Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga zimejua siri za CAF

CAF Pict



WAKATI macho ya mashabiki wa soka Afrika Mashariki na Kati yakielekezwa Kigali, Rwanda, kwenye mashindano ya Kombe la CECAFA Kagame, miongoni mwa mijadala inayoendelea ni maendeleo ya soka ndani ya ukanda huu na namna mataifa yanavyopambana kuzalisha vipaji pamoja na makocha bora.


Miongoni mwa wanaotazama mabadiliko hayo kwa jicho la kitaalamu ni kocha wa Bugesera FC ya Rwanda, Musa Gatera ambaye ameeleza jinsi soka la Tanzania lilivyopiga hatua kubwa katika miaka ya karibuni kupitia uwekezaji, mipango madhubuti na uendeshaji bora wa klabu.


Gatera, ambaye amewahi kutembelea Tanzania kwa shughuli mbalimbali za soka, amesema klabu za Simba na Yanga zimekuwa mfano wa kuigwa baada ya kufikia hatua ya kushindana na timu kubwa barani Afrika katika mashindano ya CAF.

“Hongera kwa soka la Tanzania. Timu hizi zina vipaji na zimepiga hatua kubwa. Kiwango walichofikia sasa ni kizuri kwa sababu wameweka mambo yao kwenye mstari,” amesema Gatera.

Kocha huyo amesema mafanikio ya Simba na Yanga hayajatokana na bahati, bali yamechangiwa na mfumo mzuri wa uendeshaji, mipango ya muda mrefu na uelewa wa soka la kisasa kama biashara.

“Mpira wa miguu leo ni sayansi; kila kitu kinachambuliwa. Wanajifunza kutoka kwa walio mbele yao ili nao waendelee kupiga hatua. Naweza kusema Simba na Yanga wametuacha sisi Rwanda kwa sababu wameelewa mpira ni nini na wameitambua biashara ya soka,” amesema.

CA 03

HARUNA, KAGERE WALIKUWA MWANZO TU

Akizungumzia wachezaji wa Rwanda waliowahi kung’ara Tanzania, akiwemo Meddie Kagere na Haruna Niyonzima, Gatera amesema bado kuna vipaji vinavyoandaliwa ambavyo vinaweza kufuata nyayo zao kutokana na mfumo mpya wa kulea vijana.

“Wale walikuwa wachezaji bora na walifanikiwa kwa sababu walikuwa na uwezo, lakini nyuma yao hakukuwa na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa tayari. Sasa tumeanza upya kwa kuanzia vijana wa miaka 14 hadi 17, na tunaamini ndani ya miaka mitatu au minne tutakuwa na wachezaji wengi zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa Rwanda imeanza kuwekeza zaidi katika programu za maendeleo ya vijana ili kuzalisha kizazi kipya cha wachezaji watakaoweza kucheza nje ya nchi.


HARUNA ANAWEZA KUWA KOCHA BORA

Akizungumzia aliyekuwa kiungo wa Rwanda pamoja na klabu za Simba na Yanga, Haruna Niyonzima, ambaye sasa anaelekea kwenye taaluma ya ukocha, Gatera amesema ana nafasi kubwa ya kufanikiwa iwapo ataendelea kujifunza na kuipenda kazi hiyo.

“Kwanza unatakiwa kuupenda ukocha. Ukipenda na ukaendelea kusoma, unaweza kufanikiwa. Wapo waliocheza mpira katika kiwango cha juu, lakini ukocha unahitaji kujifunza zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa wachezaji waliostaafu wana faida ya kuwa na uzoefu wa kufanya kazi na makocha mbalimbali.

“Haruna amefanya kazi na makocha wengi akiwa mchezaji. Akisoma vizuri na kupata elimu ya ukocha, anaweza kuwa mwalimu mzuri,” amesema.


KOZI ZA UKOCHA ZINAVYOINUA VIWANGO

Gatera amesema mafunzo ya mara kwa mara kwa makocha ni muhimu kwa sababu soka hubadilika kila siku.

“Ukiwa kocha huwezi kusema umemaliza kujifunza. Kila siku kuna jambo jipya. Kozi za maboresho zinatusaidia kukumbusha tuliyojifunza na kubadilishana mawazo na makocha wengine,” amesema.

Ameongeza kuwa uzoefu wa vitendo uwanjani ni sehemu muhimu ya kumjenga kocha bora.

“Kila unapokutana na timu tofauti unajifunza. Unaona kiwango cha mpinzani, unatambua ulipokosea na kujua unachoboresha.”


RWANDA YATUMA MAKOCHA HISPANIA

Kocha huyo pia amepongeza jitihada za Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) za kuwapeleka makocha kujifunza nje ya nchi, akitolea mfano safari ya baadhi yao kwenda Hispania kupitia ushirikiano na Atlético Madrid.

“Ni jambo zuri kwa sababu makocha wanapata fursa ya kujifunza mambo mapya. Ukocha hauna mwisho wa kujifunza; unaendelea kusoma hadi siku unapoamua kuacha kazi,” amesema.

Amesema mataifa mengine ya Afrika Mashariki yanapaswa kuiga mfumo huo ili kuongeza ubora wa makocha wa ndani.

CA 01

YANGA NA SIMBA WANA MTIHANI CAF

Kuhusu nafasi ya Yanga katika mashindano ya Afrika baada ya kufika hatua za juu katika miaka ya karibuni, Gatera amesema changamoto kubwa huanza timu zinapofika robo fainali na nusu fainali.

“Si rahisi. Kufika nusu fainali kunamaanisha tayari una kiwango kizuri, lakini huko unakutana na timu zilizozoea kushinda mataji,” amesema.

Amesema Simba na Yanga wanapaswa kuendelea kujifunza kutoka kwa klabu kubwa kama Mamelodi Sundowns na nyingine zinazotawala soka la Afrika.

“Wanapaswa kujiuliza kwa nini wanafika hatua fulani halafu wanakwama. Wakilitambua tatizo na kulifanyia kazi, watafika mbali zaidi,” amesema.

CA 02

CECAFA NI MAANDALIZI

Akizungumzia mashindano ya CECAFA Kagame Cup yanayoendelea nchini Rwanda, Gatera amesema ni fursa muhimu kwa timu kujiandaa kabla ya kuanza msimu mpya na mashindano ya CAF.

“Haya ni maandalizi mazuri kwa sababu timu zinakutana na wapinzani tofauti. Zinapata nafasi ya kubaini makosa yao kabla ya kuanza mashindano makubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa timu kama Simba, APR, Rayon Sports na nyingine zinapata nafasi ya kupima ubora wao kupitia mashindano hayo.