali kama itafanya kweli katika mechi za robo fainali na nusu fainali ambazo ndizo zinazotajwa kuwa ngumu zaidi kwenye michuano hiyo mikubwa.