Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hapa Mapinduzi kuna vita nzito

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi 2023 inatarajiwa kufunguliwa rasmi leo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, kabla ya timu 12 kuanza kupepetana hadi Januari 13 na kupatikana bingwa wa msimu huu.

Safari hii michuano hii inashirikisha timu 12, tatu zaidi ya zile zilizoshiriki msimu uliopita ulioshuhudiwa Simba ikibeba taji la nne la michuano hiyo kwa kuilaza Azam kwa bao 1-0 kupitia penalti ya Meddie Kagere, kutokana na kosa lililofanywa na kipa Mathias Kigonya.

Kilichosisimua zaidi msimu huo ni kitendo cha mfungaji bora wa michuano hiyo ya 2022 kunyakua tuzo kwa kufunga mabao mawili tu. Hujakosea! Mabao mawili tu, naye alikuwa ni Kagere ambaye msimu huu atashiriki michuano hiyo akiwa na kikosi kipya cha Singida Big Stars.

Kagere alilingana idadi ya mabao na aliyekuwa Mchezaji Bora wa michuano, Pape Ousmane Sakho (Simba) na Idris Mbombo (Azam) sambamba na Heritier Makambo (Yanga), Abrahman Othman (KMKM) na Hussein Mwinyi (Meli 4 City) ambao timu zao zilitolewa mapema.

Mbombo, Makambo, Sakho na Abrahman Othman bado wapo kwenye timu zao kitu kinachoonyesha huenda msimu huu mambo yakawa moto zaidi katika mchuano wa ufungaji bora.

Mbali na nyota hao, lakini ushiriki wa klabu 12 wakiwamo wageni Singida yenye majembe ya Kibrazili kama Bruno Gomes na wengine kunaongeza utamu, mbali na mastaa wa klabu za Simba, Yanga, Azam, Namungo, KMKM, Chipukizi, Jamhuri, Mlandege, Malindi na Aigle Noir ya Burundi.

Mbali na nyota wanaochuana kwenye Ligi Kuu Bara (TPL) na wale wa ZPL, lakini zipo taarifa kwamba baadhi ya klabu zinaweza kushusha mastaa wapya kabisa hasa wa kigeni na wazawa ambao wanapigiwa hesabu za kusajiliwa kwenye dirisha dogo na kuliamsha dude kibabe.

Tayari Simba inaye Saido Ntibazonkiza aliyeshiriki na kubeba ubingwa wa Mapinduzi 2021 akiwa na Yanga na kocha Juma Mgunda alikaririwa anataka kuitumia michuano hiyo kuwapa nafasi wale wachezaji ambao hawajatumika sana kwenye mechi za Ligi ya Bara.

Wazo kama hilo limetolewa pia na Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, ambaye msimu uliopita walitema taji kwa watani wao kulibeba. Nabi alikaririwa hivi karibuni akiahidi kuwapa mapumziko baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza wanaotumika sana katika TPL akiwamo Fiston Mayele.

Mayele ndiye kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 14, akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10 ambaye hata hivyo hatashiriki michuano hiyo kutokana na kuwa majeruhi akiumia kwenye mechi ya ligi dhidi ya Kagera Sugar iliyoisha kwa sare ya 1-1.

Mashabiki wa soka wana hamu kubwa ya kutaka kuona nani anayeibuka mkali wa mabao wa michuano ya msimu huu, hasa kwa kuzingatia imepita zaidi ya miaka 10 sasa hakuna mchezaji aliyewahi kumaliza michuano hiyo akifunga zaidi ya mabao matano.

Rekodi ya mabao matano iliyowekwa na Jesse Were wakati akiichezea Tusker ya Kenya katika michuano ya mwaka 2013, kisha Obrey Chirwa alipokuwa Azam naye akajibu 2019 na baada ya hapo, haijawahi kufikiwa wala kupitwa kwani wengine wote walikuwa wakimaliza na mabao chini ya hayo.

Pia kuna rekodi nyingine ya kutetea tuzo ya ufungaji bora, haijawahi kutokea katika misimu 11 iliyopita tangu 2012 mchezaji yeyote kutetea tuzo hiyo, licha ya Simon Msuva aliyekuwa Yanga aliwahi kubeba tuzo mara mbili ndani ya misimu mitatu. Alitwaa 2015 na kurejea tena 2017 kabla ya kuuzwa Morocco na sasa anacheza soka la kulipwa Saudi Arabia.