KMC yatimkia Moro, wajiandaa kutambulisha mastaa wao
Dar es Salaam. KLABU ya KMC FC imeanza rasmi kambi kwa ajili ya kujiandaa vizuri na msimu mpya wa Ligi kuu soka Tanzania Bara 2021/2022 kwa kuamua kulihama jiji la Dar es Salaam na kwenda kujichimbia Morogoro.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala ni kwamba vijana hao wa Kino boys waliondoka jijini Dar jana (Jumatano) asubuhi na ilifika salama mkoani humo ambapo ndipo imeweka kambi yake.
Ikiwa kambini, KMC itakuwa na programu mbalimbali za mazoezi pamoja na kucheza mechi za kirafiki kwa lengo la kuwapima na kuwaweka vizuri wachezaji kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu itakayoanza Septemba 27 mwaka huu.
Aidha kuhusu suala la usajili, KMC inaendelea kufanya usajili na wakati wowote kwa utaratibu wa klabu utakapokamilika itaanza kuwatambulisha wachezaji wote ambao wamesajiliwa katika dirisha kubwa lililofunguliwa mapema Agosti mwaka huu.
Mwagala alisema KMC inawajulisha mashabiki, wapenzi na Watanzania kwa ujumla kuwa usajili unaoendelea kufanyika umezingatia matakwa ya mwalimu na kwamba inasajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu na bora watakaoleta manufaa makubwa katika timu yetu.