King Kiba aliamsha Uhuru kwa staili ya kifalme
Muktasari:
- Msanii huyo aliteka mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Uhuru, baada ya kuingia akiwa amebebwa katika kiti cha kifalme, jambo lililoibua shangwe kwa mashabiki waliohudhuria kwa wingi katika tamasha hilo linalotimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009.
MSANII wa Bongo Fleva nchini, Ali Kiba 'King Kiba' ameibua shangwe la aina yake kwenye Uwanja wa Uhuru wakati alipoingia kuburudisha mashabiki wa Simba katika kilele cha Simba Day, kinachofanyika leo ikiwa ni miaka 90 tangu klabu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1936.
Msanii huyo aliteka mashabiki wa timu hiyo waliojitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Uhuru, baada ya kuingia akiwa amebebwa katika kiti cha kifalme, jambo lililoibua shangwe kwa mashabiki waliohudhuria kwa wingi katika tamasha hilo linalotimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009.
Baada ya kuingia uwanjani hapo, Ali Kiba aliimba nyimbo mbalimbali zikiwemo za Sinderela, Kadogo, Finale, utanionea, Bhuju, Sumu na zinginezo ambazo ziliamsha shangwe kubwa la mashabiki walioshindwa kujizuia na kuinuka katika viti vyao, huku wakiimba wote kwa pamoja.
Licha ya kuimba nyimbo mbalimbali, ila miongoni mwao zilizogusa hisia za mashabiki ni wimbo maarufu wa 'Mnyama' ambao ni maalumu kwa klabu hiyo ukiwa umebeba ujumbe wenye maana ya hakuna timu tishio zaidi ya Simba, kutokana na mafanikio yake kwa Tanzania hadi Barani Afrika.
Hata hivyo, wakati akiendelea kutoa burudani hizo, Ali Kiba alipiga kijembe cha staili yake kwa wapinzani wa Simba, Yanga, baada ya kudai yeye ni shabiki wa Simba na anajivunia timu hiyo inayotimiza miaka 90 leo tangu kuasisiwa kwake mwaka 1936.