Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kagere: Mo Dewji ni ‘Game Changer’

KAGERE Pict

Muktasari:

  • Kwa Kagere, uwekezaji wa Dewji ndani ya Simba ulikuwa mwanzo wa mapinduzi yaliyobadili sura ya soka la Tanzania na kuifanya kuwa miongoni mwa timu zinazotajwa kwa heshima Afrika.

MEDDIE Kagere ameshuhudia mengi ndani ya soka la Afrika Mashariki na Kati. Amefunga mabao Rwanda, Kenya na Tanzania, lakini anasema jambo moja ambalo haliwezi kulinganishwa na mambo mengine yote aliyoyaona katika safari yake ya soka. Ni uwekezaji wa Mohammed Dewji ndani ya Simba.

Kwa Kagere, uwekezaji wa Dewji ndani ya Simba ulikuwa mwanzo wa mapinduzi yaliyobadili sura ya soka la Tanzania na kuifanya kuwa miongoni mwa timu zinazotajwa kwa heshima Afrika.

Kagere anatumia neno moja kumuelezea mfanyabiashara huyo ambaye ni mwekezajia wa klabu hiyo kuwa ni “Game Changer.”

Mchezaji huyo anasema alipojiunga na Simba 2018, aliikuta imeanza kuingia zama mpya za uwekezaji mkubwa.

Wachezaji wa kiwango cha juu walianza kusajiliwa mmoja baada ya mwingine, mazingira ya kazi yaliboreshwa na malengo ya klabu yakabadilika kutoka kushindania mataji ya ndani na kuanza kulenga mafanikio makubwa kwenye mashindano ya Afrika.

Anasema Mo Dewji alitambua jambo ambalo wengi hawakuliona.

MO 02

“Ukitaka kitu kikubwa lazima uwekeze kikubwa. Huwezi kutaka mafanikio makubwa wakati unawekeza kidogo,” anasema Kagere.

Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo, usajili wa nyota kama Clatous Chama, Pascal Wawa, yeye na wengine haukuwa matumizi yasiyo na mpango, bali sehemu ya mkakati wa kuijenga Simba kuwa timu yenye uwezo wa kushindana Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kagere anaamini watu wengi waliona fedha zikitumika, lakini hawakuona picha kubwa iliyokuwa mbele.

Anasema Dewji hakuangalia gharama za usajili pekee, bali aliona mapato ambayo yangerejea kupitia mafanikio ya timu.

“Ukifika hatua ya makundi kuna fedha. Ukifika robo fainali kuna fedha nyingine. Kadri unavyosonga mbele ndivyo mapato yanavyoongezeka,” anasema mchezaji huyo.

Kwa mtazamo wake, hiyo ndiyo ilikuwa siri ya mafanikio akiamini uwekezaji mkubwa huzaa matunda makubwa.

Kagere analinganisha falsafa hiyo na klabu kubwa za Ulaya, akisema timu kama Real Madrid zinapotumia fedha nyingi kusajili nyota hazifanyi hivyo kwa kubahatisha, bali zinafahamu mapato yatakayopatikana kupitia mauzo ya jezi, udhamini na ongezeko la thamani ya klabu.

Kwa mtazamo wake, ndivyo Dewji alivyofikiria kuhusu Simba. Hakutumia fedha kwa hasara, bali alikuwa akiwekeza na uwekezaji huo ulianza kuonyesha matokeo.

MO 03

Simba iliingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na baadaye robo fainali, huku ikianza kujijengea heshima mpya mbele ya vigogo vya Afrika vilivyokuwa vikipoteza mechi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Lakini, Kagere anaamini athari kubwa zaidi haikuishia Msimbazi. Anasema mafanikio hayo yaliifanya Yanga ibadili namna ilivyokuwa inafikiria.

Kwa mara ya kwanza, wapinzani wao wakaanza kuamini nao wanaweza kufika mbali katika mashi-ndano ya Afrika.

“Yanga waliona kama Simba wanafanya vizuri Afrika, kwa nini sisi tushindwe?” anasema Kagere. Ndipo mbio mpya za uwekezaji zilipoanza.

KAGE 01

Kwa Kagere, hapo ndipo ushindani wa kweli ulipozaliwa. Haikuwa tena vita ya ubingwa wa ndani, bali nani angefika mbali zaidi Afrika.

Anasema kila mafanikio ya Simba yaliilazimisha Yanga kuongeza kiwango chake na kila mafanikio ya Yanga yaliisukuma Simba kufanya vizuri zaidi.

Ndiyo sababu leo Tanzania imekuwa na klabu zinazoheshimika katika mashindano ya CAF.

Anasema ushindani huo umeongeza ubora wa ligi nzima na klabu nyingine kama Azam FC na Singida Black Stars zimeanza kuongeza uwekezaji ili zisiwe nyuma.

Kwa Kagere, hilo ndilo jambo muhimu zaidi na kadri timu nyingi zinavyowekeza, ndivyo ushindani unavyoongezeka na ubora wa ligi unavyopanda.

Anasema hatua ya robo fainali ya mashindano ya CAF kwa Simba ambayo zamani ilikuwa ndoto sasa imekuwa jambo linalowezekana na linalotarajiwa.

Anasema sasa malengo yamehamia hatua nyingine, ambayo ni kutwaa ubingwa wa Afrika.