Ken Gold , Pamba ngoma nzito Championship
Muktasari:
- Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ni kati ya tatu zitakachezwa leo, huku kesho zikipigwa mbili na raundi ya 26 itamalizika Jumatatu kwa Green Warriors kumalizana na Pan Africans inayopambana kuepuka kushuka daraja.
Ligi ya Championship imefikia patamu baada ya jana kupigwa mechi mbili, leo kuna kazi nzito wakati kinara wa msimamo wa ligi hiyo, KenGold itakapoikaribisha Pamba Jiji katika pambano litakalotoa picha halisi kwa timu hizo kwenye mbio za kupanda daraja Ligi Kuu Bara.
Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ni kati ya tatu zitakachezwa leo, huku kesho zikipigwa mbili na raundi ya 26 itamalizika Jumatatu kwa Green Warriors kumalizana na Pan Africans inayopambana kuepuka kushuka daraja.
Michezo ya leo itahusisha pia Copco ya Mwanza itakayoialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Nyamagana na maafande wa Polisi Tanzania watakuwa wenyeji wa Mbuni katika Uwanja wa Ushirika, Moshi zikiwa ni mechi za kupambana kujiweka salama kwa msimu ujao wa ligi hiyo.
Ebu turudi jijini Mbeya, KenGold inayonolewa na Jumanne Challe inaonyesha dhamira ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2024-2025 ikiwa imekusanya pointi 59 leo itakuwa na kazi ya kuongeza pointi ili kujihakikisha kutimiza ndoto za kuliongezea jiji hilo timu za Ligi Kuu.
Awali ratiba ilionyesha mechi hiyo ya KenGold na Pamba ilikuwa ipigwe jana Ijumaa sambamba na ile ya Ruvu Shooting dhidi ya Stand United, lakini ikasogezwa leo kwa sababu ya wadhamini wanaorusha mchezo huo na ile mechi ya FGA Talents na TMA iliyopangwa kesho ikasogezwa jana, ilimradi mashabiki wapate burudani ya wikiendi.
Pamba iliyohaha kupanda baada ya kusota katika ligi hiyo tangu iliposhuka mwaka 2000, yenyewe ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 54, lakini haina amani kutokana na Biashara United iliyopo ya tatu ikiwa na pointi 53 baada ya wikiendi iliyopita kuifumua Ruvu Shooting mabao 7-0 ikiitishia amani.
Mechi hito ya leo ni vita nzito kwelikweli kwa makocha wa timu hizo na hata wachezaji kila moja akitaka pointi za kuwaweka katika mstari mnyoofu wa kupanda daraja, kwani Pamba ikishinda itafikisha 57 na kujiwepa pazuri kati ya timu mbili zinazopanda moja kwa moja.
Kupoteza mchezo huo kisha Biashara itakayocheza kesho dhidi ya Mbeya Kwanza itamaanisha kuipa kazi katika mechi nne zilizosalia kukimbizana na wapinzani wao hao katika kuwania nafasi moja kwani Kengold itakuwa imeshatanguliza mkono mmoja kwenye tiketi ya kupanda kwa kufikisha pointi 62.
Kocha msaidizi wa Pamba, Renatus Shija alisema mechi ya leo ni ngumu, lakini wamejidhatiti kuweza kupata ushindi kutimiza ndoto zao, lakini wenyeji wakisema wanaendelea walipoishia wikiendi iliyopita.
Mbali na mechi hizo za leo, kesho zitapigwa mechi nyingine mbili Transit Camp iliyotoka kuitungua Pan kwa mabao 2-1 itakuwa wenyeji wa Cosmopolitan, huku Biashara ikamlizana na Mbeya Kwanza.