HUMUD : Stori yake na Toto la Kitanga ni tamu

Muktasari:
Wengi wenu mmeshazoea kuona vitu vyake akiwa uwanjani, lakini safari hii Mwanaspoti iliamua kumzukia ili umjue kwa undani nje ya soka yeye ni nani na huwa anafanya nini.
MBISHA hodi safari hii alifunga safari mpaka jijini Tanga, nyumbani kwa kiungo mmoja fundi ambaye wengi wanamfahamu kwa jina la ‘Gaucho’. Ndio Gaucho! Anayefananishwa na nyota wa zamani wa Kibrazili, Ronadinho Gaucho. We unadhani ni nani aliyezukiwa maskani safari hii? Ni Abdulhalim Humud, anayeichezea Coastal Union kwa sasa baada ya kukipiga Mtibwa, Simba na Azam.
Wengi wenu mmeshazoea kuona vitu vyake akiwa uwanjani, lakini safari hii Mwanaspoti iliamua kumzukia ili umjue kwa undani nje ya soka yeye ni nani na huwa anafanya nini.
Jamaa anabana maeneo ya Sahar, jijini Tanga, nyumba yake iko hatua chache kutoka zilipo fukwe maarufu ya Bahari ya Hindi ya jijini humo iitwayo Tanga Beach, yaani yeye ni full kipupwe cha asili.
Mwandishi alifika na kukaribishwa kwa bashasha, ni nyumba kubwa inayojitosheleza kwa kila kitu na ndani mmeenea fenicha za maana na za thamani. Katika nyumba hiyo anaishi pamoja na mkewe, Shaymaa Said Amour, Toto la Kitanga ambalo kwa jinsi Gaucho alivyokolea kwake amezoea kumuita Msomali wake.
Wawili hao wameoana kama mwaka mmoja na ushei, lakini kwa jinsi wanavyoishi kama njiwa tunduni, ni lazima upatwe na wivu. Wanapenda na kuiva sana pamoja.
Kutokana na namna walivyonivutia, makala yetu nitaipindua, tuanzie kwenye mapenzi yao kisha mengine yafuate au waonaje?
MALAVIDAVI
Mwanaspoti: Mmh! Waonyesha mnapendana sana, hivi haya mapenzi ni ya leo au ya muda wote?
Humud: Hii ni kawaida yetu, kwa wapendanao huwezi kuuliza kitu. Naweza kusema tunapendana hata mambo yetu tunafanya kama mapacha vile. Tangu nilipomwoa tuna kama mwaka hivi na mambo yetu yako poa.
Mwanaspoti: Ni katika mazingira gani uliyompata mkeo na nani alianza kumweka sawa mwenzake?
Humud: Ni stori ndefu kama unavyojua kwa kawaida mapenzi huja ‘automatic’ tu na safari yetu ilikuwa hivi. Nilikuwa Dar es Salaam kwenye mapumziko wakati huo nimeshaanza kuichezea Coastal, nikapigiwa simu na Shaymaa ambaye kwa wakati huo nilikuwa simjui kabisa. Baada ya kunipigia simu, tulizungumza mambo mengi nikavutiwa naye, nilipomwambia nampenda na yeye hakunificha, alinambia ananipenda kumbe alikuwa anasubiri, nimtamkie tu. Lakini alinipa msimamo wake na kuniambia kama na mimi nampenda, niende kwao nikajitambulishe.
Na kama unavyojua, siku hizi mambo hadharani, baada ya kuona picha zake, mwonekano wake ulinivutia, alikuwa na vigezo vyote ambavyo mimi navipenda na kwa sababu nilikuwa sina mahusiano na mtu mwingine yoyote kwa wakati huo, nilimfungia kazi.
Kabla sijafanya maamuzi yoyote juu yake, kwa takribani kipindi cha mwezi mmoja tulikuwa tunachati tu kwenye simu na kuzungumza mengi tu, wakati huo yeye yupo Tanga na mimi Dar es Salaam na baadaye, niliamua mwenyewe kupanda basi hadi Tanga kwa ajili ya kuonana naye.
Nashukuru, nilifika salama na Shaymaa alinipokea na kunipeleka nyumbani kwao sambamba na kunitambulisha, kiukweli nilifurahia mazingira yale, nilijua ni mtu ambaye kweli ananipenda na ananiheshimu na amenipa thamani ya kunipeleka hadi kwao jambo mbalo kwa msichana asiyeeleweka ni ngumu kulifanya.
Baada ya hapo, kwa sababu nilishakuwa nimemzoea kutokana na namna tulivyokuwa tunawasiliana kwenye simu, kubwa alinisisitizia nianze mchakato wa ndoa, na kwa wakati huo, mimi nilikuwa nimeshamzimikia, nikaanza taratibu.
Huwezi kuamini, baada ya tukio hilo, sikufichi, haikupita hata wiki, nikakamilisha mambo yote na kufanikiwa kumwoa Shaymaa akawa mke wangu rasmi na ndivyo tunaishi hadi sasa.
Mwanaspoti: Kitu ambacho hupendezwi nacho, pale Shaymaa anapokifanya?
Humud: Kitu ambacho sikipendi akifanye mke wangu, sipendi mtu anayependa kuzurura hovyo bila mpango, ninachotaka kumwona anatulia nyumbani na kufanya majukumu ya hapa ndani, yeye ni mke wa mtu. Kingine tabia ya kuvaa hovyo bila kujisitiri siipendi, yeye ni mtoto wa Kiislamu na anajua majukumu yake katika uvaaji, anapovaa hivyo, lengo lake amwonyeshe nani maumbile yake wakati mimi mumewe nipo?
SHAYMAA ACHOMBEZA
Mwanaspoti: Eti hiki anachokiongea Humud namna mlivyokutana ni kweli?
Shaymaa: Ni kweli kabisa, hajaficha na kwa kukuongezea stori kamili ilivyokuwa. Unajua nilibahatika kuiona picha yake mahali fulani nikaipenda, basi nikaichukua na kuisevu kwenye ‘profile’ ya Whatsapp kwenye simu yangu, hapo nilikuwa simjui anaishi wapi na hata kazi yake sijui. Watu walivyokuwa wanaiona, walikuwa wananiuliza, vipi unamjua huyo jamaa? Nilipowajibu simjui ndipo walianza kunipa wasifu wake kuwa ni mchezaji wa Coastal na mambo mengi basi nikawaambia naombeni namba yake na nilipoipata, nikampigia na kuanza urafiki wetu.
Tulikuwa tunazungumza mambo mengi lakini binafsi, ukweli wa mambo nilikuwa naujua mwenyewe rohoni. Nilikuwa nampenda sana na kusema kweli, nilikuwa nasubiri yeye tu anitamkie na alipofanya hivyo, sikuwa na jinsi, nilikubali fasta.
Mwanaspoti: Kitu gani kilivutia kwake na Humud ni mtu wa namna gani?
Shaymaa: Nilimpenda tu kutokana na namna alivyo siwezi kuelezea zaidi. Kuhusu Humud ni mtu mwenye malengo na mipango kwanza, siyo mtu wa kuzurura vijiweni, anapokosekana nyumbani, basi atakuwepo kwenye timu na ratiba yake iko hivi, asubuhi anapoamka anakwenda kukimbia na akirudi anakunywa chai analala baada ya hapo chakula cha mchana, anaenda kambini. Kila jioni lazima akimbie na anapenda sana kulala.
Mwanaspoti: Ni chakula gani anachopendelea?
Shaymaa: Ni mpenzi wa viazi vilivyochanganywa na nyama au samaki, ukiaandaa chakula hicho, anafurahi sana.
NYUMBANI
Mwanaspoti: Hapa nyumbani unishi na nani?
Humud: Naishi na mke wangu Shaymaa.
Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani unapendelea kufanya nini?
Humud: Kupumzika tu na kusikiliza muziki au kuangalia televisheni.
Mkali huyo anasema malengo yake kisoka ni kuhakikisha anarejea kwenye makali yake kama alivyoweza kung’ara miaka ya nyuma na hasa kwenye pambano la Taifa Stars dhidi ya Brazil mwaka 2010 na Tanzania kufungwa mabao 5-1.