Kibarua cha Okello kuvunja rekodi?
Muktasari:
- Okello alijiunga na Yanga Januari 13, 2026, akitokea Vipers ya kwao Uganda, na baada ya kukaa Tanza-nia kwa siku 220, sawa na takribani miezi saba na siku nane, Agosti 21, 2026, akatambulishwa rasmi na AS FAR Rabat ya Morocco, moja ya ligi zenye ushindani Afrika.
UKIONYESHA kitu watu watakuona. Ndivyo ilivyotokea kwa Allan Okello, ambaye hakuhitaji muda mrefu tangu alipojiunga na Yanga katika dirisha dogo, kabla kiwango chake kuwavutia mabosi wa AS FAR Rabat ya Morocco iliyohitaji huduma yake.
Okello alijiunga na Yanga Januari 13, 2026, akitokea Vipers ya kwao Uganda, na baada ya kukaa Tanza-nia kwa siku 220, sawa na takribani miezi saba na siku nane, Agosti 21, 2026, akatambulishwa rasmi na AS FAR Rabat ya Morocco, moja ya ligi zenye ushindani Afrika.
Na sasa suala siyo kusajiliwa na timu hiyo, ni kuendeleza kiwango bora alichoonyesha akiwa Yanga ndani ya nusu msimu tu hadi AS FAR kuvutiwa naye. Ipo mifano ya nyota waliowahi kutikisa Ligi Kuu walipotimkia Uarabuni, wakashindwa kuonyesha kiwango chao. Sasa je, ataandika historia yake mwenyewe Morocco au ataendeleza rekodi ya baadhi ya nyota waliotoka Tanzania wakiwa kwenye kilele, wakaenda ligi za Kiarabu lakini wakashindwa kubaki kwenye kiwango kilekile?
MTEGO, KIBARUA KILIPO
Akiwa Yanga, Okello hakuhitaji muda mrefu kujitambulisha. Muda mfupi aliokaa Jangwani, alifunga mabao 14 na kutoa asisti nane katika mechi 23 za ligi, akisaidia Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu. Hiyo ndiyo rekodi aliyokwenda nayo Morocco, na ndiyo inayoweka presha kubwa kwake.
AS FAR si klabu aliyokwenda kwa bahati. Ni timu iliyofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ulio-pita, hivyo Okello anahamia mazingira ambayo kiwango kinapimwa si kwa jina tu, bali kwenye mashindano makubwa. Zaidi ya hapo, atakutana tena na kocha Pedro Gonçalves, ambaye alikuwa se-hemu ya sababu za kupelekwa Yanga na sasa amekuwa kivutio katika safari yake mpya Morocco.
Okello ameondoka Tanzania akiwa amepata kitu ambacho si rahisi kwa mchezaji wa kigeni kuaminiwa haraka.
Yanga ilimpa nafasi, naye akaonyesha kwa kufunga mabao, asisti na ubunifu. Lakini AS FAR haitakuwa Yanga.
Atakutana na kikosi kipya, ushindani mpya, lugha mpya ya mpira na wachezaji ambao nao wana malen-go yao. Hata kama kocha anamjua, Okello atalazimika kuthibitisha kwamba kiwango chake hakikutoka-na na mazingira ya Tanzania tu. Hilo ndilo eneo ambalo nyota wengine waliowahi kuondoka Ligi Kuu wamekumbana nalo.
AZIZ KI
Mfano wa hivi karibuni ni kiungo wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki aliyeondoka Yanga baada ya kuten-geneza jina kubwa Jangwani, akatimkia Wydad Casablanca. Akiwa Yanga, alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa klabu hiyo, akifikisha mechi 114, mabao 52 na asisti 32, pamoja na kusaidia klabu kushinda mataji tisa. Msimu wake wa mafanikio zaidi ulikuwa 2023/24, alipofunga mabao 21 ya ligi na kuchukua tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, MVP na kiungo bora.
Lakini safari ya Wydad haikuwa kama baadhi ya watu walivyotarajia kumuona KI aliyekuwa kwenye kilele, kama ilivyokuwa Jangwani. Baadaye alihamia Al-Ittihad Tripoli ya Libya kabla ya kurejea Yanga mwaka 2026. Hii ndiyo picha ambayo Okello anayo. Si kwamba kuondoka Yanga ni kosa. La hasha, tatizo ni kuondoka ukiwa kwenye kilele, halafu kushindwa kuendeleza kiwango ukiwa kwenye mazingira mapya.
CLATOUS CHAMA
Mwa-mba wa Lusaka aliwahi kuondoka Simba na kwenda RS Berkane kwa mkopo msimu wa 2021/22. Huko Morocco hakupata nafasi ya kuendeleza kiwango alichokuwa nacho Simba; rekodi inaonyesha alicheza mechi 10 za ligi bila kufunga bao. Baadaye akarudi Simba na kuendeleza historia yake Tanzania. Na tangu arejee wakati huo, aliwaka tena na kuisaidia Simba kucheza robo fainali tano mfululizo akiwa na ufalme wake kwenye kikosi cha Msimbazi.
JEAN BALEKE
Jean Othos Baleke naye aliondoka Tanzania akiwa ameacha picha nzuri Simba. Alikuwa kwenye kikosi cha Simba kwa mkopo kutoka TP Mazembe na alifunga mabao nane katika kipindi alichokuwa Simba. Baadaye TP Mazembe ikampeleka kwa mkopo Al-Ittihad Tripoli ya Libya Januari 2024.
Hii ni mifano inayonyesha kwamba mafanikio ya Tanzania hayawezi kuwa tiketi ya kudumu nje, hivyo Okello anapaswa kuongeza juhudi mara mbili ya zile alizokuwa anaonyesha akiwa na Wananchi.
NICKSON KIBABAGE
Nickson Kibabage ni mfano mwingine, hasa kwa sababu safari yake ilipitia Morocco. Alijiunga na Difaâ El Jadida, kisha akapelekwa kwa mkopo Youssoufia Berrechid kabla ya kurejea Tanzania.
Kibabage hakwenda Morocco akiwa amekosa uwezo. Alikwenda akiwa mmoja wa mabeki waliokuwa na kiwango kizuri Tanzania, lakini mazingira ya soka la Morocco hayakumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake.
FAIDA, KIBARUA CHAKE
Pamoja na mifano hiyo, Okello ana faida ambayo inaweza kumsaidia, kwani ni mchezaji anayekwenda AS FAR akiwa bado kwenye kasi ya ushindani. Hajaondoka Tanzania baada ya msimu mrefu wa kushuka kiwango. Ameondoka baada ya kuwa na nusu msimu uliomfanya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi Yanga.
Zaidi ya hapo, AS FAR yenyewe ilimuhitaji sana kiasi kwamba mazungumzo ya mkataba yalichukua kari-bu wiki moja kabla ya makubaliano kukamilika. Ripoti kutoka Daily Monitor zinaeleza kwamba dili hilo lilifikia thamani ya jumla ya takribani Dola 800,000 kwa mkataba wa miaka mitatu, huku ada ya uham-isho iliyolipwa Yanga ikiwa takribani Dola 500,000, kwa mujibu wa vyanzo hivyo.
Anatakiwa kuonyesha kwamba mabao 14 na asisti nane hazikuwa bahati. Anatakiwa kuonyesha kwamba ubunifu wake unaweza kufanya kazi kwenye mfumo mwingine, dhidi ya mabeki wenye vi-wango tofauti na kwenye mashindano yenye presha kubwa zaidi.
Akifanya hivyo, atakuwa amefanya kitu ambacho baadhi ya nyota waliomtangulia walishindwa kuen-dana na kasi ya Morocco. Akifanya hivyo, atavunja mwiko wa wachezaji waliotoka Tanzania wakiwa na viwango bora lakini wakashindwa.
HAWA PIA
Mbali na hao walioshindwa kuendana na ligi hiyo, wapo waliofaulu. Baadhi yao ni Simon Msuva, am-baye alijiunga na Difaa El Jadida msimu wa 2017-2020 akitokea Yanga, ambako alikuwa na kiwango bora.
Kwenye misimu mitatu aliyocheza Difaa ya Morocco, alicheza mechi 80, akifunga mabao 28, ndipo msimu uliofuata Wydad ikamnunua, ambako nako alicheza mechi 37, akifunga mabao 10 kabla ya sa-kata la kudai fedha zake kuanza kurindima. Mwingine ni Fiston Mayele, alitimka Jangwani mwaka 2023 na kujiunga na Pyramids ya Misri, ambako alikuwa na kiwango bora. Ndani ya misimu mitatu aliyocheza ligi hiyo, alicheza mechi 79, akifunga mabao 30.