Hasnath Ubamba aanza kwa kishindo Madrid
Muktasari:
- Ubamba aliyeanza msimu mpya akiwa na hamu ya kuendeleza kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita akiwa FC Masar, alitumia dakika 15 tu kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Madrid CFF.
WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Hasnath Ubamba, ameanza kwa kishindo maisha yake mapya ndani ya klabu ya Madrid CFF ya Hispania baada ya kuanza katika kikosi cha kwanza na kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini humo.
Ubamba aliyeanza msimu mpya akiwa na hamu ya kuendeleza kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita akiwa FC Masar, alitumia dakika 15 tu kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Madrid CFF.
Bao hilo lilikuwa mwanzo mzuri kwa nyota huyo wa Tanzania ambaye alipewa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Valencia, kabla ya Madrid CFF kuendeleza ubabe na kumaliza mchezo huo kwa ushindi wa mabao 3-1.
Kuanza kwake katika kikosi cha kwanza na kufunga mapema kunaweza kuwa ishara nzuri kwa Ubamba katika safari yake mpya Hispania, hasa baada ya msimu uliopita kuonyesha uwezo mkubwa akiwa FC Masar na kujijengea nafasi katika soka la wanawake barani Afrika.
Ubamba ameingia Madrid CFF akiwa na jukumu la kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji, huku uwezo wake wa kucheza pembeni na kutengeneza nafasi ukitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mipango ya timu hiyo msimu huu.
Ushindi wa mabao 3-1 pia umeifanya Madrid CFF kuanza kampeni ikiwa na morali nzuri, huku Ubamba akipata nafasi ya kuonyesha uwezo wake kwenye moja ya ligi zinazoshindaniwa zaidi katika soka la wanawake barani Ulaya.
Mbali na Ubamba Mtanzania mwingine aliyeanza vizuri wikiendi hii ni Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr Women ya Saudia alifunga hat-trick kwenye ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Al Hilal katika fainali ya mashindano ya Super Cup.
Clara na mbongo mwenzie Julietha Singano wanaandika historia ya kubeba taji la Super Cup wakiitandika mahasimu wao Al Hilal kwenye fainali ambayo imekuwa na ushindani wa aina yake.