Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hata hii Taifa Stars nayo imeteuliwa pub

Kikosi cha Taifa Stars

Muktasari:

Ndicho kilichoniingia akilini wakati nikipitia majina ya timu yetu ya soka ya taifa, Taifa Stars, iliyotangazwa juzi Jumanne na Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura. Ni timu ya kujiandaa na pambano la kirafiki dhidi ya Namibia la Machi 5.

UNAWEZA kuchora picha kichwani, mlevi mmoja akiropoka katika baa moja ya katikati ya jiji akisema: “Mkate Sure Boy, ingiza Hassan Mwasapili, ondoa Simon Msuva, ingiza Mcha Khamis. Huyu Mcha ananikosha sana.”

Ndicho kilichoniingia akilini wakati nikipitia majina ya timu yetu ya soka ya taifa, Taifa Stars, iliyotangazwa juzi Jumanne na Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura. Ni timu ya kujiandaa na pambano la kirafiki dhidi ya Namibia la Machi 5.

Makini kama alivyo, mpole kama unavyomwona na msikivu kama alivyozaliwa, Wambura alionekana kufadhaika sana katika kupokea maswali ya Waandishi wa Habari. Ndiyo, namfahamu Wambura. Mtu makini na Mwandishi wa Habari za Michezo wa muda mrefu. Hata hivyo, anapitia wakati mgumu kwa sababu anafanya kazi ngumu na watu wagumu. Mbaya zaidi, kazi yake ni kuagizwa.

“Timu hii imeteuliwa na TFF na si kocha, hiyo ndiyo taarifa rasmi, kusema nani atafundisha naomba muwe na subira, itajulikana ndani ya saa 48,” alisema Wambura.

Maajabu yaliyoje! Hili ni soka la karne ya Vasco da Gama? Tangu lini timu ya taifa ikachaguliwa na TFF kama TFF? Kocha yuko wapi?

Jibu utakalopata ni rahisi tu kuwa kocha Kim Poulsen ameondolewa madarakani. Nadhani anasubiri kukabidhiwa barua tu ingawa nina uhakika kwa mdomo ameshaambiwa.

Tatizo si kuondolewa kwa kocha. Makocha wote maarufu duniani huwa wanaondolewa. Waliondolewa akina Jose Mourinho, Guus Hiddink, Carlos Alberto Perreira na wengineo. Haishangazi kuona Kim akiondolewa.

Lakini kwa muundo wa timu yenye heshima kama Taifa Stars, unatazamia kuwa achaguliwe kocha wa muda (Caretaker) kwa ajili ya kukabidhiwa jukumu hata la wiki moja tu la kuongoza timu katika mechi ya kirafiki au ya kimashindano kabla ya kocha kamili hajatangazwa.

Ni suala la heshima na linalomfanya mchezaji ajiamini na timu ya taifa nayo iheshimiwe. Sio lazima kocha wa muda awe mzungu. Anaweza kuwa Ken Mwaisabula ambaye kila mwisho wa wiki hakosekani katika viwanja vya soka akifuatilia mechi za Ligi Kuu Bara.

Kupeleka majina ya wachezaji katika meza za baa na kuchagua wachezaji huku msemaji akikiri kwamba timu haikuchaguliwa na kocha nadhani ni kulikosea soka heshima, hasa timu yenyewe inapokuwa ya Taifa.

Sitaki sana kuingia kwa undani kuhusu majina. Lakini kwa uzoedu wangu wa kutembelea katika viwanja vya soka kila wiki, ni wazi kwamba yeyote aliyeteua timu akiwa katika meza ya Pub alikuwa akiomba ushauri kwa wapita njia.

Mcha Khamis ‘Vialli’ hana nafasi katika kikosi cha Azam kwa sababu kiwango chake kiko ovyo kwa sasa kuliko kipindi kingine chochote. Nafasi yake upande wa kushoto ameipoteza kwa kinda Joseph Kamwaga ambaye naye ameumia na hivyo kupisha nafasi kwa John Bocco ambaye amerudi uwanjani.

Sasa Azam inasimamisha watu watatu katika mfumo wao wa 4-3-3. Mbele wanacheza Brian Umony, John Bocco na Kipre Tchetche. Katikati wanacheza Himid Mao, Kipre Balou na Salum Abubakar.

Walimuona wapi Mcha? Kwanini walimchagua? Jibu ni moja tu. Inawezekana TFF yetu mpya inatengeneza urafiki wa kasi na Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA). Si ajabu walitaka kutengeneza sura ya Muungano kwa kuwepo Mcha. Wakati huo, mmoja kati ya wachezaji wenye pasi nyingi za mwisho, Simon Msuva amekatwa.

Kwanini rafiki yangu Chuji ameitwa? Nani hajui kiwango kibaya ambacho Chuji amepitia siku za karibuni pamoja na matatizo yake ya Yanga? Mechi ya mwisho kubwa alicheza ile ya Mtani Jembe dhidi ya Simba Oktoba 21 mwaka jana. Nyingine ni ile ya pili dhidi ya Comorozane. Waliochagua walimchunguza Steven Mazanda wa Mbeya City?

Wakati mwingine nawaza tu kwamba si ajabu hata jina la Sure Boy lilisahaulika tu baada ya glasi kupamba moto mezani, lakini siamini sana kama walikusudia kumuacha. Hauwezi kumpata kiungo anayetawala mechi kwa muda mrefu zaidi ya Sure Boy hata kama hana pasi nyingi za mwisho kwa washambuliaji.

Sehemu ya ulinzi wa kati ina walinzi wawili tu, Kevin Yondan na Aggrey Morris. Si ajabu mlevi mmoja kando ya meza alisema ‘hao hao wanatosha’ kwa kuamini kuwa hili ni pambano moja tu, tena la kirafiki tu.

Lakini kama lolote likitokea, sioni mlinzi mwingine wa pembeni anayeweza kucheza katikati. Siamini kama kocha yeyote mzawa angechagua hivi, hata kama tungempa timu hii kwa muda.

Wiki iliyopita niliandika kuwa Taifa Stars inaendeshwa kwa mawazo ya baa kufuatia mpango wao wa kusaka vipaji vilivyosahaulika mikoani. Lakini kwa hili, nadhani ni wakati wa kila mtu kushuhudia kuwa tumeshalirudisha soka letu vijiweni kama ilivyokuwa zama za FAT.

Kama msemaji wa taasisi husika anakiri kwamba timu haikuchaguliwa na kocha, basi sio mbaya kukisia kwamba timu yenyewe ilichaguliwa katika meza ya baa huku wateja wengine wakichangia mawazo ingawa hawajui kama Mcha anacheza au hachezi.