JKT Tanzania inataka kuzivurugia Simba, Yanga
Muktasari:
- JKT Tanzania imeanza msimu kwa matokeo ambayo bado hayajaonyesha kikamilifu kile ambacho benchi la ufundi linakitaka, lakini kocha huyo amesema wana nafasi ya kubadilika na kuanza kukusanya pointi kwa kasi kadiri msimu unavyoendelea.
KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema kikosi chake hakijaingia Ligi Kuu Bara msimu huu kwa ajili ya kushiriki tu, bali kina mpango wa kuendelea kusalia kwenye nafasi za juu na kuvuruga hesabu za vigogo Simba, Yanga na Azam katika mbio za ubingwa.
JKT Tanzania imeanza msimu kwa matokeo ambayo bado hayajaonyesha kikamilifu kile ambacho benchi la ufundi linakitaka, lakini kocha huyo amesema wana nafasi ya kubadilika na kuanza kukusanya pointi kwa kasi kadiri msimu unavyoendelea.
Timu hiyo ikiwa tayari imecheza dhidi ya Yanga, imeshuhudia ikikubali kichapo kikali cha mabao 4-0, huku ikiwa bado haijakabiliana na Simba wala Azam.
“Mpango wetu ni kusalia nafasi za juu. Tunajua Simba, Yanga na Azam wana uzoefu na ubora, lakini sisi pia tumejipanga kupambana nao na kuhakikisha tunakuwa sehemu ya timu zinazofukuzana juu,” amesema kocha huyo.
“Tunawaheshimu Simba, Yanga na Azam, lakini hatuogopi kucheza nao. Tunataka timu yetu iwe katika nafasi nzuri na mwisho wa msimu watu waone JKT imekuwa sehemu ya ushindani wa juu.”
JKT ilimaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 10, sare 12 na kupoteza nane.
Kikosi hicho kilikusanya pointi 42, kikifunga mabao 30 na kuruhusu 33, hivyo kuwa na tofauti ya mabao matatu. Ilikuwa nyuma ya Singida Black Stars iliyomaliza nafasi ya nne kwa pointi 50 na TRA United iliyokuwa nafasi ya tano kwa pointi 43.
Rekodi hiyo ndiyo inayowapa JKT sababu ya kuamini inaweza kusogea zaidi msimu huu, kwani tayari ilionyesha msimu uliopita, inaweza kushindana na timu kubwa. Katika mechi mbili dhidi ya Simba msimu uliopita, JKT ilipoteza zote ikianza kufungwa 2-1 (Novemba 8, 2025), kisha 1-0 (Mei 6, 2026). Pia ilifungwa na Yanga 2-0 (Februari 22, 2026), kabla ya kupoteza tena 3-0 (Juni 30, 2026).
Ilipocheza dhidi ya Azam, ilianza na sare ya 1-1 (Oktoba 1, 2025), kisha ikafungwa 3-0 (Aprili 17, 2026), hivyo kuambulia pointi moja pekee kati ya 18 katika mechi sita dhidi ya vigogo hao baada ya kupoteza tano na sare moja.
JKT imecheza mechi nne hadi sasa katika msimu wa 2026-2027, ikianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya TRA United (Agosti 16). Ikapoteza 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania (Agosti 20), ikakumbana na kipigo kikubwa cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga (Agosti 24), kisha ikaifunga Namungo 2-1 (Agosti 29).
Kwa hesabu hizo, JKT ina pointi nne katika mechi nne, ikiwa imeshinda moja, sare moja na kupoteza mbili, huku ikifunga mabao matatu na kuruhusu manane.