Azam FC ndani ya mipango mizito
Muktasari:
- Baada ya msimu uliopita ambao Azam ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya mashindano ya CAF na kumaliza katika nafasi za juu kwenye Ligi Kuu Bara, uongozi umeweka wazi kuwa kazi kubwa iliyopo mbele ni kuongeza ubora wa kikosi, kuimarisha benchi la ufundi na kuhakikisha timu inasogea zaidi katika mashindano ya kimataifa.
AZAM FC imeingia katika msimu mpya ikiwa na mipango mikubwa ya kuboresha zaidi kikosi chake na kuvuka mipaka iliyowekwa katika misimu iliyopita, huku uongozi wa klabu hiyo ukisisitiza kuwa safari yao haitakuwa ya kushiriki tu bali kupigania mafanikio makubwa ndani na nje ya Tanzania.
Baada ya msimu uliopita ambao Azam ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya mashindano ya CAF na kumaliza katika nafasi za juu kwenye Ligi Kuu Bara, uongozi umeweka wazi kuwa kazi kubwa iliyopo mbele ni kuongeza ubora wa kikosi, kuimarisha benchi la ufundi na kuhakikisha timu inasogea zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Mwanaspoti ilipata nafasi ya kufanya mahojiano na mwenyekiti wa Azam FC Nassor Idrssa Mohamed na anaeleza mipango ya klabu hiyo ya msimu ujao ikiwemo kuwapangua vigogo wa ligi Simba na Yanga.
MAANDALIZI YA MSIMU
Azam ilianza maandalizi yake katika kituo chake cha Chamazi kabla ya mpango wa kwenda Rwanda kwa ajili ya kuweka mazingira bora zaidi ya maandalizi kuanza.
Nassor anasema sababu kubwa ya mpango huo ilikuwa kumpa Kocha Florent Ibenge mazingira anayoyahitaji katika kukiandaa kikosi kwa msimu mpya.
“Tulianza maandalizi uwanjani kwetu Chamazi, lakini ni mwalimu tu akapanga kwenda Rwanda yeye mwenyewe. Kwa hiyo ni matakwa ya kocha yalikuwa kwa ajili ya timu kupata kujiandaa zaidi,” anasema.
"Azam ni timu inayompa nafasi kocha wake katika kupanga programu ya maandalizi, hasa wakati timu ikiwa inajiandaa kwa mashindano ya ndani na ya CAF."
IBENGE AAMINIWA
Katika suala la benchi la ufundi, Azam imechukua hatua ya kuhakikisha Ibenge anaendelea kuwa sehemu ya mpango wake wa muda mrefu.
Uongozi wa klabu hiyo unaamini moja ya njia za kujenga timu imara ni kuwaendeleza watu waliothibitisha uwezo wao badala ya kubadilisha benchi la ufundi kila msimu.
“Hatua kubwa ya kwanza ya kutunza ubora wako ni kuwabakisha uliokuwa nao bora. Ya kwanza ilikuwa ni kumbakisha Ibenge na kumuongezea mkataba ni kocha bora,” alisema.
Ibenge anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa katika soka la Afrika, jambo ambalo Azam inaamini limeisaidia timu hiyo katika safari yake ya mashindano ya kimataifa.
“Mwalimu Ibenge ni mmoja wa walimu wakubwa sana katika bara letu la Afrika mwenye uzoefu wa kufundisha mpira hata nje ya bara la Afrika. Uwepo wake tu mwaka wa mwanzo ndio ambao mwaka tumeweza kufanikiwa kuendelea hatua ya makundi na tukikusanya alama nyingi sana,” alisema.
USAJILI KIPAUMBELE NI MBELE
Mwenyekiti huyo anasema, katika usajili wa msimu huu, Azam imeelekeza nguvu zaidi kwenye maeneo ya kiungo na sehemu za mbele, ikiamini kuwa ubora katika eneo hilo unaweza kuongeza ushindani wa kikosi.
Uongozi unaona kiungo ni sehemu muhimu kwa sababu ndiyo inayounganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.
“Tumegusa zaidi kiungo kwenda mbele. Kama ujuavyo timu, sehemu ya kiungo ni sehemu muhimu sana sababu ndiyo kama kiunganishi cha ulinzi na ushambuliaji,” alisema.
Pamoja na usajili uliofanyika, Azam bado haijafunga kabisa milango yake. Uongozi umeeleza kuwa kuna uwezekano wa kuongeza mchezaji mmoja endapo mazungumzo yaliyopo yatafanikiwa.
“Tupo katika hatua za mwisho za kufunga milango ya usajili kwa msimu huu. Tupo katika hatua za mwisho za kumalizia usajili. Nafikiri kutakuwa labda na ongezeko la mchezaji mmoja ambayo kama tutafanikiwa kumpata basi atakuwa huyo ndio wa mwisho,” anasema.
FEI TOTO NA OFA
Anasema kwa upande wa kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’, uongozi wa Azam umeweka wazi kuwa hadi sasa haujapokea ofa yoyote rasmi kwa ajili ya mchezaji huyo.
“Hapana, mpaka sasa katika ofisi yetu, katika meza yangu mimi, hatujapokea ombi lolote wala ofa yoyote kwa ajili ya mchezaji wetu Salum,” anasema.
LENGO NI KILELE
Anasema Azam haijaficha kwamba lengo lake kwa msimu mpya ni kwenda hatua nyingine zaidi katika ushindani wa Ligi Kuu Bara.
Baada ya kuwa miongoni mwa timu zinazoshindana katika nafasi za juu kwa misimu kadhaa, uongozi unasema hautaki kubaki katika kiwango hicho pekee.
“Tuna nia kila siku ya kwenda juu zaidi. Tunazidi kuboresha timu yetu ili tuwe na ubora wa kuweza kufika juu kabisa kileleni,” anasema.
CAF WATAKA KUVUKA MAKUNDI
Anasema katika mashindano ya kimataifa, Azam imeweka lengo la kuvuka hatua ya makundi baada ya kufanikiwa kufika huko msimu uliopita.
Uongozi unaamini uzoefu walioupata katika kampeni iliyopita unaweza kuwa msingi wa kufanya vizuri zaidi safari hii.
“Nia na lengo letu ni kusogea mbele zaidi ya makundi ili tuweze kuzidi kusonga mbele. Kwa hiyo hiyo ndio mipango yetu, kwani tulionyesha hatua nzuri sana kwa kufika makundi.” anasema.
IBENGE AMEITAZAMA POLISI
Anasema katika mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Polisi ya Arusha, Ibenge ameshaanza maandalizi kwa tahadhari akitambua kuwa timu hiyo imeingia Ligi Kuu kwa nguvu baada ya kupata mafanikio katika Championship.
“Mwalimu yupo na anaandaa kwa tahadhari kubwa namna ya kuikabili Polisi. Mwalimu akiisifia akisema kwamba hata ujio wake wa kuja katika Premier League wamekuja kwa kishindo kikubwa zaidi baada ya kuwaondoa timu ambayo ilikuwa katika Premier League ya Prison,” anasema.
RATIBA HAINA MALALAMIKO
Kwa upande wa ratiba ya Ligi Kuu Bara, uongozi wa Azam unasema msimu huu umeanza kwa utulivu tofauti na nyakati ambazo ratiba zinapozinduliwa baadhi ya klabu huibua malalamiko.
“Naona katika miaka ambayo ratiba haina malalamiko basi huu ni mwaka ambao ratiba haina malalamiko. Sijawahi kusikia tangu imetoka, sikusikia malalamiko kutoka klabu yoyote ile,” alisema.
REKODI ZA MSIMU ULIOPITA
1.Ligi Kuu ya NBC (NBC Premier League)
Rekodi ya Kihistoria ya Nyumbani: Azam FC iliweka rekodi mpya kwa kuwa timu ya kwanza kumaliza msimu mzima wa Ligi Kuu bila kuruhusu wavu wake kuguswa (clean sheets zote) kwenye uwanja wa nyumbani wa Azam Complex.
Mfungaji Bora wa Timu: Feisal Salum "Fei Toto" aliongoza safu ya ufungaji ya klabu hiyo akipachika mabao 15 kwenye ligi.
Licha ya uimara wa nyumbani, walikabiliwa na changamoto ugenini kwa kuweka rekodi ya kutoka sare michezo 10 kwa msimu mzima.
2. Kombe la Shirikisho la CRDB (CRDB Federation Cup)
Azam FC ilitinga hatua ya fainali ya kombe hili baada ya kuiondoa Yanga kwenye hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 3-2 baada ya muda wa ziada.
Walipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Simba SC kwa kufungwa bao 1-0, na hivyo kuishia kuwa washindi wa pili.
3. Mashindano ya kimataifa (CAF Confederation Cup)
Azam FC ilifanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo iliweka rekodi ya kukusanya alama 9.