Kagera Sugar katika matumaini mapya msimu wa 2026-2027
Muktasari:
- Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
KLABU ya Kagera Sugar maarufu kwa jina la utani la ‘Wanankurukumbi’, ni timu kutoka Mkoa wa Kagera, uliopo Kanda ya Ziwa iliyobeba matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya msimu wa 2026-2027, hususani Ligi Kuu Bara.
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, amekirejesha tena kikosi hicho baada ya mwenendo mzuri kwa msimu wa 2025-2026.
Katika Championship msimu wa 2025-2026, Kagera ilimaliza nafasi ya pili na pointi 72, baada ya kushinda mechi 22, sare sita na kupoteza mbili kati ya 30, iliyocheza, ikirejea Ligi Kuu Bara na mabingwa Geita Gold iliyomaliza na pointi 77.
Wakati mashabiki wa Kanda ya Ziwa wakiwa na matumaini makubwa kwa kikosi hicho, Mwanaspoti linakuletea rekodi mbalimbali ambazo timu hiyo imeziandika tangu ianze kucheza Ligi Kuu Bara na sajili zilizobeba imani kubwa kwa msimu wa 2026-2027.
TAJI MOJA
Tangu mwaka 2005, moja ya mafanikio makubwa ya Kagera Sugar ni kuchukua ubingwa wa Tusker mwaka 2006, ilipoichapa Simba mabao 2-1, kwenye muda wa nyongeza katika fainali ya michuano hiyo iliyofanyika jijini, Dar es Salaam, Agosti 20, 2006.
Katika mechi hiyo ya fainali, Omary Changa ndiye aliyeizamisha Simba kwa kufunga mabao yote mawili ya dakika za muda wa nyongeza ya 90 na 97, huku kwa upande wa bao la kufutia machozi kwa Simba lilifungwa na Emmanuel Gabriel dakika ya 80.
MAINGIZO MAPYA
Baada ya Kagera kushindwa kufikia makubaliano na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mzambia Obrey Chirwa, mabosi wa kikosi hicho wakafanya maboresho ya kusaka mbadala wake na kumsajili, Mkenya Collins Maina kutokea Fortune Sacco FC.
Nyota huyo alionyesha kiwango kizuri akiwa na Fortune Sacco FC na msimu wa 2025-2026 alimaliza kinara wa ufungaji baada ya kufunga mabao 25, kwenye michuano ya National Super League (Championship).
Mabosi wa Kagera kumsajili Maina ili kuongezea nguvu eneo la ushambuliaji, akiungana na Naku James aliyetokea Polisi Tanzania na Mudathir Said aliyetoka kwa maafande wa Mashujaa FC.
Mbali na hilo, ila Kagera imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali ili kuendana na ushindani wa Ligi Kuu Bara uliopo kwa kuwasajili nyota wazoefu, wakiwemo, Said Ndemla akitokea JKT Tanzania.
Wengine ni kiungo mshambuliaji, Mrundi Emmanuel Mvuyekule aliyetokea Vision FC ya kwao Burundi, akiwa na uzoefu mkubwa wa kucheza timu mbalimbali za Tanzania, ikiwemo Mbao FC ya Mwanza, KMC FC na matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
Katika eneo la kujilinda, Kagera imemsajili pia aliyekuwa kipa wa TMA FC ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, Said Kudo ili kuongeza nguvu, sawa na beki wa kimataifa, Boniface Onyango aliyetokea Kakamega Homeboyz ya kwao Kenya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Samson Sikira anasema usajili uliofanyika unatoa matumaini ya timu hiyo kufanya vizuri katika msimu wa 2026-2027, licha ya ushindani utakaokuwepo kutokana na mahitaji ya kila mmoja.