Vita ya ubingwa Kagame yachukua sura mpya
Muktasari:
- Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Jamus SC ya Sudan Kusini na Al Hilal ya Sudan ndizo zimekata tiketi ya kucheza nusu fainali, mechi zitakazopigwa Agosti 4, 2026.
BAADA ya siku 10 za ushindani mkali zilizoambatana na jumla ya mabao 42 katika hatua ya makundi, matokeo ya kushtua na kuzaliwa kwa nyota wapya, michuano ya Kombe la CECAFA Kagame 2026, sasa imeingia kwenye hatua ya nusu fainali kuelekea kumsaka bingwa huku timu nne zikibaki kwenye mbio za kutwaa taji hilo.
Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Jamus SC ya Sudan Kusini na Al Hilal ya Sudan ndizo zimekata tiketi ya kucheza nusu fainali, mechi zitakazopigwa Agosti 4, 2026.
Wenyeji Rayon Sports, ndiyo timu yenye rekodi bora zaidi katika hatua ya makundi. Miamba hiyo ya soka la Rwanda ilimaliza Kundi C ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu dhidi ya KVZ (2-0) ya Zanzibar, kisha Tusker (1-0) ya Kenya kabla ya kuhitimisha safari yao kwa kuifunga Al Hilal ya Sudan bao 1-0.
Bao pekee la Atisso Kodjo lililofungwa mapema katika mchezo huo liliihakikishia Rayon Sports ushindi wa tatu mfululizo na kuifanya kuwa timu pekee iliyomaliza hatua ya makundi ikiwa na asilimia 100 ya ushindi.
Rayon Sports sasa itakutana na Jamus SC ya Sudan Kusini katika mchezo wa pili wa nusu fainali, pambano ambalo wengi hawakulitarajia kabla ya kuanza kwa mashindano.
Jamus imekuwa gumzo kwenye michuano ya Kagame mwaka huu baada ya kuibuka kama timu tishio ikipenya kwenye kundi B ambalo lilikuwa na bingwa wa kihistoria, Simba na aliyekuwa bingwa mtetezi, Singida Black Stars.
Wawakilishi hao wa Sudan Kusini waliingia kwenye mashindano bila kupewa nafasi kubwa, lakini wakawashangaza wengi kwa kufuzu hatua ya nusu fainali.
Miongoni mwa matokeo yaliyowafanya watu waanze kuiheshimu Jamus ni ushindi dhidi ya Singida Black Stars, jambo lililoonyesha kuwa timu hiyo haikushiriki mashindano kwa bahati mbaya, bali ilikuwa na uwezo wa kushindana na yeyote.
Kocha wa Rayon Sports, Christian Francis Haringingo, alisema ameridhishwa na namna kikosi chake kilivyomaliza hatua ya makundi, lakini amesisitiza kuwa kazi kubwa ndiyo inaanza sasa.
“Hii ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya, tumefanikiwa kushinda mechi zote tatu na sasa tuko tayari kukutana na timu yoyote katika hatua ya nusu fainali,” alisema Haringingo.
Wakati Rayon Sports ikijivunia rekodi safi, Al Hilal nayo imefanikiwa kufuzu licha ya kupoteza mchezo wake wa mwisho dhidi ya wenyeji hao.
Miamba hiyo ya Sudan imekata tiketi ya nusu fainali kama timu bora iliyomaliza nafasi ya pili, baada ya kukusanya pointi sita na kuwa na tofauti nzuri ya mabao kuliko timu nyingine zilizoshika nafasi hiyo.
Hatua hiyo imefanya kuwepo kwa mechi nyingine kubwa kati ya Al Hilal na Gor Mahia, mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na uzoefu wa timu hizo katika mashindano ya kimataifa.
Gor Mahia imeingia kwenye nusu fainali ikiwa na matumaini ya kurejesha makali yake kwenye Kagame ikiwa kinara wa kundi A huku Al Hilal ikisaka kuthibitisha kuwa kufuzu kwake hakukutokana na bahati bali ubora wa kikosi chake.
Mbali na timu zilizofuzu, mashindano hayo pia yameshuhudia timu kadhaa zikitumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya.
Miongoni mwao ni Tusker FC ya Kenya ambayo ilihitimisha ushiriki wake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ ya Zanzibar kupitia mabao ya Ian Simiyu na Victor Mbaoma.
Hata hivyo ushindi huo haukutosha kuivusha Tusker hatua ya makundi na sasa klabu hiyo imeelekeza nguvu zake kwenye maandalizi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba SC utakaochezwa Agosti 8 jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Simba Day.
Kwa upande wa KVZ ya Zanzibar, mashindano hayo yamewapa somo la kutosha baada ya kumaliza bila pointi yoyote. Timu hiyo ilipoteza mechi zote tatu, haikufunga bao hata moja na iliruhusu mabao manane, rekodi iliyoifanya kuaga mapema.
Kadiri mashindano yanavyokaribia tamati, macho ya mashabiki wengi sasa yataelekezwa kwenye mechi hizo ambapo timu nne zilizosalia zitapambana kuwania nafasi ya kucheza fainali.
Kwa Rayon Sports ni nafasi ya kutwaa ubingwa mbele ya mashabiki wake. Kwa Jamus ni fursa ya kuendeleza simulizi ya timu ambayo haikuwa ikipewa nafasi ikifanya maajabu. Gor Mahia inataka kurejesha heshima ya soka la Kenya huku Al Hilal ikisaka kuthibitisha kuwa bado ni moja ya klabu kubwa zaidi katika ukanda wa CECAFA.
WASIKIE KAGERE, NIYONZIMA
Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Rwanda, Meddie Kagere na Haruna Niyonzima, wamesema hatua hiyo itakuwa kipimo halisi cha ubora wa timu nne zilizobaki kwenye mashindano hayo.
Kagere ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Simba na Namungo za Tanzania Bara, alisema anafurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na Rayon Sports tangu kuanza kwa mashindano, akiamini ushindi wa mechi zote tatu za hatua ya makundi umeipa morali kubwa kuelekea mchezo dhidi ya Jamus SC ya Sudan Kusini.
“Tutashuhudia mechi nzuri zaidi katika hatua ya nusu fainali kutokana na timu ambazo zimefuzu, wameonyesha kuwa wanastahili kuwa hatua hii kwa kile walichofanya hatua ya makundi,” alisema Kagere.
Kagere alisema pamoja na Rayon Sports kupewa nafasi kubwa kutokana na kucheza nyumbani, haitakuwa na kazi rahisi kwani Jamus imeonyesha uwezo mkubwa kwa kuziondoa kwenye hesabu baadhi ya timu zilizokuwa zinapewa nafasi kubwa kabla ya mashindano kuanza.
Naye Niyonzima ambaye aliwika akiwa na Simba na Yanga, alisema mechi za nusu fainali hazina nafasi ya makosa, akieleza kuwa timu yoyote itakayoshindwa kutumia nafasi chache itajikuta ikitolewa.
“Uzoefu wa Gor Mahia na Al Hilal unafanya pambano lao kuwa gumu kutabirika, wote wanavikosi bora na wachezaji mmoja mmoja wenye uwezo mkubwa,” alisema.
Niyonzima alisema amefurahishwa na kiwango cha timu za ukanda wa CECAFA katika mashindano ya mwaka huu, akieleza kuwa ushindani ulioshuhudiwa unaonyesha maendeleo ya soka la Afrika Mashariki na Kati huku timu nyingi zikicheza soka la kuvutia na lenye ushindani.
Nyota hao wa zamani wa Amavubi walikubaliana kuwa kufuzu kwa Jamus SC ni moja ya matukio makubwa ya mashindano hayo, wakisema timu hiyo imeonyesha kuwa katika soka la sasa hakuna timu ndogo ikiwa maandalizi na nidhamu vinazingatiwa.