Kifo cha Houllier chatikisa familia ya michezo
Paris, Ufaransa. Kocha wa zamani wa Liverpool na Aston Villa, Gerard Houllier amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73, ikiwa ni kwiki tatu tangu alipofanyiwa upasuaji wa moyo mjini Paris.
Mfaransa huyo, ambaye alifundisha pia Paris Saint-Germain na Lyon, ana historia ya kukimbizwa hospital, mara zote akiwa na tatizo la moyo na shinikizo la damu, lakini chanzo cha kifo hakijafahamika.
Houllier, ambaye aliiongozaLiverpool kutwaa mataji mawili 2001, anatajwa na wachezaji aliowafundisha na makocha wenzake kama kocha mwema aliyewahi kutokea ambaye mara zote ‘huwapa kipaumbele wengine kwanza’.
Shabiki huyo mkubwa wa Anfield, Houllier alishawahi kuumwa ghafla akiwa anaisimamia timu hiyo dhidi ya Leeds, 2001. Baadaye alifundisha pia Villa ambako pia alisumbuliwa na moyo na kujiuzulu na hakuwahi kufundisha tena tangu 2011.
Redio ya Ufaransa ya RMC na gazeti la michezo la L’Equipe viliripoti kwamba Houllier alifariki baada ya kufanyiwa upasuaji mjini Paris. Kwa mujibu wa mwandishi wa L’Equipe, Vincent Duluc, Houllier alifanyiwa upasuaji wiki tatu zilizopita na aliruhusiwa kutoka hospitali ya Paris kurudi nyumbani Jumapili.
Alidaiwa kutuma ujumbe wa simu wikiendi akisema: “Naumwa, lakini naamini nitapona.”
Liverpool ilitoa salamu za rambirambi kwa kocha wao wa zamanijana, waliandika: “Tunasikitika kwa kuondokewa na kocha aliyetupa mataji mawili kwa pamoja, Gerard Houllier.
“Pole kwa kila mmoja ndani ya Liverpool na klabu ipo pamoja na familia ya Gerard na rafiki zake katika kipindi hiki kigumu.”
Taarifa ya Villa ilisomeka: “Sote hapa Aston Villa tumesikitishwa na taarifa za kifo cha Gerard Houllier, aliyekuwa kocha wetu msimu wa 2010/11.
“Pole kwa familia nzima ya Gerard na tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu.”
Beki wa zamani wa Liverpool na mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Carragher, ambaye alicheza kipindi cha Houllier ndani ya Anfield, aliandika: “Hakika nimeshitushwa na taarifa za kifo cha Gerard Houllier, niliwasiliana naye wiki iliyopita tu juu ya yeye kuja Liverpool.
“Nilimpenda sana mtu huyu, amehusika kunibadilisha.”