Kipunje anavyokula 'bata' Brazil
Muktasari:
Issa Salumu Mchinjakuku, maarufu kwa jina la Kipunje, ni yule mwamuzi wa soka ambaye habari zake kupitia gazeti hili zilisambaa nchini Tanzania mwaka jana kuwa anachezesha mechi za uswahilini huku akiwa anajihami na silaha za jadi kama panga, rungu na sime.
HAUWEZI kuamini kama kweli ni yeye. Ni kwa jinsi anavyokatisha katika mitaa ya Carvalho de Vieira na Ruo Aurora iliyopo hapa jijini Sao Paulo, Brazil akionekana mtu mstaarabu na makini, hauwezi kuamini kuwa unapishana na refa mwenye kasheshe kubwa Tanzania.
Issa Salumu Mchinjakuku, maarufu kwa jina la Kipunje, ni yule mwamuzi wa soka ambaye habari zake kupitia gazeti hili zilisambaa nchini Tanzania mwaka jana kuwa anachezesha mechi za uswahilini huku akiwa anajihami na silaha za jadi kama panga, rungu na sime.
Nimekutana naye katika mitaa ya Jiji la Sao Paulo akiwa mmoja kati ya mashuhuda wa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea hapa Brazil.
Kipunje anaonekana hana wasiwasi. Yuko peke yake. Namvamia na kuanza kumuuliza maswali tofauti ambayo Mtanzania yeyote angeweza kumuuliza.
Kwa nini yupo Sao Paulo?
Swali hili Kipunje analidaka bila ya wasiwasi. Anaonekana kuwa na uhakika na anachokizungumza. Kama unadhani kuwa ndoto za kutazama Kombe la Dunia zilikuwa zinatimizwa na matajiri, basi unakosea.
Kipunje ni kondakta wa daladala na anachezesha mechi za uswahilini kwa shida kwa ajili ya kujiongezea riziki. Pamoja na yote, Kombe la Dunia lilikuwa ndoto zake.
“Ilikuwa ndoto yangu kutazama Kombe la Dunia. Mwaka 2010 nilijipanga kwenda Afrika Kusini lakini nikakosa baadhi ya vitu muhimu nikashindwa. Mwaka huu nilifanikiwa kufanikisha vitu hivyo nikachukua visa pale ubalozini kwetu Dar es salaam na kufanikiwa kutimiza ndoto zangu,” anasema Kipunje.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuwa nje ya Tanzania. Nauli nilijaribu kuchanga mwenyewe, lakini kuna watu wawili watatu waliniongezea pesa kwa sababu walijua kuwa nilikuwa na ndoto za kuja Brazil kutazama Kombe la Dunia.”
Kumtazama Van Persie ‘Live’
Kipunje ana tiketi zake mfukoni na hakuja kibabaishaji. Alikuja kwa ajili ya kutazama mechi za Kombe la Dunia kwa uhalali kabisa bila ya kubabaisha.
“Kuna ndugu yangu huku nilipomwambia kwamba nataka kuja na nikamhakikishia kwamba ilikuwa lazima nije, alininunulia tiketi. Nina tiketi za mechi tano. Mbili kati ya hizo ile ya Chile ya Uholanzi ambayo itachezwa hapa hapa Sao Paulo na nyingine kuna ile ya Australia na Chile,” anasema Kipunje.
Hata hivyo, tayari Kipunje amekoshwa na uwezo wa waamuzi wa Kombe la Dunia ambalo amekuwa akilishuhudia nchini hapa. Anajaribu kulinganisha uwezo wake wa kuchezesha uwanjani pamoja na uwezo wa waamuzi wengine wa Tanzania dhidi ya waamuzi wa fainali hizi na anakiri kwamba mambo ni tofauti.
“Kuna tofauti kubwa. Waamuzi wa Kombe la Dunia wana uzoefu, umakini na ni wepesi sana. Wanaijua sana kazi yao aisee. Nimejifunza mambo mengi kutoka kwao,” anasema Kipunje.
Hata hivyo, Kipunje anatoa maoni yake kuhusu penalti mbili zilizozua utata katika mechi kati ya Brazil na Croatia ambayo mshambuliaji wa Brazil, Fred, alizawadiwa penalti baada ya kuvutwa na beki mmoja wa Croatia huku pia akitoa maoni yake kwa penalti waliyopewa Hispania dhidi ya Uholanzi baada ya mshambuliaji, Diego Costa kuonekana kuangushwa katika eneo la hatari.
“Kama mimi ningekuwa mwamuzi wa pambano la Brazil dhidi ya Croatia ningeipa penalti Brazil kwa sababu Fred alivutwa halafu akaachiwa. Lakini penalti ya Costa katika mechi ya Uholanzi nisingetoa. Alimdanganya mwamuzi tu yule,” anasema Kipunje kwa kujiamini.
Aitaka filimbi ya fainali
Kipunje hana hofu yoyote ya kuchezesha mechi yoyote ile ya fainali ya Kombe la Dunia. Anaweka jaketi lake vizuri na kuzungumza kwa kujiamini kabisa.
“Wanipe tu filimbi. Kama kungekuwa na uwezekano huo, sina hofu kabisa. Unajua lugha ya mpira ni ile ile tu. Kitu muhimu ni kufuata sheria za soka ambazo zipo duniani kote. Niko tayari kabisa na wala sina hofu,” anasema.
Kuthibitisha kwamba hana hofu, Kipunje amepata bahati ya kuchezesha mechi mbili za mchangani kwa raia wa kigeni wanaojiburudisha siku za wikiendi nchini Brazil huku mojawapo ikiwa kati ya Nigeria na Senegal.
“Nilichezesha vizuri kabisa. Hawakuwa na mwamuzi na nikawaambia Watanzania wenzangu wawaambie kwamba naweza kuchezesha. Nikapewa filimbi na kuchezesha vizuri tu,” anasema.
“Nigeria ilishinda 2-1 ingawa wachezaji wake ni walalamishi, lakini nimegundua kuwa wenzetu wana heshimu sana maamuzi ya mwamuzi licha ya kubishana hapa na pale. Ukitoa maamuzi analalamika kidogo tu kisha mchezo unaendelea. Hawakuwa na wasiwasi na mimi baada ya kugundua kuwa nilikuwa Mtanzania na sikuwa na upande wowote.”
Ashindwa kubeba mapanga yake Brazil
Kipunje anacheka sana baada ya kuulizwa kwanini hakuchukua mapanga yake Brazil.
“Ningepita nayo wapi? Wangeyaweka wapi katika ndege? Acha hizo bwana. Lakini unajua siku hizi sichezeshi na yale mapanga,” anaongeza Kipunje.
Kipunje ana wake wawili, mkubwa ni Sofia Said au Mama Zulfa na wa pili ni Fatina Eliaki. Anadai kwamba wake zake hawana tatizo na safari ya Brazil kwa sababu aliwaaga vizuri na ni wao ndio waliompa mkono wa kwaheri wakati akipanda teksi kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.