Dubu Baya atajwa kuibukia Wiki ya Mwananchi
Muktasari:
- Mwaka huu 2026, Yanga inakwenda kusherehekea Tamasha la Wiki ya Mwananchi ikiwa ni msimu wa nane tangu kuanza kwake 2018.
YANGA SC imeanza kuweka mambo sawa kuelekea tamasha lake la Wiki ya Mwananchi litakalofanyika Agosti 9, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku ikielezwa klabu hiyo imefungua mazungumzo na msanii mkongwe, Dudu Baya ili apafomu siku hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo inalenga kufanya tamasha litakalowagusa mashabiki wake wa rika zote, hivyo mbali na wasanii wa kizazi kipya, pia imeona umuhimu wa kuwapa nafasi wakongwe wa muziki ambao nyimbo zao zimeishi kwa muda mrefu.
Kamwe amesema mazungumzo na Dudu Baya yanaendelea, huku akieleza kuwa uwepo wa msanii huyo pamoja na wakongwe wengine utasaidia kufanya tamasha hilo liwe na ladha tofauti na kuwakutanisha mashabiki wa Yanga wenye umri tofauti.
Amesema, Yanga imefanya uchambuzi wa aina ya burudani ambayo inaweza kuwafaa mashabiki wake, kuanzia vijana wanaofuatilia muziki wa kizazi cha sasa hadi wale wenye umri mkubwa ambao wamelelewa na muziki wa zamani.
“Tumefanya uchambuzi mzuri na tutawatangazia orodha nzuri ambayo itakuwa sawa kulingana na umri kila mtu akapate burudani iliyo sahihi,” amesema Kamwe.
Kwenye tamasha la mwaka jana, msanii kutoka Wasafi, Zuhura Othman maarufu Zuchu ndiye alikuwa msanii mkuu aliyepafomu kwenye tamasha hilo. Wengine baadhi waliokiwasha alikuwa D Voice na Dogo Paten.
Mbali na burudani, Kamwe amezungumzia timu watakayocheza nayo mechi ya kirafiki kwenye tamasha hilo.
"Timu tayari ipo lakini tulipata tabu kuwashawishi, walituuliza hadi kikosi tutakachoingia nacho sisi tukawaambia hilo ni jukumu la kocha, ukawaondoa wasiwasi kuwa hiyo ni mechi ya kirafiki tutacheza kirafiki tu," amesema Kamwe.
Mwaka huu 2026, Yanga inakwenda kusherehekea Tamasha la Wiki ya Mwananchi ikiwa ni msimu wa nane tangu kuanza kwake 2018.