Eti walibebwa?

Ajibu wa Simba na Donald Ngoma wa Yanga
Muktasari:
KUNA ubishi unaendelea mtaani juu ya uhalali wa Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu. Kuna wale ambao wanaona Yanga alistahili na wengine wanabisha. Ubaya ni kwamba baadhi ya mashabiki wa Simba wanaamini kuwa timu yao iko vizuri pengine hata kuliko Yanga, lakini haijawa tu na bahati ya kutwaa ubingwa.
KUNA ubishi unaendelea mtaani juu ya uhalali wa Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu. Kuna wale ambao wanaona Yanga alistahili na wengine wanabisha. Zaidi ni kwamba baadhi ya mashabiki wa Simba wanaamini kuwa timu yao iko vizuri pengine hata kuliko Yanga, lakini haijawa tu na bahati ya kutwaa ubingwa.
Simba ilipoteza mechi zote dhidi ya Yanga, ikapoteza na Toto Africa hata na Mwadui juzi kwenye Uwanja wa Taifa. Ni pointi nyingi ilizopoteza ambazo zilichangia kuibeba Yanga. Hebu tuangalie nafasi moja moja ya timu hizo uwanjani halafu tuzioanishe.
Hebu angalia hao wachezaji halafu utafakari je, ni kweli Yanga walibebwa au ni Simba walibebwa msimu huu?
ANGBAN VS DIDA
Raia wa Ivory Coast, Vincent Angban amekuwa tegemeo kubwa katika kulinda lango la Simba msimu huu tangu alipofanikiwa kuingia kikosi cha kwanza akimpoka namba Manyika Peter, ambaye hakuonyesha kiwango cha kuvutia kwenye mechi za mwanzoni mwa mzunguko wa kwanza. Angban licha ya kutofahamu vizuri lugha za kiingereza na kiswahili, ana uwezo mkubwa wa kupanga mabeki wake na kuokoa mashambulizi ya ana kwa ana. Tatizo lake kubwa ni tabia yake ya kupenda kutokea mipira pamoja na kutokuwa na hesabu nzuri kwenye kuokoa krosi. Lakini amefanya kazi kubwa sana kuinusuru Simba licha ya kwamba, maji yalikuja kuzidi unga.
Kama ilivyo kwa Angban, Dida naye ana uwezo mkubwa wa kupanga mabeki. Pia ana ustadi wa hali ya juu katika kuokoa krosi na kona akichagizwa na umbo refu na wepesi wa mwili wake. Kasoro ya Dida ni kujisahau wakati mwingine pindi anapokuwa golini, tatizo ambalo hupelekea kufungwa mabao yasiyotarajiwa. Uimara wa mabeki wake ulimbeba msimu huu.
ABDUL VS KESSY
Juma Abdul ana uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi na kupiga krosi ambazo zimekuwa zikitumiwa vilivyo na washambuliaji wa Yanga katika kufumania nyavu za timu pinzani.
Pia ni miongoni mwa mabeki wenye sifa ya ziada ya kufumania nyavu za timu pinzani kutokana na uwezo wake wa kupiga mashuti makali.
Tatizo linalomkabili Juma Abdul ni majeraha ya mara kwa mara ambayo wakati mwingine humfanya ashindwe kumaliza dakika tisini za mchezo.
Kwa upande wa Simba mchezaji aliyecheza nafasi ya beki wa kulia kwa muda mrefu ni Hassan Kessy, ambaye ana kasi kubwa inayomfanya aweze kwenda mbele kusaidia mashambulizi na kurudi nyuma kwa haraka kuzuia.
Hata hivyo, ana tatizo la kupiga krosi na pasi za mwisho pale anapokwenda kusaidia mashambulizi pamoja na tatizo la kujisahau hasa anapopanda mbele. Kessy taarifa rasmi ni kwamba ameshasaini Yanga, je, atauweza mziki wa Juma Abdul au atahama namba?Tusubiri.
OSCAR VS TSHABALALA
Oscar Joshua ndiye anayecheza nafasi ya beki wa kushoto ya Yanga kwa sasa. Umbo lake refu na mwili uliojengeka umemfanya awe na uwezo wa kuwadhibiti washambuliaji na mawinga wengi anaokabiliana nao ingawa ana tatizo la kushindwa kuwadhibiti mawinga wenye kasi kutokana na wakati fulani kuwa mzito.
Simba wao wana Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ni mwepesi, anaweza kupanda kwa haraka kusaidia mashambulizi kupitia krosi zake na pia ana miguu kama sumaku inayoweza kuutuliza mpira unaokuja kwenye kimo chochote. Pamoja na hayo, umbo lake fupi limekuwa likimpa wakati mgumu kukabiliana na washambuliaji warefu na wenye maumbo makubwa.
JUUKO VS CANNAVARO
Mganda Murshid Juuko, ni mtaalamu wa kuokoa mipira ya juu akisaidiwa na urefu wake, ana uwezo wa kupanga mabeki wenzake pamoja na kuwahamasisha kupambana.
Kasoro kubwa ya Murshid ni tabia yake ya kucheza rafu hasa kupiga viwiko wachezaji wa timu pinzani huku pia akiwa na tatizo la kutokuwa na kasi pindi anapokuwa uwanjani. Alicheza mechi nyingi msimu huu.
Kwa upande wa Cannavaro, ana sifa ya kupiga vichwa, kusaidia mashambulizi hasa pale Yanga inapopata kona au faulo huku pia akiwa na nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja na ni mzoefu sana. Changamoto ya Cannavaro ni tabia yake ya kubutua ovyo mipira hasa pale Yanga inapotangulia kupata bao, jambo linalowapa nafasi wapinzani kuishambulia timu hiyo.
YONDANI VS LUFUNGA
Kelvin Yondani anabebwa na kigezo cha utulivu hali ya kujiamini inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uzoefu aliokuwa nao uliotokana na kucheza kwake mechi nyingi akiwa Simba, Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’. Kinachomwangusha Yondani ni tabia yake ya kucheza rafu zisizo na sababu pamoja na kupenda kuzozana na wachezaji wa timu pinzani.
Kwa sasa mchezaji anayecheza nafasi hiyo kwa Simba ni Novat Lufunga, ambaye amesajiliwa kwenye kipindi cha usajili wa dirisha dogo. Lufunga anabebwa na umbo lake refu linalomsaidia kumudu kuokoa mipira ya juu na pia kupiga ‘tackling’ washambuliaji wa timu pinzani ili wasilete madhara langoni mwake. Kama ilivyo kwa Juuko, Lufunga naye ni mzito na amekuwa akisumbuliwa na washambuliaji wenye kasi.
KAMUSOKO VS MAJABVI
Wazimbwabwe hao wawili wamekuwa nguzo imara kwenye nafasi ya kiungo wa ulinzi ya Simba na Yanga. Kamusoko ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao ingawa ana tatizo la kutegea kukaba pindi timu inapokuwa haina mpira.
Majabvi licha ya uwezo mkubwa wa kukaba na kuzima viungo washambuliaji wa timu pinzani, amekuwa hana uwezo mkubwa wa kupeleka mbele timu kutokana na kujikita kwake kwenye kuzuia muda mwingi wa mchezo.
MSUVA/MKUDE
Katika winga ya kulia, Yanga imekuwa ikimtegemea zaidi Saimon Msuva ambaye amecheza mechi 23 za Ligi Kuu msimu huu. Msuva amekuwa mzuri katika mipira ya krosi na pia katika kufunga akiwa na mabao nane mpaka sasa.
Hata hivyo winga huyo amekuwa pia akipoteza nafasi nyingi.
Simba mara nyingi imekuwa haichezeshi winga wa moja kwa moja kutokana na mfumo wao wa kutumia viungo watatu. Kutokana na hali hiyo kiungo Jonas Mkude ndiye amekuwa akicheza kama winga feki.
Mkude amekuwa msingi mkubwa wa Simba msimu huu, lakini amepunguza kasi ya mashambulizi kutokana na mara nyingi kucheza katikati.
NIYONZIMA/KAZIMOTO
Kwa upande wa Yanga kiungo mshambuliaji, Haruna Niyonzima licha ya kukosekana katika baadhi ya mechi za katikati ya msimu, amekuwa mchezaji muhimu katika nafasi hiyo. Niyonzima amekuwa akicheza mbele ya Kamusoko na kuufanya mpira kuwa rahisi katika eneo la mbele. Anakochifanya Niyonzima ni kupeleka mipira kwa mawinga wa timu hiyo Msuva na Deus Kaseke ambao wamekuwa wakipiga krosi za maana. Ni mara chache sana kwa Niyonzima kupiga pasi za kupenyeza.
Kiungo mwenye kesi ya kumpiga mwandishi wa kampuni Mwananchi, Mwanahiba Richard, Mwinyi Kazimoto ndiyo amekuwa akipewa majukumu ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo. Kazimoto, ambaye amekuwa nje ya uwanja tangu alipoumia mwezi Machi, amekuwa akiifanya kazi ya ufungaji hasa kwa straika Hamis Kiiza kuwa nyepesi.
TAMBWE/KIIZA
Miongoni mwa wachezaji hatari zaidi Ligi Kuu msimu huu ni mastraika Amissi Tambwe wa Yanga na Hamis Kiiza wa Simba.
Mastraika wote hao wawili ni waviziaji wazuri, wanajua kucheza na nafasi pamoja na kufunga. Tambwe anaongoza ligi kuu akiwa na mabao 20 wakati Kiiza ana mabao 19, wote wamefanya vizuri.
Tofauti yao ni kwamba Tambwe kwa sasa ameimarika zaidi na anarudi nyuma kusaidia kukaba na kupandisha mipira. Sio Yule Tambwe aliyezoeleka kuwa eneo la hatari kwa muda wote wa mechi.
Kiiza mbali na kufunga sio mzuri katika kukaba na kusaidia kupandisha mashambulizi pindi timu yake inapokuwa inacheza chini. Hana wakati mzuri kwa sasa kutokana na kutofautiana na kocha wake, Jackson Mayanja.
NGOMA/AJIBU
Donald Ngoma ndiye mchezaji wa Yanga aliyehusika katika mabao mengi zaidi msimu huu. Amefunga mara 16 na amehusika katika kusaidia mabao mengine nane.
Ananyumbulika, anacheza na nafasi na ni msumbufu. Yanga imepata penalti saba msimu huu na tatu kati ya hizo zimetokana na Ngoma. Wachezaji wa timu pinzani wamekuwa wakichukua kadi nyekundu za kutosha kutokana na kushindwa kumkaba vizuri straika huyo.
Simba kwa msimu huu imekuwa ikimtegemea zaidi Ibrahim Ajibu kama namba 10 wao. Ajibu amejitahidi kwa kufunga mabao tisa msimu huu huku akipika mabao mengine kadhaa yaliyofungwa na timu yake.
Ajibu ana uwezo mkubwa wa kupiga chenga, kufungua timu na kutengeneza nafasi. Kikubwa anachokosa mshambuliaji huyo ni uwezo wa kupambana kwani, muda mwingi hanaonekana amechoka na ana hasira za karibu kama zilizomgharimu juzi akaonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Mwadui ya Shinyanga na Simba ikapoteza mchezo.
KASEKE/MWALYANZI
Deus Kaseke ameitawala winga ya kushoto ya Yanga kwa takribani msimu mzima. Amekuwa akifunguka na kutengeneza nafasi kwa mastraika wake hasa kwa kujaribu kupenyeza mipira na pia kwenye krosi. Kaseke amekuwa vizuri pia katika kukaba na kusaidia kupandisha timu.
Simba imekuwa ikimtegemea Peter Mwalyanzi zaidi katika winga ya kushoto msimu huu licha ya nyakati fulani kukosekana kikosini hapo. Mwalyanzi amecheza mechi zaidi ya 16 msimu huu na kuwa straika wa pembeni aliyeitumikia nafasi hiyo kwa muda mwingi zaidi.
Kiungo huyo amekuwa akipata wakati mgumu katika kutengeneza mashambulizi kutokea upande wake licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga chenga.