Kaze awashukia wadandiaji

SIKU moja tu baada ya Mwanaspoti kufanya mahojiano maalumu na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, kuna baadhi ya vyombo vya habari zimekuwa zikinakili mahojiano hayo na kuongeza maneno yao, jambo lililomchukia kocha huyo na kuwashukia.
Kaze, amesema anachukizwa na wanaomnukuu bila ya kufanya naye mahojiano katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari nchini ikiwa ni siku chache tu tangu mkataba wake usitishwe wa kukinoa kikosi hicho cha Wananchi.
Kocha huyo raia wa Burundi ametumia ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa Instagram kueleza hilo, huku akisema chombo pekee ambacho alifanya nacho mahojiano ni Gazeti Bora linaloongoza kwa Habari za Michezo na Burudani la Mwanaspoti pekee.
Ujumbe huo ulisomeka kwamba, "Wanaoninukuu katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu klabu ya Yanga baada ya kuachana nao wapuuzwe."
"Nimeongea na Mwanaspoti pekee, lakini naona kuna vyombo vinatumia jina langu kwa nukuu potofu. Nilitolea ufafanuzi kuhusu safari ya Saido kwenda Burundi na kuwa bado ni mchezaji wa Yanga na ufanisi wangu ndani ya Yanga. Mengine ni uzushi. Asanteni," ujumbe huo ulieleza.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na kocha huyo aliyeiongoza Yanga kwenye mechi 18 za Ligi Kuu Bara na kushinda 10, saba akipata sare na kupoteza moja mbele ya Coastal Union na kuchapishwa kuanzia jana Jumamosi na kumalizika leo Jumapili.