Prime
Kocha Simba avunja ukimya, atoboa siri
KOCHA wa Simba, Steve Barker amekiri kuwa kikosi bado hakijafikia kiwango cha juu cha utayari na makali anayotaka huku akielekeza nguvu kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baada ya kupoteza Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa New Amaan.
Simba ilikumbana na kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Jumatano iliyopita Zanzibar, matokeo ambayo yameifanya mechi yake inayofuata kuwa na umuhimu mkubwa zaidi, kwani itakuwa ya kwanza Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya uliopita kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker raia wa Afrika Kusini amesema licha ya kutoridhishwa na matokeo ya Ngao ya Jamii, mchezo huo umempa nafasi ya kuona maeneo ambayo kikosi chake kinahitaji kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kampeni ya ligi.
“Niwe mkweli kupoteza mchezo dhidi ya Yanga siyo matokeo tuliyoyataka. Ni jambo la kukatisha tamaa kwa sababu Simba kila mchezo tunaocheza tunataka kushinda na kila fainali tunayocheza tunataka kushinda. Kwa hiyo tumejisikia vibaya kushindwa kufikia lengo hilo,” amesema Barker.
Hata hivyo, Barker anaamini mchezo huo umekuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Simba kuelekea Ligi Kuu Bara, akisisitiza kuwa kikosi bado hakijafikia asilimia 100 ya kiwango anachotaka.
“Sidhani kama tupo katika asilimia 100 ya ubora wetu kwa sasa, lakini mchezo kama huu ulikuwa mzuri kwetu kupata utimamu wa mechi na ukali wa ushindani ambao utatusaidia kujiandaa kwa ligi,” amesema Barker.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Barker amesema muda mfupi uliopo wa maandalizi hautawazuia kuingia kwa lengo la kuanza ligi vizuri huku akisisitiza umuhimu wa kuonyesha ubora baada ya kupoteza Ngao ya Jamii.
“Tumekuwa na siku chache za kujiandaa dhidi ya Kagera. Naamini tutaonyesha namna ambavyo timu kubwa kama Simba inatakiwa kufanya baada ya kuteleza. Kwa sasa nguvu ni mechi ya ligi, kuanza vizuri,” amesema.
Kagera Sugar ndiyo itakayokuwa mpinzani wa Simba katika mchezo huo huku historia ya mechi tano za mwisho ikionyesha kuwa Wekundu wa Msimbazi wamekuwa na matokeo mazuri dhidi ya wapinzani hao. Katika michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kati ya timu hizo, Simba imeshinda mara tatu na kutoka sare mara mbili.
Rekodi hizo zinaonyesha kuwa katika mchezo wa Juni 22, 2025, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar. Kabla ya hapo, Desemba 21, 2024, Simba iliifunga Kagera Sugar mabao 5-2 ugenini, wakati Mei 12, 2024, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Desemba 15, 2023, Simba ilishinda 3-0 huku mchezo wa Desemba 21, 2022 ukimalizika kwa sare ya bao 1-1. Kwa jumla, katika michezo hiyo mitano, Simba imefunga mabao 11 na kuruhusu manne pekee.