Yanga yaonywa CAFCL
Muktasari:
- Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Septemba 5, 2026 watakuwa uwanjani nchini Botswana kukabiliana na Gaborone United ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika. Marudiano ni Septemba 12, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
YANGA imeanza msimu kwa kishindo, lakini staa wa zamani wa timu hiyo, Sekilojo Chambua, amesema bado kuna eneo moja ambalo mabingwa hao wanapaswa kulifanyia kazi haraka kabla ya kuingia kwenye mikikimikiki ya michuano ya kimataifa.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Septemba 5, 2026 watakuwa uwanjani nchini Botswana kukabiliana na Gaborone United ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika. Marudiano ni Septemba 12, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chambua alisema anaamini Yanga inazalisha nafasi nyingi mbele ya lango la wapinzani, lakini bado haijawa na utulivu wa kutosha katika kuzitumia, jambo ambalo anaona linaweza kuwa tatizo kubwa watakapokutana na wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambao hawatoi nafasi nyingi kama timu za ndani.
Yanga imeanza Ligi Kuu msimu huu ikiwa na rekodi nzuri ya ufungaji na ulinzi. Katika mechi tano imefunga mabao 15 na kuruhusu mawili pekee, huku ikiwa na pointi 15 baada ya kushinda mechi zote ikiongoza msimamo kwa tofauti ya mabao dhidi ya Simba.
“Sitaki Yanga iangalie tu idadi ya mabao inayofunga, bali namna inavyotengeneza na kutumia nafasi, kwani kwenye michuano ya kimataifa kila nafasi inayopotezwa katika mechi hizo inaweza kuwa na gharama kubwa,” alisema Chambua.
Chambua alisema Yanga inapaswa kutumia michezo ya ligi kama sehemu ya kujinoa zaidi katika eneo hilo, badala ya kuridhika na ushindi na idadi ya mabao inayopatikana.
“Yanga inapata nafasi nyingi, lakini inatumia chache. Mbele kuna michuano ya CAF, hivyo michezo hii itumike kama mazoezi ya kujinoa ili wakifika huko wafanye makubwa,” alisema Chambua.
Kauli hiyo inakuja wakati Yanga ikiwa imeshaonyesha makali ya kushambulia. Katika mechi tatu za mwanzo za ligi, ilifunga mabao 11, ikizifunga Namungo 3-1, Coastal Union 4-1 na JKT Tanzania 4-0. Makali hayo yakaendelea kwenye mechi mbli zilizofuata ikizifunga Pamba Jiji na Fountain Gate kwa matokeo ya kufanana 2-0.
AMGUSIA SHALULILE
Chambua alisema anaona washambuliaji kama Peter Shalulile wanahitaji kutengenezewa mazingira sahihi ya kufunga, badala ya kuwalazimisha kutafuta mabao kwa mashuti ya mbali kila wanapopata mpira.