Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gwiji Afrika aliye chanzo cha Mogella kuitwa ‘Golden Boy’

Muktasari:

Nilipomuleleza nilichoitiwa ofisini Mzee Polo aliniambia: ”The last time they fixed us oooh… this time they go die...they will die inside,” akimaanisha: “Mra ya mwisho walitufunga, lakini safari hii watakufa… watakiona cha mtema kuni.”

NDIO kwanza nimefika nyumbani kwangu Accra, Ghana, kutoka Nigeria nilikokwenda kuandika makala kwenye gazeti la Sunday News.

Nikiwa nimepumzika alikuja nyumbani dereva na kuniambia nilitakiwaofisini haraka.Nilipomuuliza kuna nini aliniambia haelewi isipokuwa alitumwa na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Serikali la Daily Graphic, Kofi Bedu, nililokuwa ninalifanyia kazi kunichukua.

Nilipata mawazo mengi, lakini lililotawala fikra zangu ni kumetokea jambo katika familia yangu Zanzibar. Nilimtaka samahani sahiba wangu, Mzee Ahmed Mohamed Polo (baba wa Mohamed Polo) aliyeibuka baada ya kuondoka Ghana kuwa mchezaji nyota wa soka wa nchi hiyo, Ahmed Mohamed Polo.

Huyu bwana alikuwa jirani yangu Barabara ya Adabraka, Accra na alikuja nyumbani kunisalimia baada ya kufahamu nimerudi safari ya wiki moja Nigeria.Niliondoka na dereva na nilipofika ofisini nilikwenda moja kwa moja ofisi ya Kofi Bedu.Baada ya kusalimiana nilimuuliza kama nyumbani Tanzania ni salama aliniambia : “Usiwe na wasi, nilichokuitia ni kwamba kesho Hearts na Kotoko wanacheza na ninataka habari zake ziandikwe na Mtanzania na sio Mghana”.

Baada ya kupumua kwa kuwa sikutarajia ujumbe kama ule, nilimwambia: “Unanielewa, mimi jembe naliita jembe na sio kijiko cha kuchota mchanga. Kama Kotoko itaboronga nitaandika kama nilivyouona mchezo.” Kofi ambaye ni wa Kabila la Ashanti na kwao ni Kumasi, makao makuu ya timu ya Kotoko, alikuwa mjumbe wa kamati ya uongozi ya timu hiyo na hakuficha mapenzi yake.

Lakini kama yalivyokuwa mapenzi ya Mhariri Mtendaji wa Daily News wawakati ule, marehemu Sammy Mdee kwa Yanga, Kofi hakuingilia kitengo cha michezo cha gazeti kilipoandika habari za Kotoko.

“Upo huru, fanya kazi yako na ripoti yako ikiiponda Kotoko sitakuwekea vikwazo vya posho,” aliniambia huku akitabasamu. Lakini hakusita kuelezea hisia zake kwa kuniambia alikuwa na imani Kotoko ingeshinda. Alisema hakutaka mtu mwingine ofisini aandike habari za mchezo ule kwa sababu hata angeandika vipi angeambiwa ameshabikia Kotoko au Hearts.

Niliporudi nyumbani nilikwenda kwa Mzee Polo. Aliitwa Polo kwa vile alisakata mchezo huo wa mpira ambapo mchezaji hupanda farasi. Mzee Ahmed ambaye alikuwa ndio kwanza amestaafu kuichezea Hearts nilimkuta na mwanawe Ahmed aliyekuwa kama na umri wa miaka 17 hivi ambaye baadaye aliichezea Hearts na baadaye kuwa kocha wa timu hiyo.

Nilipomuleleza nilichoitiwa ofisini Mzee Polo aliniambia: ”The last time they fixed us oooh… this time they go die...they will die inside,” akimaanisha: “Mra ya mwisho walitufunga, lakini safari hii watakufa… watakiona cha mtema kuni.”

Nilimtaka asubiri filimbi ya mwisho, lakini wakifungwa asininyime banku (ugali uliovunda unaotumika Ghana).

Mke wake, Bi. Khadija, alicheka na kuniambia hatoninyima banku. Usiku ule kila pembe ya Accra watu walizungumzia pambano la mahasimu hao, kama ilivyo Dar es Salaam siku ya mkesha wa mchezo wa Simba na Yanga.

Wanaume, wanawake, wazee, vijana na watoto walivaa sare za timu zao na magari, pikipipi na baiskeli zilipambwa bendera za Kotoko na Hearts.Siku ya pili watu walimiminika uwanjani tokea alfajiri na ilipofika saa 8 uwanja ulifurika na polisi walizuwia watu zaidi wasiingie.

Nilipofika uwanjani saa 9 pamoja na Watanzania wenzangu waliokuwepo Ghana wakati ule, Kambona) (aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Utalii na Bugingo (alikuwa mwalimu Chuo Kikuu cha Achimota, Ghana) niligundua waamuzi walitoka nchi jirani ya Togo kwa vile klabu zote mbili zilimkataa kila mwamuzi waliyepangiwa.

Timu zilipongia uwanjani niliona Kotoko wakiwa na vijana kama wanne wadogo ambao nilikuwa sijawawaona kabla kuchezea timu hiyo. Wakati mashabiki wa Kotoko walishika tama na kuona viongozi waowalifanya mzaha wenzao wa Hearts waliigiza kilio cha mtoto mchanga kuwakebehi watani wao.

Mtangazaji wa Radio Ghana, Kwesi Armah, aliniambia: “Kotoko wanafanya utani. Huu sio mchezo wa watoto,” nilimwambia huenda watoto ni washindikizaji na tugesubiri mchezokuanza. Badaaye niliona wawili wakiwemo katika kikosi kilichoingia kucheza. Haikuchukua muda niligundua Kotoko walikuwa na haki ya kujiamini kwakuwachezesha wale vijana.

Mmoja wao ni Karim Abdu Razak aliyekuwa na miaka kama 16. Alilisakata kabumbu kwa kujiamini na kumchezesha shere nahodha mahiri wa Hearts Mama Acquah (alifariki 2006). Mwanawe Mama Acquah alikuwa katika kikosi cha Ghana kilichocheza fainali za AFCON zilizofanyika Misri karibuni.

Abdul Razak alishirikiana vizuri na wachezaji waliomzidi umri, wengine wenye umri wa baba yake. Alifunga bao moja na kuwa chanzo cha bao jengine katika ushindi wa 2-1 wa Kotoko. Utani uliofuata baadaye unaweza kuandikiwa kitabu, lakini kwamuhtasari wapo waliokwenda makaburini kufurahia ushindi na jamaa zao waliotangulia mbele ya haki.

Usiku ule, pamoja na Mwandishi wa Gazeti la Daily Graphic, Dan Tetteh, nilitembelea makaburi ya Kokomlemlele, nje kidogo ya Accra. Niliyoyakuta yalinishangaza. Vikaratasi vilivyokuwa Kotoko 2 Hearts 1 vilibandikwa kwenye makaburi.

Miezi michache baada ya kuondoka Ghana nilisikia Abdul Razak alivyong’ara na kuitwa ‘Golden Boy’ (Mtoto wa Dhahabu). Jina la ‘Golden Boy’ lilikuja kutumia kumueleza mchezaji mashuhuriwa Tanzania, Zamoyoni Mogella. Abdul Razak alitajwa mmoja wa wachezaji bora wa Ghana na kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Afrika wa mwaka 1978, akiwa na miaka 22.

Aliisaidia Ghana kubeba Kombe la Mataifa la Afrika 1978 na aliichezea Ghana michezo 70 ya kimataifa na kuifungia mabao 25.

Wakati mmoja ilisemekana kutaka kujiunga na Hearts kutokana na urafiki wake na nahodha wa Kotoko, Mama Acquah aliyefuatana naye msikitini na kufanya ibada asubuhi.

Alipoulizwa lini angejiunga na Hearts alisema: “Kuwa na urafiki na wachezaji wa Hearts kusiwe nongwa. Siku nitakayoamua kuichezea Hearts ndio Mama Ackwah atajiunga na Kotoko.”

Katikati ya miaka ya 1980, Abdul Razak alikwenda Marekani kujiunga na New York Cosmos na kujumuika na Franz Beckenbauer wa Ujerumani naCarlos Alberto wa Brazil.

Baadaye alichezea klabu za nchi za Ghuba, Misri na Ivory Coast.Abdul Razak alizaliwa Kumasi na kuwa kinara tangu mdogo alipochezea shule ya msingi ya Asem. Klabu yake kubwa ya kwanza likuwa Cornerstones mwaka 1972.

Alipostaafu alifundisha klabu za Togo na Benin na mwaka 2000 alichaguliwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ghana, lakini alikaa nayo kwa muda mfupi na kwenda Mali kuifundisha klabu ya Stade Malien.

Alichaguliwa kocha wa Kotoko mwaka 2003 na kuiwezesha kuwa mabingwa baada ya kuukosa kwa miaka 10.

Mwandishi wa habari wa Ghana aliyekuja Tanzania kufanya kazi na Daily News kama mimi nilivyokwenda Ghana, Kwamena Aponsah, aliniambia Abdul Razak baada ya kustaafu alifundisha soka watoto wadogo.

Vilevile ni mmoja wa washauri wa timu ya Ghana, pamoja na mchezaji wa zamani wa Kotoko, Malik Jabir aliyekuja kucheza Tanzania siku Kotoko ilipokutana na Yanga.

Wote wawili walisafiri na Black Stars katika fainali za AFCON zilizofanyika Misri hivi karibuni.

Siku hizi Abdul Razak hutembelea sehemu mbalimbali za Ghana kutoa mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa vijana, lakini hivi karibuni alikwenda Togo kuifundisha klabu ya daraja la pili Etoile Filante. Huyu ni mchezaji ambaye Kotoko, Ghana na Afrika itamkumbuka.