Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi kabambe za Simba Day tangu mwaka 2009

SIMBA DAY Pict

Muktasari:

  • Lengo kubwa la tamasha hilo, ni kutambulisha pia wachezaji wapya watakaokichezea kikosi hicho kwa msimu ujao, wanachama kutambuana na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji kutoka kila maeneo.

NI mwaka wa 17 tangu kuanzishwa rasmi kwa Tamasha la Simba Day mwaka 2009, chini ya Mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo, Hassan Dalali na aliyekuwa katibu wake mkuu, Mwina Kaduguda, likiwa ni tukio kubwa lililojizoelea umaarufu hapa nchini.

Lengo kubwa la tamasha hilo, ni kutambulisha pia wachezaji wapya watakaokichezea kikosi hicho kwa msimu ujao, wanachama kutambuana na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji kutoka kila maeneo.

Katika makala haya, Mwanaspoti linakuletea orodha na matokeo ya mechi zote 17, zilizopita ambazo Simba ilicheza kwenye tamasha hilo, huku rekodi zikionyesha kati ya hizo imeshinda 11, sare mbili na kupoteza nne tangu mwaka 2009.


Simba 1-0 SC Villa (2009)

Hili ndilo lililokuwa pambano la kwanza la 'Simba Day' na timu hiyo iliialika SC Villa kutoka Uganda katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru (enzi hizo ukiitwa Uwanja wa Taifa) na miamba hiyo kushinda kwa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa dakika ya nane tu ya mechi na aliyekuwa kiungo nyota wa timu hiyo, Mkenya Hilary Echessa, akiwa ndio kwanza amesajiliwa kutoka SC Villa, huku kipindi hicho Simba ilikuwa chini ya Kocha Mkuu raia wa Zambia, Patrick Phiri.

Msimu huo utakumbukwa zaidi kwani Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza mechi na kati ya 22, ilishinda 20 na kutoka sare mbili, huku nyota wa Uganda, Emmanuel Okwi na Joseph Owino wakisajiliwa kwa mara ya kwanza kikosini.


Simba 0-0 Express (2010)

Hii ndio mechi pekee ya Simba iliyoshindwa kutoa mshindi, kwani Simba ikiadhimisha mwaka wake wa pili wa tamasha hilo ililazimishwa suluhu na vijana hao wa Uganda na mechi ilipigwa Uwanja wa Uhuru, enzi hizo ukiitwa Uwanja wa Taifa.

Safari hii Simba ilikuwa pia chini ya Kocha Patrick Phiri na iliundwa na nyota kama Ally Mustafa 'Bathez', Joseph Owino, Mohamed Banka, Rashid Gumbo, Emmanuel Okwi, Patrick Ochan, Shija Mkina, Amri Kiemba, Mussa Hassan Mgosi na Jerry Santo.

SIMBA D 06

Simba 0-1 Victors FC (2011)

Kama ilivyokuwa kwa misimu miwili ya Simba Day, kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kiliialika pia timu ya Uganda na safari hii ilikuwa ni zamu ya Victors FC, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Kwa mara ya kwanza, Simba ilishindwa kutamba na kushuhudia ikipoteza mechi hiyo kwa kuchapwa bao 1-0, la dakika ya 70, kwa mkwaju wa penalti na nyota, Patrick Sembuya na utakumbuka enzi hizo Kocha Mkuu alikuwa ni Mserbia Milovan Cirkovic.


Simba 1-3 Nairobi City Stars (2012)

Simba chini ya Kocha Cirkovic iliendelea kuteseka tena kwa kufungwa mabao 3-1 kutoka kwa vijana wa Nairobi City Stars ya Kenya, ikiwa ni kichapo cha pili kwa kikosi hicho baada ya mwaka 2011, kuchapwa pia bao 1-0 na Victors FC ya Uganda.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilitangulia kupata bao la Mzambia Felix Sunzu dakika ya 15, kisha wageni kuchomoa kupitia kwa, Duncan Owiti dakika ya 57, Bruno Okullu dakika ya 69 na Boniphace Onyango dakika ya 79.


Simba 4-1 SC Villa (2013)

Kipigo cha Wakenya kiliiamsha Simba na katika tamasha la mwaka huo, iliwaalika tena SC Villa ya Uganda na kushinda mabao 4-1.

Pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ilikuwa chini ya Kocha mzawa Abdallah 'King' Kibadeni aliyechukua nafasi ya Cirkovic na chipukizi wa kipindi hicho, Jonas Mkude alifungua pazia kwa bao la dakika ya 43.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na William Lucian 'Gallas dakika ya 53, huku Betram Mombeki akifunga mawili dakika ya 70 na 72.

SIMBA D 02

Simba 0-3 ZESCO FC (2014)

Tanesco ya Zambia, Zesco FC ilifanya kufuru kwa kuitibulia Simba sherehe hizo kwenye tamasha hilo ambalo lilikuwa ni la sita kwake kufanyika kwa kuinyoosha kwa mabao 3-0, enzi hizo timu hiyo ikiwa chini ya Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic.

Wazambia hao walipata mabao kupitia kwa Jackson Mwanza dakika ya 14, Clatous Chama anayeichezea kwa sasa Simba akafunga la pili kwa penalti ya dakika ya 64, kisha, Mayban Mwamba akatupia tena la tatu dakika ya 90 na kupeleka kilio Msimbazi.


Simba 1-0 SC Villa (2015)

Tamasha la saba ya Simba Day liliishuhudia SC Villa ikirudi tena nchini kwa mara ya tatu kuvaana na Simba na kama ilivyo kawaida iliendeleza uteja na kukubali kichapo cha bao 1-0, lililofungwa na kiungo nyota, Awadh Juma katika dakika ya 89.


Simba 4-0 AFC Leopards (2016)

Katika mechi hii iliyokuwa ya nane kwa Simba kuadhimisha siku yao, ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya.

Ibrahim Ajibu ndiye aliyekuwa shujaa wa mechi hiyo kwa kufunga mabao mawili, huku straika raia wa Burundi aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Vital'O FC, Laudit Mavugo akionyesha kiwango bora na kufunga bao moja.

Bao lingine la kikosi hicho lilifungwa na winga, Shiza Kichuya aliyekuwa akiicheza timu hiyo kwa mara ya kwanza akitokea Mtibwa Sugar, japo kwa sasa nyota huyo anaichezea Coastal Union ya jijini Tanga aliyojiunga nayo akitokea JKT Tanzania.

SIMBA D 03

Simba 1-0 Rayon Sports (2017)

Mwaka huu Simba iliialika kikosi cha Rayon Sports ya Rwanda na ilishinda bao 1-0 lililofungwa na aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Mohammed Ibrahim 'Mo' dakika ya 15, akipokea pasi iliyopigwa na mshambuliaji raia wa Uganda, Emmanuel Okwi.


Simba 1-1 Asante Kotoko (2018)

Hii ilikuwa ni mechi ya pili kwa Simba kucheza na timu kutoka nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Zesco ya Zambia mwaka 2014 na ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Asante Kotoko ya Ghana kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa).

Asante ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 44 kupitia kwa Obed Owusu na Simba kusawazisha kupitia kwa Emmanuel Okwi dakika ya 76, huku ikishuhudia aliyekuwa nyota wa kikosi hicho cha Msimbazi, Adam Salamba akikosa penalti dakika ya 87.


Simba 3-1 Power Dynamos (2019)

Ikiwa katika kiwango bora, Simba ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamos kutoka Zambia huku, Meddie Kagere akifunga yote matatu dakika ya 3, 58 na 73 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika tamasha hilo kufunga (Hat-Trick).


Simba 6-0 Vital'O FC (2020)

Mwaka huo Vital'O FC ya Burundi ilikumbana na kichapo cha kupoteza mabao 6-0, yaliyofungwa na waliokuwa mastaa wa kikosi hicho, Bernard Morrison, John Bocco, Ibrahim Ajibu, Chris Mugalu, Charles Ilanfya na Clatous Chama aliyepo hadi sasa.

Ukiachana na ushindi huo ilioupata na kuwapa furaha mashabiki waliojitokeza kwa wingi ila viongozi wa Simba walimualika msanii mkubwa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambaye siku hiyo alitua kwa helikopta, ingawa kwa sasa ameshahamia Yanga.

SIMBA D 04

Simba 0-1 TP Mazembe (2021)

Haukuwa mwaka mzuri kwenye tamasha hilo, baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya wageni zao TP Mazembe kutoka DR Congo.

Katika tamasha hili bao la wageni lilifungwa kwa staili ya Tik-Taka na mshambuliaji nyota, Mkongomani Jean Baleke ambaye baadaye ilimsajili kuichezea timu hiyo, kisha kujiunga na Yanga ambako pia ameshaondoka.


Simba 2-0 St George (2022)

Mwaka huu ulikuwa ni mzuri sana kwa Simba kwani walirudisha matumaini kwa mashabiki zao kwenye tamasha hilo na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya St George kutoka Ethiopia yaliyowekwa kimiani na mastaa, Kibu Denis na Nelson Okwa.


Simba 2-0 Power Dynamos (2023)

Baada ya Power Dynamos kuchapwa mabao 3-1 mwaka 2019, ilishindwa kutamba dhidi ya Simba na kuendeleza uteja wa kufungwa tena mabao 2-0 ya Leandre Onana dakika ya tano tu na Fabrice Ngoma dakika ya 75.

Katika mechi hiyo, Simba iliibuka na ushindi huo mbele ya Rais wa Tanzania awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mbali na Onana na Ngoma waliong'ara ila wengine ni Che Malone Fondoh na Luis Miquissone.

SIMBA D 05

Simba 2-0 APR FC (2024)

Simba iliingia katika mechi hiyo ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini aliyetambulishwa Julai 5, 2024, akichukua nafasi ya Mualgeria Abdelhak Benchikha aliyeondoka kikosini, Aprili 28, 2024.

Fadlu alitambulishwa ndani ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi ikiwa ni muda mfupi tangu aipe ubingwa wa Ligi Kuu Morocco 'Botola Pro', Raja Casablanca akiwa ni msaidizi wa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mjerumani Josef Zinnbauer.

Kocha huyo alianza vizuri baada ya Simba kushinda mabao 2-0, dhidi ya mabingwa wa Rwanda APR FC, yaliyofungwa na Debora Fernandes Mavambo dakika ya 47 akiwa ni mchezaji mpya aliyetokea Mutondo Stars FC ya Zambia na Edwin Balua dakika ya 67.

Katika mechi hiyo, mshambuliaji mpya wa Simba, Mganda Steven Dese Mukwala aliyesajiliwa na kikosi hicho akitokea Asante Kotoko ya Ghana, alianza vibaya maisha yake ndani ya timu hiyo ya Msimbazi baada ya kukosa mkwaju wa penalti dakika ya 44.


Simba 2-0 Gor Mahia FC (2025)

Katika mechi hii iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Septemba 10, 2025, Simba iliendelea kufanya vizuri mbele ya mashabiki 60,000 na kikosi hicho cha Kocha Fadlu Davids kilishinda mabao 2-0, dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.

Mabao ya Simba yalifungwa na Abdulrazack Hamza dakika ya 7 na Steven Mukwala dakika ya 49, huku nyota wapya, Rushine De Reuck, Naby Camara, Neo Maema, Anthony Mligo, Jonathan Sowah, Morice Abraham na Seleman Mwalimu 'Gomez' wakivutia wengi.


Simba Vs Kenya Police FC (2026)

Hii ni mechi ya 18 kwa Simba kucheza katika kilele cha Simba Day na kwa mwaka 2026, imeialika mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2024-2025, Kenya Police FC, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Agosti 8, 2026.

Tamasha hili linakuwa ni la kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Steven Barker aliyejiunga rasmi na kikosi hicho, Desemba 19, 2025, akitokea Stellenbosch FC ya kwao Afrika Kusini, aliyechukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyeondoka Desemba 2, 2025.

Licha ya mashabiki kuona wachezaji wapya wakicheza Kombe la Kagame 2026, lililofanyika Rwanda, ila wanahitaji kuwaona zaidi, ambao ni Kelvin Nashon, Nathaniel Chilambo, Bakari Msimu, Keletso Makgalwa, Ibraheem Jabaar na Ibrahim Doumbia.