Ishu ya Simba kukosa uwanja, iko hivi
Muktasari:
- Siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, Simba ililalamikia kukosa uwanja wa kufanyia mazoezi mkoani Kagera. Hata hivyo, Nkwera amesema tatizo halikuwa upatikanaji wa uwanja, bali mahitaji ya Simba kuhusu ubora wa uwanja.
KUFUATIA Simba kukosa uwanja wa kufanyia mazoezi kabla ya mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Jacob Nkwera, amesema viwanja vipo, ila changamoto ilikuwa ni ubora wa uwanja uliokuwa ukihitajika na timu hiyo.
Siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, Simba ililalamikia kukosa uwanja wa kufanyia mazoezi mkoani Kagera. Hata hivyo, Nkwera amesema tatizo halikuwa upatikanaji wa uwanja, bali mahitaji ya Simba kuhusu ubora wa uwanja.
Kanuni mpya za Ligi Kuu Bara hazilazimishi timu ngeni kufanya mazoezi kwenye uwanja ambao utatumika kwa mchezo husika siku moja kabla, tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita. Jambo hilo limeonekana kuleta changamoto kwa Simba, ambayo awali ilikuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Simba iliweka picha ya uwanja ambao, kwa mujibu wa timu hiyo, haukuwa na viwango vinavyokidhi mahitaji yake na kuandika:
“Timu yetu imeshindwa kufanya mazoezi leo jioni, siku moja kabla ya mchezo, kutokana na kukosekana kwa uwanja wenye ubora mkoani Kagera.”
Akijibu suala hilo, Nkwera amesema tatizo halikuwa ukosefu wa uwanja, bali aina ya uwanja ambao Simba ilikuwa ikiuhitaji.
“Siyo kweli kwamba hakuna uwanja mkoani hapa, bali ni uwanja ambao walikuwa wanahitaji Simba ndiyo tatizo. Sisi tuna Uwanja wa Kaitaba ambao awali ulikuwa ukitumika. Viwanja vipo, lakini ubora ambao Simba walikuwa wanahitaji ndiyo walikosa.
“Sasa wametushtua na tutajipanga ili kuboresha vile vilivyopo, ili baadaye kusiwe na shida kama hii. Lakini pia natoa wito kwa wadau wa maendeleo kuja kujenga viwanja vizuri mkoani hapa,” amesema Nkwera.
Pia, Mkurugenzi huyo amesema hakuna changamoto yoyote iwapo Uwanja wa Kaitaba utatumika kwa mechi za usiku za Ligi Kuu Bara, hata kama mchezo utachezwa saa 8:00 usiku, akisisitiza kuwa kila kitu kipo vizuri.