Kaze ataja kirusi ndani ya Yanga

KOCHA aliyeachishwa kazi na Yanga wiki iliyopita, Cedric Kaze ameibuka hadharani kupitia Mwanaspoti na kueleza mambo mazito yaliyomkuta lakini akasema Kocha mpya ajaye (Hubert Velud raia wa Ufaransa) kama atapewa uhuru kiufundi atakuwa na kazi rahisi kwa vile ameshamrahishia uwanjani.
Kaze ambaye huenda akaondoka nchini leo kwenda kwao Burundi, aliiambia Mwanaspoti kwamba tatizo kubwa lililomfanya akayumba ndani ya Yanga ni kuingiliwa katika utendaji wake.
“Unajua lazima niseme wazi kabisa, familia moja haiwezi kuwa na baba wawili lazima itayumba, hakutakuwa na maelewano kwa vile kila mmoja atakuwa anatoa maelekezo yake na yatavuruga mambo.
“Ndani ya Yanga kuna baba wawili, wenye akili watanielewa. Kocha unakaa na wachezaji wako mnapanga hili anakuja baba mwingine huku anawaambia mengine, baba mwingine anapiga simu kwa wachezaji anazungumza vitu vya ajabu kabisa ambavyo vinavuruga umoja na kutengeneza makundi ya hapa na pale,” anasema Kaze
“Lakini uzuri ni kwamba wachezaji walikuwa wanakuja wananiambia kila kitu wanachoambiwa, mnakaa kikao cha mipango yako huku pembeni anakuja mtu mwingine naye ana mambo. Nilivumilia sana na nikawa nawaelewesha wachezaji wangu na uzuri walikuwa wananielewa, ingawa wakati mwingine binadamu unaelewa walivyo. Kwa hali hii ya muingiliano na watu kuingilia mambo ya kiufundi na wachezaji Yanga haiwezi kufika mbali.”
Kaze anasisitiza kwa kusema: “Ilifika mpaka wakati mtu anapiga simu eti usimchezeshe huyo ni Simba. Vitu vya ajabu kabisa kwenye hii dunia nimevikuta Yanga. Ninakaa nazungumza na wachezaji wangu, lakini mtu anapiga simu anachunguza kutaka kujua kitu hayo yanamhusu nini? Na akishajua anaanza kuingiza mambo yake mengine.
“Nataka niwaambie mashabiki na wanachama wa Yanga kwamba mimi Kaze niliipenda sana timu yao na nimefanya kila kinachowe zekana kuwapa raha ndio maana sijafungwa na Simba, nimewapa Kombe moja la Mapinduzi, nimeacha timu inaongoza ligi, wasiumie. Wasisononeke. Ila wasikitike jinsi timu yao inavyoendeshwa. Kocha yeyote hawezi kufanikiwa kama hapewi nafasi ya kuwa huru kwa mipango yake na wachezaji wake.
“Mimi ni kocha hata kama nisipoendelea kufanya kazi hii, nitafanya biashara zangu. Yanga itabaki milele, ubingwa wanaweza kuchukua msimu huu kwenye ligi hata FA, lakini waangalie muundo wa timu yao pande zote. Wanayanga wawe na maono ya mbali zaidi na nje ya timu yao, wajitahidi kuwa na watu sahihi na wanaojitambua kwenye nafasi walizowapa. Yanga ni kubwa sana lazima iwe na watu makini.”
NIDHAMU KAMBINI
Juu na nidhamu ndani ya timu hiyo kocha huyo anafunguka: “Katika muda wangu wote ndani ya Yanga nilijitahidi sana kulinda nidhamu na kuhakikisha kikosi kina usawa, kila mmoja anapata nafasi kutokana na uwezo wake na hata kama haendi sawa namwambia ukweli nikiwa mimi na yeye na anajirekebisha, maisha yanaendelea.”
“Sio kweli kwamba kulikuwa na tatizo la nidhamu ndani ya timu kama baadhi ya viongozi wanavyodai. Kuna tatizo dogo lilianza kujitokeza kutokana yaleyale niliyokuwa nakwambia kwamba huyu baba wa pili alikuwa anasambaza maneno ya hapa na pale na kutaka mchezaji au wachezaji fulani wawe spesho kuliko wengine, hili nililikatakaa kabisa na mpaka wananitoa ndio ulikuwa msimamo wangu,” anasema Kaze, raia wa Burundi aliyewahi kuzinoa timu karibu zote za soka za Taifa za Burundi.
TIMU KUYUMBA
Kuhusu tatizo la timu kuyumba, alisema: “Tatizo ni presha. Baadhi ya wachezaji wameshindwa kuhimili presha ya timu kubwa kama Yanga, inapotokea timu iko nyuma kwa matokeo au tulipoteza mchezo uliopita wanapoanza mchezo mwingine wanakuwa kwenye presha sana. Nimejitahidi sana kuitoa hiyo hali kuanzia mazoezini mpaka kambini kwa kuzungumza na mmojammoja lakini wakati mwingine inatokea tena wakati timu ikiwa kwenye presha ya mashabiki uwanjani, baadhi ya wachezaji walikuwa wanashindwa kubeba uhalisia wa timu kubwa, wanashindwa kuelewa kwamba sasa wako Yanga na wanapaswa kufanya nini wanapokuwa kwenye presha kubwa hata kama tumepoteza mpira au tuko nyuma kwa matokeo.
“Sasa inapofika kwenye hatua kama hiyo ndipo kama timu mnakuwa mnahitaji watu kama Saido (Ntibazonkiza) na Yacouba aliyeko fiti. Na hata ukiangalia katika mechi zote walizocheza timu ilikuwa tofauti kabisa na hatukuwa kwenye wakati mgumu kama hizi mechi za mzunguko wa pili. Lakini bado tulipambana kila mchezaji alijituma kwa nguvu zake zote kwa masilahi ya Yanga. Ila wakati mwingine kiufundi ndiyo hivyo uwezo unakuwa umeishia hapo na nataka nikuhakikishie kwamba japo tulikuwa kwenye wakati mgumu, lakini tulikuwa na mipango mizuri na tulikuwa tunatoka kwenye hali muda si mrefu angalia mechi na Polisi tulivyocheza. Ni kosa moja tu la dakika za mwisho tena tulilipigia kelele mno kambini ndilo lililokwenda kujirudia.”
ULIFANYA USAJILI?
“Nikwambie ukweli, mimi nimesajili wachezaji watatu tu Yanga Saido, Fiston na Dickson Job. Hao wengine wote niliwakuta na kama kiongozi hata kama hawakuwa na ubora wa staili yangu ya mchezo nilitakiwa kuwaingiza kwenye mipango yangu kwa namna yoyote ile timu ipate matokeo. Hakukuwa na namna na simaanishi kwamba walikuwa wachezaji wabaya hapa ila kiuhalisia kwa kiwango cha Yanga baadhi yao walikuwa wa wastani. “Yanga ni timu kubwa yenye presha inahitaji watu wa kazi, wachezaji ambao muda wowote wanaweza kufanya lolote bila kukosekana kwa mtu mmoja au wawili. Ilipofika kwenye dirisha dogo nikapendekeza wachezaji watano wauzwe ili tuingize nguvu mpya zaidi kwavile tuliona kabisa mzunguko wa pili mambo yatakuwa magumu sana na timu zitakuwa zimeimarika zaidi, yale mapendekezo yangu hayakutekelezwa. Ikabidi niingize watatu tu wapya. Kwanza kuboresha pale kwenye ukuta kwa kumtumia Job ambaye hata umri wake ni mdogo na atacheza miaka mingi,” anasema.
“Lengo ni kucheza staili yangu ya soka ya kumiliki mpira na kule mbele na kati tuwe na watu watulivu wanaoweza kumiliki na kusambulia kwa aina ya viwanja na timu za Tanzania na baada ya msimu tuangalie nini cha kufanya kuelekea kimataifa.”
GSM VIPI
“Hawa kama wadhamini nimefanya nao kazi vizuri kwa vile ndiyo walionileta Tanzania lakini nilikuwa na uhusiano mzuri pia na wadhamini wengine wa klabu.”
UBINGWA
“Nilijua kabisa siwezi kukosa ubingwa pamoja na Kombe la FA. Tulijua kabisa kwamba Simba watakuja kwa nguvu sana mzunguko wa pili ila hesabu ilikuwa hata kama wasipopoteza mchezo lakini tukikutana nao angalau tuwe juu yao kwa pointi tatu kwavile lazima nilikuwa naenda kuwafunga,ningekuwa pointi sita juu yao na mbio zingeendelea. Hata kama ingetokea bahati mbaya lakini tungetofautiana kwa pointi tatu au mbili mwisho wa msimu na tusingeshindwa kubeba FA.”
USHIKAJI NA WACHEZAJI
“Hawa wachezaji ni binadamu, siyo watumwa wala mashine. Hata mashine kuna muda inazimwa inafanyiwa sevisi. Unahitaji kuwapa malengo lakini wakishafanya kazi wanapaswa pia kuwa na muda wa kupumzika na nilikuwa nawapa siku mbili wakasalimie familia zao. Sikuona kama hilo ni tatizo ingawa baadhi ya viongozi haohao wanaonisema vibaya walilipinga wakitaka timu ishinde kambini msimu mzima, nilikataa nikawaambia nawajua wachezaji na hilo mnalotaka halipo duniani popote.”
KOCHA MSAIDIZI
“Kama kuna kitu ambacho nilikumbana na figisu nyingi ni hili la ajira ya Kocha Msaidizi. Yanga simu zilikuwa nyingi kweli, kila kiongozi ana Kocha wake lakini nikiangalia wote sikuona mtu wa kunifaa. Nilitaka mtu mwenye maono ya mbali, anayejua soka la kisasa, aliyecheza mbali zaidi ya wachezaji wote niliona ndio maana baada ya usaili nikamchukua Nizar ambaye pia nilidhani angekuja kuwa thamani kubwa kwa Yanga na timu ya taifa miaka ijayo. Sikujali hata walipoanza kusambaza kile kipande wakidai kwamba yeye ni timu pinzani, ule ulikuwa ni uzushi tu. Watanzania lazima ifike sehemu tubadilike kifikra kama tunataka kwenda mbali zaidi, haya mambo ya kuhisi vitu bila kuwa na uhakika navyo yanaturudisha sana nyuma, tuachane na Usimba na UYanga tujikite kwenye misingi ya soka.
“Yule Nizar alikuwa ana msaada mkubwa sana kwa wachezaji, anawapa kitu ambacho ni halisi kabisa. Hata Yule Eden Mortosi wa viungo ambaye nilimtoa Canada, ana vitu vya tofauti sana na ndio maana umeona wamekuja kumrudisha tena.”
Kaze ameizungumzia Simba na kuichambua kwa mapana, je unajua ameichambuaje? Kwa Maoni tutumie 0658376417
ITAENDELEA KESHO