HISIA ZANGU : Nilimsikiliza Van Dijk nikamuelewa vizuri sana!
Muktasari:
- Van Dijk alikuwa anawashukuru wachezaji wenzake wa Liverpool kwa kumuwezesha kuwa mchezaji bora wa msimu huku akidai kwamba anaamini kwamba licha ya ukweli kwamba yeye ni mlinzi mzuri lakini ulinzi ni kazi ya timu nzima.
PAMBANO la soka Ligi Kuu ya Tanzania bara linamalizika. Unapata hamu ya kuwasikiliza manahodha wa pande zote mbili. Ghafla hamu yako inatoweka. Wanaongea kile kile walichoongea katika mechi zilizopita. Na wote wanaongea kitu kimoja.
Wa kwanza atasema “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumemaliza mechi salama. Kama mnavyojua, mpira una matokeo matatu. Kushinda, sare au kufungwa. Kocha atakuwa ameona makosa tutayarebisha kwa ajili ya msimu ujao.”
Nahodha wa upande wa pili atasema vile vile tu. Anachoweza kubadlisha labda ni kusema “Tunashukuru Mungu tumepata matokeo”. Atachomokea maneno hayo katika sehemu ambayo mwenyewe alisema ‘kocha atarekebisha makosa’. Hii ndio inabakia kuwa tofauti yao.
Wikiendi ijayo ukisubiri watasema hivyo hivyo. Imekuwa hivyo hivyo kwa manahodha wote wa Ligi Kuu wakihojiwa pale Azam TV mara mechi zinapomalizika. Unajiuliza, wanaelewa walichokuwa wanakifanya uwanjani? Wana ufahamu na mchezo wenyewe?
Upande wa makocha hadithi imekuwa hii hii ingawa wao huwa wanalia zaidi na waamuzi. Wakati ukisubiri kocha aseme kwanini wamepoteza mechi au wameshinda mechi utaishia kusikia malalamiko dhidi ya waamuzi basi.
Sawa, mwamuzi anaweza kukubali bao la kuotea, lakini kocha anapaswa kutuambia mwelekeo wa mechi ulivyokuwa. Kipindi cha kwanza kilivyokwenda, au akabadili nini kuelekea katika kipindi cha pili. Hautasikia. Utasikia malalamiko kwa waamuzi tu basi.
Kama kocha hatamlalamikia mwamuzi basi ataishia kusema ‘wamekubali kichapo na wanajipanga kwa ajili ya mechi ijayo’. Hawezi kufafanua zaidi. Unajiuliza kama kweli anaifahamu kazi yake. Kocha ambaye namkubali anaweza kufafanua zaidi ni kocha wa Simba, Patrick Aussems.
Wiki moja iliyopita nilikuwa namsikiliza mlinzi wa Liverpool, Virgil van Dijk baada ya kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa msimu. Nilitabasamu nilipojaribu kumfananisha na manahodha wetu wa Ligi Kuu.
Van Dijk alikuwa anawashukuru wachezaji wenzake wa Liverpool kwa kumuwezesha kuwa mchezaji bora wa msimu huku akidai kwamba anaamini kwamba licha ya ukweli kwamba yeye ni mlinzi mzuri lakini ulinzi ni kazi ya timu nzima.
Nilipenda jinsi alivyofafanua kuhusu falsafa nzima ya ulinzi. Aliongea katika namna ambavyo ungependa kuona makocha wetu wazawa wakiongea au manahodha wetu wakiongea. Vilikuwa ni vitu viwili tofauti.
“Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa sababu ulinzi ni kazi ya timu nzima na siyo mchezaji mmoja. Washambuliaji wetu wale watatu kule mbele kama hawana mpira huwa wanatoa mbinyo (pressing) kwa mabeki wao. Mpira ukivuka kuingia katikati kuna viungo wanawajibika kukaba vema. Lakini wale wa mbele wanarudi katikati kusaidia, na mwishowe kabisa wanasaidia nyuma,” alisema Van Dijik.
Huyu alikuwa anafafanua kitu ambacho tunakiona pale Liverpool. Lakini huyu alikuwa anachambua kama mchambuzi au kama kocha. Ni mchezaji ambaye anajua timu yake inafanya nini uwanjani. Ni mchezaji ambaye kama timu yake ikifungwa basi anaweza kutuambia kwanini imefungwa. Hata kama imeshinda anaweza kujua kwanini timu yao imeshinda.
Akina Jamie Carragher walianzia katika mahojiano kama haya kwenda kuwa wachambuzi wazuri wa soka. Siyo kila mchezaji mzuri anaweza kuwa mchambuzi mzuri. Inabidi uufahamu mchezo wenyewe. Unaweza kuwa hatari uwanjani lakini ukaondoka uwanjani ukiwa haujui kwanini timu yako imeshinda au imeshindwa.
Kila nikiwatazama wachezaji wetu wanapohojiwa pale Azam TV nataka tamaa kuona kama wanaweza kuwa wachambuzi siku za usoni. Matokeo yake kuna vijana wengi mitaani ambao siyo wanasoka lakini wanakalia katika viti vya televisheni siku hizi kutuchambulia soka na wanachambua vema tu.
Wanasoka wa zamani wanalalamika lakini ukweli unabakia pale pale kwamba kuwa mwanasoka wa zamani siyo leseni ya kuwa mchambuzi wa soka au kocha. Ni kazi mbili tofauti na kucheza soka. Zinahitaji upeo tofauti. Hii ni kazi mpya.
Mara nyingi huwa naongea na staa wa Simba, Emmanuel Okwi. Unaona kabisa kwamba anaufahamu mpira. Akiwa kocha mzuri sitashangaa. Atakwambia kwanini Simba imefungwa au imeshinda. Atakwambia kuhusu upungufu na ubora wa timu. Atakupa na mifano hai ndani ya uwanja. Anaweza kukwambia kwamba wameshinda lakini wamecheza ovyo kwa sababu kadhaa.
Zamani nilikuwa naongea na mshambuliaji wa Kenya, Ben Mwalala. Yeye alikuwa mchezaji wangu Coastal Union wakati huo nikiwa msemaji. Mechi zinapokwisha tunapoamua kuchambua mpira unajua unachambua mpira na mtu ambaye anayeufahamu mpira. Sijashangaa kuona amekuwa kocha mzuri pale Kenya.
Nimekaa na wachezaji wetu wazawa. Mara nyingi ukiongea nao huwa anakwambia kuhusu majukumu yake uwanjani. Kama ni beki atakwambia alikuwa anafeli kwa sababu winga wake alikuwa hamsaidii kukaba. Hatakwambia kiujumla jinsi timu yao ilivyocheza.
Tujifunze kuufahamu mpira. Tujifunze kuusoma mpira. Tujifunze kuuelewa mpira. Uwe mchezaji, kocha, shabiki, mwandishi wa habari, na watu wa taaluma nyingine. Ni vema kujifunza kuulewa mpira. Kwa wachezaji wetu ambao wanatamani kuwa wachambuzi au makocha, ni vema kuufahamu mpira.