Ibenge afichua jambo Azam
Muktasari:
- Matokeo hayo yanaweza kuwa ishara ya mapema kwa Azam ambayo msimu uliopita ilikwama kwenye mbio za ubingwa kutokana na sare nyingi, ikiwa nazo 10 na kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 64.
KOCHA wa Azam, Florent Ibenge amesema kikosi chake bado hakijawa tayari kwa ushindani wa msimu wa 2026-2027 baada ya kuanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania.
Matokeo hayo yanaweza kuwa ishara ya mapema kwa Azam ambayo msimu uliopita ilikwama kwenye mbio za ubingwa kutokana na sare nyingi, ikiwa nazo 10 na kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 64.
Kwa hesabu za msimu uliopita, Azam ilimaliza ikiwa nyuma ya Simba kwa pointi tisa, baada ya Wekundu wa Msimbazi kukusanya pointi 73 huku Yanga ikitwaa ubingwa kwa pointi 75, ikiwa na tofauti ya pointi 11 dhidi ya Azam.
Ibenge hakuficha kutoridhishwa kwake, akisema katika mchezo huo wa kwanza uliochezwa Agosti 15, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, wachezaji wake walionekana kuchoka kiakili na kushindwa kucheza kwa umakini unaohitajika ili kupata ushindi.
Wapinzani wetu katika mchezo wa kwanza Polisi Tanzania walikuwa bora sana lakini tunapaswa kujiangalia sisi. Tunajua jinsi wanavyocheza lakini hatukuwa katika hali nzuri,” amesema Ibenge.
Kocha huyo amesema Azam ilionekana kutokuwa tayari kwa kiwango kinachohitajika huku akisisitiza kuwa bado kuna kazi ya kufanya ili timu ifikie kiwango anachokitarajia msimu huu.
“Ilionekana kama tumechoka. Hatukucheza kwa umakini wa kutosha. Tunapaswa kuboresha kwa sababu katika aina hii ya mchezo, kama unataka kufanya vizuri zaidi, unatakiwa kushinda,”.
Ibenge pia aligusia maandalizi ya kikosi chake, akisema Azam ilianza maandalizi ikiwa imechelewa huku uwepo wa wachezaji wapya inahitaji muda ili kujenga muunganiko unaotakiwa. “Labda bado hatujawa tayari. Niliwaambia kwamba tumeanza maandalizi tukiwa tumechelewa na bado hatujawa tayari, lakini ninatarajia tufanye vizuri zaidi katika michezo nyetu ijayo,” amesema.
Kwa Azam, changamoto kubwa sasa ni kuhakikisha sare hiyo haibebi sura ya msimu uliopita, kwani kila pointi inayopotea mapema inaweza kuwa na gharama kubwa katika hesabu za mwisho za ubingwa.
Msimu uliopita, kama Azam ingebadilisha hata sare tano kati ya 10 kuwa ushindi, ingeongeza pointi 10 na kufikisha 74, kiwango ambacho kingeifanya iwe juu ya Simba kwa pointi moja na kuwa karibu zaidi na Yanga.
Ibenge ameweka wazi kuwa, lengo lake ni kuifanya Azam ifanye vizuri zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote lakini hatua ya kwanza ni kurekebisha uwezo wa timu kushinda michezo ambayo msimu uliopita ilikuwa ikiishia kwa sare.