Kaze: Simba wepesi tu, tatizo Chama, Luis

KATIKA toleo la jana katika mahojiano maalumu na Cedric Kaze, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga aliyefurushwa wiki iliyopita, tuliona akianika kirusi kinachoitafuna timu hiyo ya Jangwani.
Alifafanua, pia juu ya ukweli wa kukwamishwa mambo mengi aliyokuwa akiyatengeneza na wachezaji wake kwa ajili ya kuifanya Yanga iwe moto na kueleza ni kazi kubwa hata kwa kocha ajaye kama ‘kirusi’ kilichopo klabuni hapo akitadhibitiwa ili mambo yaende sawa.
Katika kuhitimisha makala iliyotokana na mahojiano hayo maalumu, Kaze ameichambua Simba na kudai mechi baina yao kwake ilikuwa ndio mechi nyepesi sana, lakini kinachoiangusha Yanga ni kule kukosekana kwa watu wenyewe uwezo mkubwa kama kina Clatous Chama na Luis Miquissone. Kivipi? Endelea naye...!
UBORA WA SIMBA
“Unajua watu wanashindwa kuelewa, Yanga haiwezi kuwa bora kwa siku moja. Hivi unakumbuka Simba ilikotoka unakumbuka kina Laudit Mavugo, Emmanuel Okwi, Charles Ilanfya, Haruna Niyonzima, Joseph Owino wale Wabrazili, Waghana na wengine ambao nimewasahau hao wote walicheza Simba kwa vipindi tofauti, wakati huo ilikuwa inajaribu. Haikuwa inajua itafikia hapa ilipo sasa,” anasema na kuongeza;
“Wamepitia safari ndefu sana kuwa na timu bora, watu wa Yanga haswa viongozi na mashabiki wanapaswa kuwa watulivu na kufanya mambo kwa mipango. Wanaelekea kwenye sehemu nzuri tayari wameanza kubadili mfumo wa uendeshaji na hayo mambo mengine yanakuja kidogokidogo huwezi kufanya yote kwa wakati mmoja.”
“Nimekutolea mfano wa hao wachezaji uone Simba ilikopita mpaka ikafikia hatua sasa inafikiria nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hawana presha kwa vile wana wachezaji wengi wakubwa na machaguo mengi ambao kila mmoja anaona haina kificho hiyo.”
CHAMA NA LUIS
Kaze anasema; “Ukiangalia Simba wakimkosa Chama leo, basi wanaye Luis na Kagere ambao wanaweza kufanya lolote na kutengeneza matokeo na hata utofauti hauonekani, lakini sisi Yanga leo tukimkosa mchezaji mmoja inabidi tutumie nguvu kubwa kuibana timu ili tusitoke kwenye reli.”

Anasema Chama na Luis na wengine Simba wana viwango vikubwa kiasi ya kumrahisishia kocha wao kuwa na machaguo mawili ya kumbeba, tofauti na ilivyokuwa kwa Yanga ambayo ina pengo kubwa baina ya wachezaji wao kwa ubora wao.
Hata hivyo anasema pamoja na Simba kuwa na kina Chama, bado kwake ukimuuliza mechi iliyokuwa nyepesi kwake ndani ya siku 142 za kuinoa Yanga, atakujibu ni Kariakoo Derby.
“Lakini angalia katika mechi mbili za watani ambazo tumecheza na Simba hiyo hiyo bora tumeweza kuibana sana na haijachukua pointi tatu. Wameambulia moja tu kwenye ligi na nakwambia ukweli hata tungekutana nao mwezi Mei nlikuwa nawapiga,japo kuna watu wanaeza wasiamini,” anasema.
“Sisi tuna timu ndogo tunaijenga lakini inafanya kitu ambacho kinaonekana ukiondoa hayo matatizo madogo ya hapa na pale ya kuingiliana majukumu ya kiufundi. Yanga wanahitaji kujipanga zaidi kujenga timu na kuwa wavumilivu, wasitoe sana presha kwa wachezaji na benchi la ufundi hakuna mtu ambaye anapenda kupoteza ndio maana kila tunapoingia uwanjani tunapambana kwa kile tulichonacho.
“Tulikuwa tunafanikiwa kwa vile tuna mipango ya mchezo kwa mchezo na tunatumia kile kidogo tulichonacho kwa kiwango cha juu.”
UJUMBE KWA MASHABIKI
“Kuna kitu kimoja nimejifunza kwao wanaipenda sana timu na wanapenda sana mpira. Yaani kitu ambacho kilinishangaza zaidi ni pale kwenye fainali ya Mapinduzi baada ya kujulikana tunakwenda kucheza na Simba mambo yalibadilika kabisa mashabiki walianza kupata hamasa kubwa na presha kubwa ikaanza kwa viongozi kuanza kuandaa ule mchezo. Lakini mimi nilikuwa nachukulia kawaida sana, yaani mpaka nikashangaa kwanini hamasa imekuwa kubwa hivi kumbe wao walikuwa na wasiwasi hawakujua kama sisi tumejipangaje na lengo letu ni kushinda. Sasa baada ya kutwaa lile kombe ndio ikawa balaa zaidi, mashabiki walifurahi kwelikweli sijapata kuona. Yaani ile kitu siji kusahau. Ndio maana tukakubaliana na wachezaji kwamba lile kombe ni la mashabiki la kwetu tunakwenda kubeba lile la Ligi na FA.
“Nilishangaa zaidi tulipopokelewa pale Bandarini Dar es Salaam ule msururu wa mashabiki wanakimbia mpaka tunafika klabuni. Yaani kutokana na mapenzi yao kwa klabu hawakujali jua lilikuwa kali walitembea juani huku wakiimba nyimbo za kusifu timu yao,nilipenda sana ile na iliwapa motisha sana wachezaji wangu kuzidi kuwaheshimu mashabiki.
“Lakini nilitaka kuwapa changamoto moja mashabiki haswa wa timu yangu ya Yanga. “Wajifunze kupenda vya kwao, wawapende wachezaji wao haswa hawa wa ndani ndio cha kwao walichonacho.
“Wasiwakatishe tama wakawashusha viwango, mimi ntakupa mfano mmoja japo siwezi kutaja majina unaeza kukuta mchezaji mzawa anafanya kazi kubwa sana uwanjani kila siku.
“Hata ukimtoa unagundua kabisa kwamba kuna sehemu pamepwaya lakini huyo unakuta mashabiki hawampi umuhimu kabisa,wanamchukulia kawaida sana na hata takwimu zake hawataki hata kuzisikia. Lakini mgeni akifanya kitu kidogo cha kawaida tu wanamtukuza kwelikweli lakini hawajui wanawafanya wale wenzao wanyonge.
“Wakati mwingine inakwenda mbali zaidi wameshaambukizana mpaka huko Simba na Azam, kosa akilifanya mchezaji wa kigeni wanavyolichukulia mashabiki ni tofauti kabisa na akifanya mzawa, hii haileti picha nzuri wanapaswa kubadilika sana na kujenga tabia ya kuthamini vya kwao,hata ikiwezekana wote wawe sawa. Wasiwe na upendeleo.”
FARID NA SARPONG
“Farid inawezekana wakati mwingine hana damu ya kupendwa na mashabiki lakini hata mchezo unamkataa, mchezaji hawezi kuwa sawa siku zote. Ukimwangalia Farid Mussa akiwa mazoezi ni mchezaji mzuri sana na hata akiwa kwenye mechi anapanda vizuri, anamiliki ni mchezaji mwenye uwezo wa kufanya jukumu zaidi ya moja kwenye mechi ndio maana huwa napenda kumtumia anachokosa ni bahati ya kufunga tu. Hata Sarpong ukimuangalia kwa jicho la kufunga mabao utasema hakuna mchezaji pale lakini ukimuangalia katika jicho na akili ya kiufundi ana majukumu mengi sana pale mbele, mwili wake na nguvu zake ni faida kubwa kiufundi.
UNAKWENDA WAPI?
“Sina ofa mpaka sasa Tanzania lakini nikuhakikishie nimepata ofa kubwa tatu Afrika kwenye timu kubwa tu, nitakachofanya sasa natuliza kwanza akili nijipange upya.
“Nitaondoka wikiendi hii niende kwetu Burundi kwanza nikasalimie halafu nitarudi Tanzania niondokee hapa kurudi Canada.
“Kule Canada ndiko iliko familia yangu, miradi yangu mingi sasa nikishafika ndio nitajipanga tena kurudi Afrika. Lakini nikuhakikishie kwamba nitarudi kwenye timu kubwa ya Afrika kuja kufundisha.”