Tanzanite Queens na historia Kombe la Dunia
Muktasari:
- Lakini kwa Tanzania timu hiyo inakuwa ya pili baada ya Serengeti Girls kucheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia U-17 mwaka 2022.
HISTORIA mpya imeandikwa. Tanzania imefanya kile ambacho kizazi cha nyuma hakikuwahi kufanya, baada ya timu yake ya vijana ya wanawake kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za Kombe la Dunia la FIFA U-20 la Wanawake.
Lakini kwa Tanzania timu hiyo inakuwa ya pili baada ya Serengeti Girls kucheza hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia U-17 mwaka 2022.
Hii ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kufika kwenye mashindano haya kwa umri huo, huku Poland 2026 ikiwa ni toleo la 12 la Kombe la Dunia la U-20 la Wanawake.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa sita yatakayocheza fainali za dunia kwa mara ya kwanza, pamoja na wenyeji Poland, Benin, Ecuador, New Caledonia na Ureno.
SAFARI YAO
Safari ya Tanzanite Queens kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu ilianzia raundi ya pili baada ya kuitoa Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0, ikishinda mabao 4-0 katika mechi ya kwanza na marudiano ikashinda mabao 3-0.
Ikatinga raundi ya tatu ikawatoa majirani zao Kenya kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na raundi ya nne ikakutana na Cameroon.
Mambo yalianza kuwa magumu kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya nne ambayo ilikuwa ya mwisho, Tanzanite ilipoteza kwa mabao 3-1 kule Cameroon na baadhi ya mashabiki waliikatia tamaa timu hiyo na kuona tayari safari yao imeishia hapo.
Licha ya kukatiwa tamaa timu hiyo ikaibuka kifua mbele na kiufunga Cameroon mabao 2-0 Uwanja wa New Amaan Complex na kuifanya Tanzanite kufuzu Kombe la Dunia.
NJAA
Timu hiyo ipo Poland kuandika historia ya kwanza ya kwenye fainali hizo ikiwa na njaa na uchu wa kufanya vizuri.
Hilo linaweza kuwapa uhuru wa kucheza bila hofu. Mfano mzuri Kombe la Dunia lililopita Cabo Verde iliandika historia ya kucheza kwa mara ya kwanza lakini ilionyesha kiwango kizuri ikacheza hadi hatua ya mtoano.
Hivyo namna Tanzanite ilivyopambana kwenye mechi za kufuzu inaonyesha kuwa hawatakiwi kuchukuliwa poa.
Kuanzia kwenye mechi dhidi ya Kenya ililoamuliwa kwa penalti hadi changamoto ya raundi ya mwisho, Tanzania ililazimika kucheza chini ya presha kubwa.
UZOEFU
Hii inaweza kuwa moja ya sababu. Tanzanite Queens haina rekodi kwenye fainali hizo, maana yake wachezaji wengi watakutana kwa mara ya kwanza na aina ya presha ambayo hawajaizoea.
Watakutana na timu ambazo zimezoea kucheza kwenye mashindano ya FIFA, zikiwa na mifumo iliyojengwa kwa muda mrefu na wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa.
Asilimia kubwa ya wachezaji wanaingia kwenye mashindano hayo wakiwa katika hatua ya kuchipukia, wakitumia jukwaa hili kupata uzoefu mkubwa zaidi baada ya kucheza ligi za ndani na baadhi yao kuitumikia timu za taifa katika ngazi mbalimbali.
Hapa ndipo tofauti ilipo, wenye mashindano ya kawaida, mchezaji anaweza kukutana na presha ya mashabiki, matokeo au ushindani wa ligi, lakini Kombe la Dunia linaongeza kitu kingine.
Brazil, England na Canada si wapinzani ambao Tanzanite Queens inaweza kuwadharau. Wote wana historia kubwa zaidi katika soka la wanawake na uzoefu wa kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa, kwa Tanzania, kila mchezo utakuwa kama darasa jingine la kujifunza, lakini darasa ambalo litahitaji pia matokeo.
KUNDI GUMU
Tanzanite wanaingia kwenye mashindano hayo wakifahamu kuwa hawapo kwenye kundi rahisi kuwekwa na vigogo kama Brazil, England na Canada ambazo zimecheza mara kadhaa kwenye fainali hizo ni uzoefu mwingine.
Brazil ni moja ya mataifa yenye utamaduni mkubwa wa soka duniani, huku England na Canada zikiwa miongoni mwa nchi zilizoendelea sana kwenye maendeleo ya soka la wanawake.
Kwa Tanzanite kila mchezo utakuwa somo na mtihani. Mchezo dhidi ya Brazil utahitaji nidhamu kubwa bila mpira na hata ukiwa na mpira. England inaweza kuwalazimisha kutumia nguvu na kasi, wakati Canada nayo inaweza kuwa changamoto kutokana na ubora wake wa kiufundi na kimwili.
Lakini Tanzania haina cha kupoteza. Kila pointi itakayopatikana itakuwa historia nyingine kwenye taifa ambalo ndio mara yao ya kwanza.
NYOTA WA KUAMUA
Miongoni mwa nyota ambao wanaweza kuwa na jukumu kubwa la kuamua mechi kwenye mashindano hayo ni winga Winfrida Gerald na Hasnath Ubamba, ambao wote wameonyesha uwezo wa kuibeba Tanzanite Queens kwenye nyakati muhimu.
Gerald anayekipiga JKT Queens ni mmoja wa washambuliaji muhimu kwenye safari ya kufuzu. Alifunga bao la ugenini dhidi ya Cameroon katika mchezo wa kwanza wa raundi ya nne, bao ambalo baadaye lilikuwa na thamani kubwa katika hesabu za kufuzu.
Ubamba naye aliandika historia hiyo baada ya kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cameroon kwenye mchezo wa marudiano Zanzibar. Bao hilo liliipa Tanzania ushindi uliowavusha kwenda Poland kwa mara ya kwanza.
Kinachowafanya wawili hao kuwa muhimu zaidi ni uwezo wao wa kucheza maeneo ya pembeni na kuvuruga ulinzi wa wapinzani kwa kasi, mipira ya kwenda mbele na uwezo wa kutengeneza nafasi.
Gerald anaweza kutumika kama silaha ya kuvunja mistari ya ulinzi, hasa pale Tanzania inapopata nafasi ya kushambulia kwa kasi. Ubamba, kwa upande mwingine, anaingia kwenye mashindano akiwa tayari ana uzoefu wa kucheza nje ya Tanzania, jambo linaloweza kumsaidia katika kukabiliana na presha ya mechi za aina hiyo.
Ubamba kwa sasa anakipiga Madrid CFF, huku rekodi zake za mwaka 2026 zikionyesha pia alifunga bao katika ushindi wa Tanzania wa 2-1 dhidi ya Afrika Kusini kwenye WAFCON 2026.