DUNIANI KUNA SOKA, TANZANIA KUNA SIMBA NA YANGA
WAKATI fulani, mwandishi wa habari Ezekiel Kamwaga, amepata kusimulia kisa fulani ambacho alikiongoza kipindi alipokuwa Katibu Mkuu wa Simba. Alisema, alipokuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, timu hiyo ilikuwa na ukata wa hali ya juu.
Yanga wakiwa na mfadhili wao Yusuf Manji, walikuwa wanatamba mno. Simba wakawa wanyonge sana. Yanga wanashinda mechi, wanachukua ubingwa. Wanasafiri sana nje kuweka kambi za kujiandaa na msimu wa ligi. Wanashiriki michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Na wakati huo, Yanga walikuwa wanachuana na Azam. Unakuta Yanga wakishinda ubingwa, Azam wanamaliza nafasi ya pili. Azam na Yanga wakahodhi tiketi za kucheza michuano ya CAF. Hivyo, Yanga na Azam wakawa na mengi ya kufurahia kuhusu mafanikio ya timu zao.
Waweke Azam pembeni, maana kwa kawaida, Kibongobongo, Simba hawawezi kuteswa sana na mafanikio ya Azam, bali Yanga. Kama Azam watakuwa wanashinda na kuchukua ubingwa, halafu Yanga nao wanakosa, maumivu kwa Simba hayawi makubwa. Kadhalika, mafanikio ya Azam hayataitesa Yanga kama Simba nayo inapigika.
Kwa ufafanuzi huo, tunashika hili, kwamba Simba walikuwa wakiteswa sana na mafanikio ya Yanga. Mashabiki wa Yanga waliwaita wenzao wa Simba kila jina. Mashabiki wa Simba hawakuwa na la kusherehekea. Yao macho tu!
Ndipo Kamwaga na wenzake wakaibuka na hamasa ya kwenda kufyeka uwanja wao wa mazoezi, uliopo Bunju. Ni huo ambao kwa sasa unaitwa “MO Simba Arena”. Akina Kamwaga wakawahamasisha mashabiki wa Simba kwenda Bunju kupalilia uwanja wao.
Kwa Simba ikawa siku nzuri. Mashabiki wakapata kitu cha kujionyesha na kutambia. Kwamba wao ubingwa walishachukua sana, kwa hiyo walijielekeza kwenye uwanja wao. Angalau hilo kwa Wanasimba wengi, liligeuka faraja.
Je, ni kweli Simba hawakuhitaji ubingwa au kushinda mechi kama wenzao Yanga? Jibu ni hapana, Simba walitamani sana mafanikio ambayo Yanga walikuwa nayo. Walikuwa na nguvu ya kusajili wachezaji ghali, Afrika mpaka Brazil. Simba hata wachezaji wenyeji walinyang’anywa.
Ondoka nyakati hizo, huu ni mwaka 2020. Simba wameshachukua kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu mfululizo. Uongozi wa timu chini ya mwekezaji, Mohammed Dewji ‘MO’, umetulia. Unapanga mambo yake bila presha.
Simba fedha zao sio za kuungaunga. Wanazo na wanazitumia kufanikisha malengo ambayo wanajiwekea. Wanasajili wachezaji ambao wasifu wao hautii shaka. Rekodi zao zinawabeba. Usajili unafanyika kwa wakati.
Namna wanavyoacha wachezaji na wanavyosajili, unaona ufundi unazingatiwa. Tamasha la klabu, Simba Day, linaandaliwa kwa ubora na linaboreshwa kila mwaka. Viongozi na mwekezaji wa Simba wanadhihirisha njaa yao ya mafanikio. Mashabiki wa Simba huwaoni wakisonya hovyo na kutukana wachezaji au viongozi. Wana utulivu.
Mashabiki wa Simba huwaoni kama wanakumbuka nyakati za kuitwa “Wa Matopeni!”. Ni kipindi hiki, Yanga wanaitwa kila jina, “Utopolo” limekuwa kubwa. Yale mengine kama “Vyura FC”, yapo sana. Huwaoni Yanga wakijiita “Wakimataifa” tena. Kwa sasa Simba ndio wanaosafiri sana angani kuvuka mipaka ya nchi.
Kama ambavyo wakati ule Simba wakiwa hohehahe, lakini wakaona wajifariji kwa kwenda Bunju kufyeka uwanja wao, ndivyo na sasa Yanga walivyo. Hawaachi Simba wajidai na mafanikio yao, bali nao wanaamua kufanya jambo.
Injinia Hersi wa GSM, kampuni inayoifadhili Yanga, anatua Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akiwa na wachezaji wawili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe, anakutana na mapokezi ya kichifu.
Hersi anabebwa kwenye kiti cha miti mithili ya wafalme wa zamani. Kisha, wachezaji waliosajiliwa na kuletwa nchini na Hersi kutokea DRC, wanapakizwa kwenye gari la wazi, kisha wanapitishwa Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi, yalipo maskani ya Simba, ili kuwaonyesha kuwa wao sio wanyonge.
Yanga wanaleta mchezaji kutoka Angola. Anapata mapokezi makubwa kuliko yale ambayo Cristiano Ronaldo aliyopata Turin, alipojiunga na Juventus. Asilimia kubwa ya mashabiki wa Yanga waliokwenda kumlaki mchezaji wao mpya kutoka Angola, wala hawamjui, hawatambui rekodi zake. Unadhani wanajali?
Mashabiki wa Yanga hawana mambo mengi ya kufurahia dhidi ya watani wao, Simba. Wanazidiwa ndani ya uwanja na hata mbinu za nje ya uwanja. Hawana muda mrefu tangu walipofungwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho, Tanzania Bara, kisha mchezaji wao kipenzi, Bernard Morrison, akatwaliwa na Simba.
Kwa vile furaha kuu ya timu ni kushinda mechi na kuchukua ubingwa, ambayo kwa Tanzania imehodhiwa na Simba hivi sasa, Yanga wanaibuka na njia mbadala za kufurahia timu yao. Ni kupitia mapokezi yenye kupitiliza kwa wachezaji wao na Hersi, ambaye ni wa GSM, kampuni inayoidhamini timu yao.
Kupokea wachezaji kwa namna ambavyo, Carlinhos kutoka Angola, alivyopokewa ni ya kumkuza mno mchezaji. Unaweza kumfanya mchezaji ajihisi kuwa yeye ni mkubwa kuliko timu. Si sawa! Hata hivyo, unadhani Yanga walifanya bahati mbaya? Walitaka kuwatambia wapinzani wao, Simba, kwamba wao si wanyonge.
Ni kwa sababu duniani kuna soka. Timu hupambana kuwa bora hasa ndani ya uwanja, lakini Tanzania kuna Simba na Yanga. Maonesho ya tambo kwa timu hizo mbili ni muhimu kuliko kitu kingine chochote. Na wachezaji wa kigeni wanaposajiliwa, haraka sana wanagundua kuwa Tanzania si soka, bali Simba na Yanga.