Nahodha Pamba Jiji achimba mkwara Ligi Kuu
Muktasari:
- Pamba Jiji ambayo ilikuwa na matokeo mazuri msimu uliopita, msimu huu haijaanza vyema licha ya kiwango cha wachezaji mmoja mmoja uwanjani, wakicheza mechi nne mfululizo bila kupata ushindi.
MECHI nne mfululizo bila ushindi zimewaamsha mastaa wa Pamba Jiji wakitaja kilichowaangusha na kutamka kwa sasa imetosha, wakiahidi ijayo dhidi ya JKT Tanzania ni zamu yao kushangilia.
Pamba Jiji ambayo ilikuwa na matokeo mazuri msimu uliopita, msimu huu haijaanza vyema licha ya kiwango cha wachezaji mmoja mmoja uwanjani, wakicheza mechi nne mfululizo bila kupata ushindi.
Katika mechi hizo wameambulia pointi moja huku wakipoteza tatu mfululizo na kuruhusu mabao saba, wakifunga matatu na kuwa nafasi ya 14 kwa pointi moja.
Timu ilizoanza nazo msimu ni dhidi ya Dodoma Jiji iliyotoa sare ya 1-1 nyumbani, ikapoteza 2-1 dhidi ya Simba huko CCM Kirumba Mwanza, kupoteza 2-1 mbele ya Azam ugenini na kulala 2-0 kwa Yanga.
Nahodha wa timu hiyo, Hassan Kibailo ameliambia Mwanaspoti kati ya mechi nne, tatu wamekutana na timu kubwa ambazo zimewazidi kila kitu na kwa sasa wanajipanga upya.
“Tumeanza na vigogo ambao wametuzidi kitu, lakini tunapoenda kukutana na saizi yetu lazima tupambane kadri tuwezavyo kuhakikisha tunashinda na tutaanza na JKT Tanzania huenda tukashangilia” amesema Kibailo na kuongeza, licha ya matokeo hayo wamekuwa na wastani wa kupata bao isipokuwa dhidi ya Yanga walioruhusu 2-0 na umakini unahitajika kwenye sehemu ya beki.