Kocha Hababuu akoshwa na Kaseke
Muktasari:
- Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali alisema katika kikosi kilichoshiriki mashibdano ya Kagame yaliyomalizika hivi karibuni nchini Rwanda, Kaseke ni mchezaji aliyemkosha kwa kiwango chake.
WINGA wa KVZ, Agustino Chalamba ‘Kaseke’, amewashangaza viongozi wa benchi la ufundi na timu hiyo kwa jumla kutokana na kiwango kizuri alichonacho.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali alisema katika kikosi kilichoshiriki mashibdano ya Kagame yaliyomalizika hivi karibuni nchini Rwanda, Kaseke ni mchezaji aliyemkosha kwa kiwango chake.
Alisema, kwa namna alivyocheza vizuri, alikuwa na hofu ya kwamba hawatoweza kurudi naye, lakini anachoshukuru bado yupo kikosini kwake hadi sasa.
“Kati ya wachezaji ambao nilienda nao Rwanda, Kaseke kachukua namba moja kwa kucheza vizuri, nilikuwa nina wasiwasi ataondoka, nafurahia kuwa naye,” alisema.
Hababuu alisema, kwa kawaida anapenda kumuangalia mchezaji akicheza mechi na sio mazoezi kwa sababu kila mmoja anajituma mazoezini na Kaseke alimpa kitu ambacho alikuwa anakihitaji.
Agosti 17, 2026, Mwanaspoti lilipata nafasi ya kumshuhudia winga huyo akiwa mazoezini katika Uwanja wa Maisara kisiwani Unguja ambapo Kaseke ni miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na kikosi hicho kuelekea msimu wa 2026-2027.
Licha ya ugeni wake kikosini hapo, winga huyo amekuwa tegemeo katika timu hiyo kwa kile kilichoelezwa ni kuwa na utulivu na kujitoa zaidi uwanjani.